RAIS SAMIA ANAVYOJIVUNIA SAFU BORA YA VIONGOZI CCM IKIONGOZWA NA DKT. NCHIMBI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 28 May 2025

RAIS SAMIA ANAVYOJIVUNIA SAFU BORA YA VIONGOZI CCM IKIONGOZWA NA DKT. NCHIMBI

 Ilani ya CCM 2025/2030 watanzania waisubiri kwa hamu 

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akipeana mkono na Katibu Mkuu wa chama hicho wakati kilipopitisha azimio la kumteua kuwa mgombea wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu. Azimio hilo pia lilimpitisha Rais wa Zanzibar Dkt, Hussein Ali Mwinyi kuwa mgombea wa Urais Zanzibar na Katibu Mkuu wa CCM Taifa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa Dkt. Samia. CCM chini ya viongozi hawa ndio kinatekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/ 2025 ambayo imafanya vizuri na taarifa rasmi ya utekelezaji wa ilani hiyo itatolewa Mei 29, 2025 katika mkutano mkuu maalumu wa chama hicho utakaofanyika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center Jijini Dodoma ambapo pia ilani ya chama hicho ya 2025/2030 itazinduliwa. 

............................................... 

IKIWA imebaki miezi mitano Tanzania kufanya Uchaguzi Mkuu 2025 kuchagua Rais,Wabunge na Madiwani, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinajivunia mafanikio lukuki kutokana na kutekelezwa vyema ilani ya chama hicho ya mwaka 2020/2025. 

Mafanikio ya CCM yamechagizwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameunda timu bora ya viongozi wakuu wa chama na serikali katika kuwaletea maendeleo Watanzania. 

Baadhi ya viongozi ambao  ni timu bora ya ushindi ndani ya chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu ni Katibu Mkuu Balozi Dk.Emmanuel Nchimbi, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Gabriel Makalla,  Katibu wa NEC Idara ya Organaizeaheni, Issa Gavu na Katibu Mkuu wa UVCCM, Jokate Mwagelo  na Ally Hapi ambaye ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi. 

Wengine ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi,  Fadhili Magaya (MNEC) na John Mongella ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa, Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM, Mohamed Kawaida na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi (NMEC). 

Kiongozi mwingine ni Mary Chatanda (MCC) ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Katibu wa umoja huo Suzana Kunambi (MNEC) na, Makamu Mwenyekiti wa UWT, Zainab Khamis Shomari (MNEC) . 

Kwa upande wa Zanzibar ni Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye ni  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania. 

Viongozi wengine ni wale wanaosimamia jumuiya zote za chama hicho chini ya wenyeviti na makatibu wa chama hicho kuanzia ngazi ya shina, kata, wilaya na mkoa. 

Viongozi hao wakuu wa chama hicho kupitia jumuiya zao ndio wenye jukumu la kutelemsha chini maelekezo ya kuboresha chama hicho ambacho kimeshika dola na kuwaletea maendeleo wananchi.

Timu hii ya viongozi wa  CCM ambayo inaangaliwa kwa karibu  na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Dkt. Samia chini ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ambaye Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho na Rais wa Awamu ya Nne Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete aliwahi kueleza kuwa chama hicho kimempata katibu mchapakazi na mwenye uzoefu mkubwa. 

“Dtk. Nchimbi ni kiongozi anayekijua chama Cha Mapinduzi vizuri na nimchapa kazi kwa kweli CCM imempata katibu mkuu anayefaa kukiongoza, alisema Dkt. Kikwete wakati katibu mkuu huyo alipofanya ziara Jimbo la Mchinga mkoani Lindi. 

 Dkt. Nchimbi ni Katibu Mkuu wa CCM wa 12 tangu chama hicho kianze kushika hatamu.  

MAKATIBU WA CCM WALIOHUDUMU NAFASI HIYO 

1.Pius Msekwa (1977-1981) 

2.Daudi Mwakawago (1981-1982) 

3.Rashid Kawawa (1982-1990) 

4.Horace Kolimba (1990-1995) 

5.Laurence Gama (1995-1997) 

6.Philip Mangula (1997-2007) 

7.Yusuf Makamba (2007-2011) 

8.Wilson Mukama (2011-2012) 

9.Abdulrahman Kinana (2012-2018) 

10.Bashiru Ally (2018-2021) 

11.Daniel Chongolo (2021-2023)

Makatibu wakuu wote hawa walifanya kazi nzuri na wataendelea kubaki na heshima hiyo kubwa baada ya kulitumia taifa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mchango wao mkubwa na uliotukuka walioutoa kwa Taifa la Tanzania. 

Kwa sasa niseme tu kwamba hatuwezi kuzungumzia siasa za Tanzania bila ya kumtaja Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye ni mbobezi na mwenye uzoefu  mkubwa wa uongozi ndani ya Serikali na katika chama hicho. 

Kupitishwa kwa Rais Dkt. Samia kuwa mgombea urais na kuteuliwa kwa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa ni ishara ya ushindi wa mapema wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi mkuu bila ya kujali wapinzani watamsimamisha nani. 

Hii inatokana na jitihada kubwa iliyofanywa na Rais Samia katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini kwa muda mfupi ikiwa ni kutekeleza ilani ya chama hicho ya 2020/ 2025 ambayo taarifa yake itapokelewa katika mkutano maalumu mkuu wa CCM utakaofanyika Mei 29, 2025 hadi Mei 30, 2025 jijini Dodoma ambapo pia ilani ya chama hicho ya 2025/ 2030 itazinduliwa, 

Kwa upande wa Dkt. kuwa mgombea mwenza kumeyavuruga mapema makundi ndani na nje ya CCM ambayo yangetaka kuwania nafasi hiyo ya urais. 

Sababu kubwa ni kwamba Dkt. Nchimbi anakubalika na wana CCM wengi  wanamtandao vijana na wazee pamoja na wananchi. 

Dkt. Nchimbi kuteuliwa kwake kuwa mgombea mwenza hakuna mashaka kabisa kwani ni mbobezi wa siasa za ushindani hapa nchini na ni kiongozi aliyezaliwa na kulia ndani ya siasa kwani Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi kutoka Wilayaya  Songea ambaye alikuwa ni askari mstaafu wa Jeshi la Polisi wakati anastaafu alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara. 

Mzee Nchimbi pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia kundi la majeshi na baadaye katibu wa CCM wa mkoa, alikoma kushiriki masuala ya kisiasa baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1991. 

Uzoefu na ufanyaji kazi wake  ndio uliomfanya kuaminiwa na kupewa nafasi hiyo kubwa ndani ya chama hicho. 

Dkt. Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya, Elimu yake ya Msingi aliianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 – 1986. 

Dkt. Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Sekondari Uru kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990. 

Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997). 

Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM). 

Dkt.  Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003. 

Alisoma shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya (benki na fedha). 

Dk Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003 – 2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe. 

Dkt. Nchimbi alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge akiwa anaongoza UVCCM. 

Mwaka 2005, aliingia rasmi kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi ambapo akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema. 

Mbogoro  alikuwa mpinzani wake mkuu, lakini kutokana na Dkt. Nchimbi kuwa na wananchi na wana CCM wengi waliokuwa wakihitaji awe mbunge wao alipata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro. 

Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapo pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010. 

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini. Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009. 

Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa Chadema na kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii Dk Nchimbi akipoteza takriban ushindi wa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro. 

Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Rais Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani. 

Baada ya hapo Rais wa Awamu ya Tano Hayati John Pombe Magufuli alimteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazili kabla ya kuhamishiwa Misri na baada ya hapo alirudi nyumbani hadi alipoteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Daniel Chongolo baada ya kujiuzulu. 

BAADHI YA KAZI ALIZOZIFANYA BAADA YA KUTEULIWA KUWA KATIBU MKUU  

Baada ya uteuzi huo Balozi Dkt. Nchimbi alikutana na viongozi wa jumuhiya zote za chama hicho na kupanga mikakati ya kuboresha baadhi ya mambo ndani ya chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya hadhara. 

Mikutano hiyo imekuwa ikitumika kusiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi na kabla ya mikutano hiyo wamekuwa wakitembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali kwa fedha nyingi zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Katika eneo hilo Balozi Dkt. Nchimbi akiwa na Katibu wa Itikadi Uenezi na Mafunzo Amos Makalla ,  Katibu wa NEC Idara ya Organaizeaheni, Issa Gavu na Katibu wa NEC Siasa na uhusiano wa kimataifa wa chama hicho, Rabia Abdallah Hamid tayari wamekwisha fanya ziara hizo karibu mikoa yote na imebaki michache baada ya kuanza na ziara hizo Zanzibar. 

Ziara hizo zimekuwa zikifanywa na viongozi wa jumuiya zote za chama hicho katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar zikifanywa chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania na  Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye ni  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania. 

Aidha ziara hizo zimeonesha kuwa na tija na mafanikio makubwa ndani ya chama hicho kwani wanachama wengi kutoka vyama vya upinzani wameondoka kwenye vyama vyao na kujiunga na CCM. 

Hali hiyo imetokana na kuona  kazi kubwa iliyofanywa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ambayo imewaondolea adha kadha wa kadha. 

Dkt. Nchimbi ambaye anakiongoza chama hicho kisayansi amekwenda mbali zaidi kwa kutoa mafunzo mbalimbali ya uongozi kwa viongozi wa jumuiya za chama hicho kama tulivyoona mafunzo yaliyofanywa kwa UVCCM mkoani Iringa na yale yaliyofanywa kwa wenyeviti wote wa CCM wa wilaya na viongozi wa UWT. 

Mafanikio mengine makubwa ambayo yameonekana ni kongamano  walilolipa jina la kuzima Zote Na kuwasha Za Kijani ambalo lilionesha kuitikiwa na kundi la vijana hata wale wasio wanachama wa chama hicho ambao nao kwa hiyari yao waliamua kujiunga na CCM. 

Tuliliona kongamano hilo lilivyokuwa likifanyika maeneo mbalimbali nchini huku likihudhuriwa na mamia ya vijana Tanzania Bara na Zanzibar. 

Niseme kuwa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi wewe ni zaidi ya yote hakika upo kukiboresha chama kazi ambayo umeachiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Rais Dkt. Samia Suluhu chini ya timu yake hiyo aliyoiunda. 

 Nguvu nyingine ya ushindi wa CCM ni uteuzi wa Stephen Wasira kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara. 

Wasira naye ni mbobezi wa siasa na uongozi hapa nchini ambapo wana CCM wanatarajia makubwa kutoka kwake. 

Stephen Wasira alizaliwa mwaka 1945 katika Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara (ana miaka 70). Alisoma katika shule tatu tofauti, ya kwanza ni Shule ya Msingi Bariri 1956-1959, ya pili ni Shule ya Msingi Nyambitilwa 1960–1961 na kisha akamalizia Shule ya Msingi Kisangwa mwaka 1962 - 1963.  

Kati ya mwaka 1964–1967, Wasira alisoma elimu ya Sekondari katika Chuo cha Ukufunzi Uingereza (British Tutorial College) na kuhitimu kidato cha nne. 

Wakati anasoma sekondari (1965–1967), pia alifanya kazi akiwa msaidizi wa masuala ya maendeleo ya jamii na alipohitimu kidato cha nne alianza kuitumikia Tanu akiwa katibu wa wilaya mwaka 1967-1973.  

Mwaka 1975–1982 alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na mwaka 1982 akateuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania Washington, D.C. Alipokuwa huko alisoma na kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Uchumi na Uhusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Amerika (American University) kilichopo Washington DC mwaka 1982–1985.  

Wasira alisoma Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Umma kati ya mwaka 1985–1986 na aliporejea nchini kuendelea na utumishi wa uwakilishi wa wananchi, aliteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani mwaka 1990-1991.  

Kati ya mwaka 1993–1995 alisoma tena Shahada ya Uzamili ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Amerika.  

Ndani ya chama chake CCM, amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) tangu mwaka 2007 na mwaka 2012 akachaguliwa katika wadhifa huo na tena kwa kura nyingi kuwashinda wajumbe wote wa Tanzania Bara. Lakini pia amekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM tangu mwaka 2011 na tena 2013 hadi sasa.  

WANA CCM WANAMZUNGUMUZIAJE DKT. NCHIMBI  

Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga anasema wanajivunia uwepo wa Dkt. Nchimbi kwa namna alivyouweka sawa mshikamano ndani ya chama.  

Alisema licha ya kuwa ni Katibu Mkuu ni Mwanadiplomasia mbobevu mwenye shahada za hali ya juu na ni  kiongozi asiyetiliwa mashaka kwa sababu uhudumu wake wa muda mrefu kwenye kamati kuu na  halmashauri kuu ya CCM.  

Bananga alisema kutokana na ubobevu wake kuanzia bungeni, ubalozini ndani ya chama na Serikalini kwa maana wizarani amesaidia kuweka mambo vizuri na kwa wao ambao ni watumishi wameona faida yake kwani wale wenye hadhi na  na sifa wamepandishwa madaraja na vyeo.  

“Kutokana na ubobezi wa utendaji kazi amekuwa kiungo madhubuti kati ya chama na Serikali na wakati mwingine amekuwa akiikosoa au kuielekeza kwa mambo ambayo yanakuwa mtambuka akisimama na kuyakataa anapoyaona hayaendi sawa,” alisema Bananga. 

Bananga aliongeza kuwa Dkt. Nchimbi ni kiongozi mwenye kuwiwa kukitumikia chama na Serikali ambaye anafanya kazi bila ya kuwa na makeke na kazi inakwenda vizuri.  

Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Singida, Juma Killimba alianza kwa kuishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani ya miaka mitano kwa utekelezaji mzuri wa ilani ya chama hicho ya 2020/2025 yenye kurasa 303 ambayo iligusa sekta ya maji, afya, elimu, barabara na maeneo mengine ambapo kilimo kilipewa kipaumbele na kutengewa bajeti kubwa ambayo  inakwenda kuondoa ufukara wa wananchi wa Mkoa wa Singida.  

Alisema shughuli zote za maendeleo zimesimamiwa vizuri kuanzia ngazi ya Taifa na CCM chini ya Dkt. Nchimbi na baada ya kuliona hilo ndio maana ikaonekana achaguliwe kuwa mgombea mwenza wa Rais Samia ili akawe msaidizi wake wa karibu na kuweza kuitekeleza ilani ya 2025/ 2030 ambayo ameshiriki kuiandaa.  

“Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020/ 2025 iliyokuwa na kurasa 303 imefanya vizuri sana chini ya Rais Samia na Dkt. Nchimbi ndio maana  kutokana na usimazi huo mzuri Nchimbi ameteuliwa kufanya makubwa zaidi katika utekelezaji wa ilani ya 2025/ 2030 ambayo itazinduliwa kwenye mkutano mkuu maalumu utakaofanyika Jijini Dodoma,” alisema Killimba.  

Mjumbe wa baraza la wazazi na baraza la UVCCM Mkoa wa Singida, Ahmed Misanga alisema Dkt. Nchimbi ni kiongozi mtendaji anayetaka aone matokeo ya kazi kwa haraka na muda mfupi.  

Alisema Dkt. Nchimbi ni mtu anayeamini kwamba maendeleo ni haki ya kila mwananchi ndio maana anafanya vizuuri majukumu yake ya kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM.  

“Katibu mkuu ndiye mtendaji mkuu wa chama ni kama gia boksi ya gari ambayo inalifanya gari litembee na injini ni Mwenyekiti wa chama,” alisema Misanga.  

Misanga alisema anapenda kuona Katibu Mkuu mpya atakaye teuliwa kumrithi Dkt. Nchimbi baada ya kuacha nafasi hiyo kufuatia kuanza  majukumu ya mgombea mwenza wa nafasi ya mgombea urais wa chama hicho Dkt. Samia Suluhu Hassan aige mfano wake ili kuendeleza yale yote yaliyokuwa yakifanywa kwa ajili ya kukiimarisha chama na maendeleo ya wananchi.  

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Siasa CCM Mkoa wa Iringa, Dkt. Tumaini Msowoya anasema Dkt, Nchimbi jambo kubwa alilolifanya ni kujenga utulivu ndani ya chama na kuwa na mshikamano.  

Amesema Dkt. Nchimbi amekuwa mtu wa kuheshimika sana na kuaminiwa kutokana na uongozi wake tangu akiwa Mwenyekiti wa  UVCCM Taifa ambapo alifanya kazi kwa weledi mkubwa hivyo vijana wa CCM wa wakati huo na wasasa wameendelea kumkubali. 

“Kutokana na mambo hayo watu wamejikuta wakiwa na imani na CCM kutokana na jinsi ambavyo anavyokiongoza chama na zaidi jinsi Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa na imani naye na kumpendekeza kuwa mgombea mwenza na mkutano mkuu kumchagua,” alisema Msowoya. 

Mwana CCM Hussein Ramadhani Layya (maarufu Msokolo) mkazi wa Kwamchina Mjini Magharibi Zanzibar amesema kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia na timu yake hiyo amefanya mambo makubwa ya maendeleo kwani kila sekta ameipaisha katika kuitekeleza ilani ya CCM ya 2020/ 2025 na sasa tutegemee makubwa zaidi katika ilani itakayozinduliwa katika mkutano maalumu mkuu utakaofanyika Dodoma.

"Mama huyu kafanya mengi ambayo hayahesabiki na amekifanya chama kuwa na mshikamano mkubwa atapata uushindi mkubwa na wakishindo katika uchguzi mkuu unaokuja kwani hana mpinzani," alisema Msokolo.

Halikadharika kwa upande wa Zanzibar Makamu Mwenyekiti wa CCM na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefanya mapinduzi makubwa ya maendeleo kwani yale yote aliyoyaahidi ameyatekeleza kuanzia sekta ya afya, elimu, maji na barabara ambazo zimejengwa kwa kiwango cha lami katika kila kona.

Alisema mapinduzi mengine makubwa anayoyafanya ni ya kiuchumi wa buluu kwa  kuwekeza katika nyanja mbalimbali.

Akimzungumzia Dkt. Nchimbi amesema amekuwa kiungo kikubwa kwa wanachama wote wa Tanzania Bara na Visiwani na kuelezea kuwa ni kiongozi ambaye ni mnyenyekevu na anayejishusha kwa watu.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa Kata ya Mianzini Mtaa wa Mji Matitu 'A' Mbagala Jijini Dar es Salaam, Hawa Omari anasema CCM kuwapitisha Rais Samia, Rais wa Zanzibar na Dkt. Emmanuel Nchimbi kugombea nafasi za uongozi wa juu haikubahatisha kutokana na viongozi hao kuwa na sifa.

Akimzungumzia Dkt. Nchimbi alisema ni kiongozi wa watu ambaye siyo mtu wa kujikweza ni mnyenyekevu na anayejali maslahi ya wengine.

" Nilitambua kuwa chama chetu kimepata kiongozi mahiri ni pale alipokuwa katika moja ya ziara zake za kuimarisha chama sikumbuki ni mkoa gani aliposema chama hicho hakiwezi kuwa na ujasiri wa kuikosoa Serikali inayoiongoza kama wao wenyewe hawawezi kutimiza wajibu wao," alisema mjumbe huyo.

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Mbiga, Angelo Madundo anasema Dkt. Nchimbi tangu ateuliwe kuwa katibu mkuu wa chama hicho amefanya mapinduzi makubwa.

"Dkt. Nchimbi amekuwa  turufu na lulu kubwa katika kukiunganisha chama na wanachama  ndio sababu ambayo imekifanya chama hicho kuwa cha kisasa zaidi," alisema Madundo.   

Kwa timu hii chini ya magwiji hawa wa siasa nchini CCM itegemee kupata ushindi mnono na wakishindo.

Makala hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba (0754362990) Email dotomwaibale@gmail.com

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Nchimbi.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa na mgombea Mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi pamoja na Mgombea Urais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi baada ya kupitishwa kuwa na mkutano mkuu wa CCM.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira.Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Gabriel Makalla.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) Oganaizesheni, Issa Usi Gavu
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiwa kwenye picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, walipokutana Ikulu Zanzibar Aprili, 14, 2025. Mwingine pichani ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Mohamed Dimwa.
 Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi,  Ally Hapi
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa, John Mongella.
Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM, Mohammed KawaidaKatibu Mkuu wa UVCCM, Jokate Mwagelo
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda (MCC) 
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi akiwa kwenye picha ya pamoja na Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndugu Zainab Shomari.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), Suzani Kunambi.
Wajumbe wakiwa katika moja ya mkutano mkuu wa chama Jjini Dodoma ambapo Mei 29 na Mei 30, 2025 watapokea taarifa ya utekelezaji ya ilani ya CCM ya 2020/ 2025 nakuzindua ilani ya 2025/ 2030.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad