SERIKALI ZANZIBAR YATAIFISHA MALI ZA WATUHUMIWA WA DAWA ZA KULEVYA

Subscribe Us

SERIKALI ZANZIBAR YATAIFISHA MALI ZA WATUHUMIWA WA DAWA ZA KULEVYA


Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanal Buruhan Zuberi Nassor akizungumza na  Waandishi wa Habari kuhusiana na kutaifisha Mali za Watuhumiwa  wa Dawa za Kulevya  zenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 900 katika mkutano uliofanyika Novemba 11, 2024  Kilimani Zanzibar. (PICHA NA YUSSUF SIMAI/MAELEZO ZNAIZBAR).

...................................

Na Khadija Khamis. Maelezo. 

Zaidi ya Tsh. milioni mia 9 zimetaifishwa na Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya Zanzibar  na kuwa mali ya Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na kupatikana kwa njia ya haramu.

Akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari huko Ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Kanal Burhan Zubeir Nassor amesema zoezi hilo limefanyika kwa mujibu wa sheria namba 8 ya mwaka 2021 ya Mamlaka ya kuthibiti na kupambana na Dawa ya kulevya Zanzibar.

Amesema Mamlaka imetaifisha Kiwanja kilichopo Matemwe na Honda ya aina ya Click, vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 422,126, Saleh Khamis Basmani Mkaazi wa Chukwani Wilaya ya Magharibi B na Mke wake Dawari Abas Fakih na kusema Mamlaka inaendelea kuchunguza mali nyengine zilizomo ndani na nje ya Nchi.

Aidha amemtaja Mtuhumiwa mwengine kuwa ni Mohamed Abdalla Juma Mkaazi wa Michenzani Wilaya ya Mjini ambae ni  Mtumishi wa Serikali katika Kada ya Sheria ambapo ametaifishwa Kiwanja kilichopo Bweleo Wilaya ya Magharibi B, chenye thamani ya Sh. Milioni 35 baada ya kubainika anashirikiana na Saleh Khamis Basmani katika utakatishaji wa fedha na kuingiza Simu zinazotumika kufanya uhalifu kutoka Nchini Afghanistan.

Hata hivyo amesema Mamlaka imetaifisha Gari aina ya Toyota na Nyumba zilizopo Paje Wilaya ya Kusini, zinazomilikiwa na Andrea Scoph Fres, Raia wa Ujerumani, zenye thamani ya Sh. Milioni 518,926 mara baada ya kukamatwa na Mashine ya kisasa ya kuoteshea Bangi, Polo moja la Bangi pamoja na Shamba la Bangi huko Paje Mkoa wa Kusini Unguja.

Mbali na hayo Kanal Burhan amesema Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya kuthibiti na kupambana na Dawa za kulevya inaendelea kuwatafuta wanaojishughulisha na Dawa hizo ili kunusuru Vijana na utumiaji wa Dawa hizo.

Itakumbukwa mnamo Aprili 22, 2024 Mamlaka hiyo ilitangaza kutaifisha mali haramu ya Dawa ya kulevya ya Saleh Khamis Basman, Mkaazi wa Chukwani na Mke wake Dawari Fakih zenye thamani ya Tsh Bilion 15.3.

Post a Comment

0 Comments