Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe.Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameongoza Mkutano wa dharura wa
Utatu wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi, na Usalama uliofanyika
jijini Harare, Zimbabwe tarehe 19 Novemba 2024.
Mawaziri wa Jumuiya ya SADC walijadiliana kwa
pamoja na kuipitisha Ajenda ya Kuangazia Hali ya Usalama Mashariki mwa Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo na njia madhubuti za kukabiliana na changamoto hiyo.
Ajenda ya Mkutano huo itaenda kujadiliwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na
Serikali ili kutolea mwongozo na maamuzi.
Wajumbe wa
Tanzania walioshiriki Mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Mhe. Dkt Stergomena Tax, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt.Samwel Shelukindo, Mkuu wa Majeshi
ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe.
Mhe. Dkt Tax nae alipata nafasi ya kuchangia
mada, na alisisitiza nia ya Tanzania kuunga mkono juhudi za kutafuta suluhu ya
kudumu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Aidha, Dkt Tax amezisihi nchi wanachama umuhimu
wa kutekeleza maagizo yanayotolewa na Wakuu wa Nchi ili kufikia malengo ya
kuleta Amani na Usalama katika Kanda.
Waziri Kombo amebainisha kua Tanzania itaendelea
kusimama bega kwa bega kushirikiana na Nchi wanachama ili ajenda ya kurudisha
Amani na Usalama DRC iweze kufikiwa.
" Mshikamano wetu ndio nguzo yetu
itakayosaidia kuleta suluhu ya kudumu na kurejesha Amani na Usalama kwa ndugu
zetu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ".
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Balozi Mahmoud Thabit Kombo (wa pili kushoto), akiwa na viongozi wengine katika mkutano huo.
0 Comments