KANUNI YA CHAMA CHA WALIMU TANZANIA (CWT) YAWAVURUGA WALIMU SINGIDA - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Sunday, 15 March 2026

KANUNI YA CHAMA CHA WALIMU TANZANIA (CWT) YAWAVURUGA WALIMU SINGIDA

Mwalimu Helena Nyahuru Mahamba wa Shule ya Msingi ya Unyakhae katika Manispaa ya Singida akiwadhoofu kutokana na maradhi ya kisukari yanayomsumbua kwa miaka 17.

.........................

Na Dotto Mwaibale, Singida

Kutokuwepo kwa kipengele ndani ya  Katiba ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) cha kutotoa msaada kwa wanachama wake wanapokuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuumwa imewavuruga walimu wa Mkoa wa Singida.

Hali hiyo imewafanya baadhi yao kujitoa kwenye chama hicho na kujiunga na vyama vingine vikiwepo  Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu Tanzania (CHAKAMWATA) na Chama cha Kulinda na Kutetea Walimu Tanzania (CHAKUHAWATA).

Akizungumza na mwandishi wa habari hii mwanzoni mwa wiki Katibu wa CWT  Manispaa ya Singida, Jones Madale alisema kwenye katiba ya chama hicho hakuna kipengele kinachoeleza kumsaidia mwalimu zaidi ya kutetea maslahi yao kwa mwajiri wao.

Kauli ya katibu huyo imekuja kufuatia mwanachama wa chama hicho Mwalimu Helena Nyahuru Mahamba wa Shule ya Msingi ya Unyakhae katika manispaa hiyo kuumwa ugonjwa wa kisukari kwa miaka 17 ambapo chama hicho kimempa Sh.100.000 tu ndani ya kipindi hicho.

 “ Mwalimu huyo ni mtumishi wa Serikali mwajiri ndiye anayewajibika sisi kama wanachama jukumu letu ni kumsukuma atoe huduma kwa mtumishi wake. Sisi huwa tunakwenda kumuangalia na kumpa pole pamoja na misaada midogo midogo kama kumpa matunda lakini ndani ya katiba yetu hakuna kipengele kinachoelezea  kumsaidia,’ alisema Madale.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya walimu wa Manispaa hiyo wamekiri wenzao kuhamia katika vyama hivyo kwa ajili ya kufuata maslahi mazuri ambapo walitoa maoni yao kama ifuatavyo.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Unyanga ambaye hakupenda jina lake liandikwe alidai kuwa licha ya kutokuwepo kwa kipengele hicho watumishi wengine wa idara zingine wanapoumwa wamekuwa wakipatiwa fedha za matibabu nje ya bima zao lakini siyo wa idara ya elimu.

Mwalimu huyo alisema kuwa walimu wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuwatengeneza watumishi wa ngazi tofauti wakiwepo  viongozi hivyo maslahi yao yanapaswa kuboreshwa.

“Kuna mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Somoko Leonard Bundara Februari 23, 2026 alivunjika mguu na kujeruhiwa kichwani baada ya kupata ajali ya pikipiki, na kupoteza fahamu.

Alipopelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma ambapo mwajiri wake alitoa gari na majeruhi aligharamia mwenyewe mafuta kwa kutoa Sh. 300,000,” alisema mwalimu huyo.

Hata hivyo mke wa majeruhi huyo Mwalimu Mwajuma Faustine amethibitisha mme wake kutoa kiasi hicho cha fedha na kudai kuwa tangu wafike hospitali hapo hakuna kiongozi yeyote  wa CWT wala mwajiri aliyefika kumjulia hali zaidi ya baadhi ya walimu ambao ni rafiki zake.

Mwalimu Helena Mahamba baada ya kushindwa kumudu gharama za matibabu alilazimika kubaki nyumbani akijiuguza huku hali yake ikiendelea kudhoofu kila siku.

 Taarifa zake zilipotolewa kwenye mitandao ya kijamii wiki liyopita akiomba msaada wa matibabu na kwa jitihada za Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi alipoisoma taarifa hiyo aliagiza mgojwa huyo apelekwe Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kuanza matibabu upya mara moja.

Pamoja na kuanza matibabu hali yake iliendelea kuwa mbaya na Machi 14, alipata rufaa ya kuhamishiwa Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma kwa ajili ya kupata matibabu kwa kusafirishwa na mwajiri wake.

Mwajiri wake alitoa fedha za kununua mafuta na Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida ilitoa gari la wagonjwa.

Ombi kubwa la walimu hao ni katika katiba yao kuwepo kipengele cha kuwasaidia walimu wanapo kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya magonjwa kutokana na michango yao wanayoichangia kila mwezi.

“Walimu Manispaa ya Singida tupo zaidi ya 800 ambapo  kwa mwezi kila mwalimu hukatwa siyo chini ya Sh. 33,000 na wale ambao wapo daraja la juu hukatwa zaidi ya kiwango hicho. Ni fedha nyingi zinazokusanywa ukipiga mahesabu hiyo ni kwa manispaa pekee, tunaomba ziwe zinatumika kutusaidia tunapokuwa na changamoto badala ya kusubiri kusaidiwa jeneza na kusafirishwa kwenda makwetu  tukifa,” alisema Mwalimu Robert Mtinga.

Kwa upande wake Mwalimu Helman Magoti alisema ni vema kuipitia katiba yao vizuri ili kuielewa kama hakuna kipengele cha kutambuliwa wanapokuwa na changamoto ya maradhi ili wapiganie kiwekwe kwa maslahi mapana ya walimu.

 “Walimu wengi ni wagonjwa lakini wanajipambania  wenyewe kupata matibabu, licha ya kuwa na bima dawa zingine zenye gharama kubwa hushindwa kuzipata na kulazimika kwenda kuzinunua. Katiba ya chama chetu ikiwekwa kipengele cha kututambua itatupunguzia mzigo wa kujigharamia matibabu ukizingatia mishahara yetu siyo mikubwa,” alisema Mwalimu Gregory Michael wa Shule ya Msingi Uhamaka.

Baada ya habari hiyo kuandikwa kwenye mitandao ya kijamii viongozi wakuu wa CWT Manispaa ya Singida Machi 8, 2026 wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, James Msai walikwenda kumjuali hali Mwalimu Mahamba.

Viongozi hao mara baada ya kuwasili kwa mgonjwa  huyo ajenda yao kubwa ilikuwa ni kuona namna ya Mwalimu Mahamba kurudishwa nyumbani kwao baada ya kushauriana na ndugu zake huku wakiahidi kufuatilia kwa mwajiri wake barua aliyoandika kuomba kusaidiwa matibabu.

Hatua hiyo ilijiri baada ya kuona hana mtu wa uhakika wa kumuuguza katika eneo hilo analoishi, ambapo walitoa pole yao kwa kumpa sabuni, mipira ya kuvaa mikononi (Groves) na Pempasi.

Viongozi wengine waliokuwepo katika msafara wa kwenda kumjulia hali mwalimu mwenzao huyo ni pamoja na Katibu wa chama hicho Manispaa ya Singida, Jones Madale na Wawakilishi, Yasinta Makaya na Innosanta Shayo.

Baadhi ya walimu wamepongeza hatua zilizochukuliwa na mwajiri wake Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Singida na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Singida kwa kufanikisha kumpeleka mgonjwa huyo Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ajili ya kuendelea kupata matibabu zaidi ambapo amelazwa wodi namba mbili ghorofa ya pili.

Pamoja na kuanza kupata matibabu Mwalimu Mahamba anahitaji msaada wa mahitaji ya kibinadamu kama chakula, maji, sabuni na mengine mengi ambayo yanahitaji fedha kwa atakaye guswa kumsaidia anaweza kumtumia kiasi chochote kupitia namba 0787820053 au 0759521565 na Mungu atakubariki kwa utoaji wako kwani kutoa siyo utajiri bali ni moyo wa mtu.

Uongozi wa Singidani Blog unatoa shukrani na pongezi nyingi kwa Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi  kwa kuchukua hatua za haraka na kufanikisha Mwalimu Helena Nyahuru Mahamba kuanza kupata matibabu baada ya kusoma habari hiyo.

Mwalimu Helena Nyahuru Mahamba akifanya mazoezi ya kutembea nyumbani kwake Unyakhae Manispaa ya Singida.

Vigogo kutoka Chama cha Walimu Manispaa ya Singida walipo kwenda kumjulia hali mwalimu mwenzao Helena Mahamba Machi 8, 2026. baada ya habari yake kuandikwa kwenye mitandao ya kijamii. Kutoka kulia ni Yasinta Makaya, Innosanta Shayo na Mwalimu aliyetambulika kwa jina la Shani Rajabu wa Shule ya Msingi, Unyakhae.
Mwalimu Helena Nyahuru Mahamba alivyokuwa kabla ya kuanza kuumwa.

Taarifa hii imeandikwa na Dotto Mwaibale namba 0754362990.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad