DC HANANG ATATUA MGOGORO WA ARDHI KWA MASAA MANNE WANAWAKE WAKESHA SIKU TISA

Subscribe Us

DC HANANG ATATUA MGOGORO WA ARDHI KWA MASAA MANNE WANAWAKE WAKESHA SIKU TISA

Mkuu wa Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, Janeth Mayanja, akizungumza juzi na Wananchi wa              Kijiji cha Mogitu kilichopo Kata ya Mogitu  wakati akitatua mgogoro wa ardhi ambao uliwafanya  wanawake wa kijiji hicho wa kabila la Barbaiq kukesha siku tisa wakishinikiza kurudishiwa eneo lao la kuabudia lililouzwa.

Wananchi wa Kijiji cha Mogitu wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya , Janeth Mayanja (hayupo pichani) wakati akitatua mgogoro huo.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja, akiwa amekaa na Wananchi wa Kijiji cha Mogitu baada ya kutatua mgogoro wa ardhi.
Wananchi na Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja wakiwa kwenye eneo lililokuwa na mgogoro.


Na Mwandishi Wetu, Hanang


MKUU wa Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, Janeth Mayanja  ametatua mgogoro wa ardhi kwa muda wa masaa manne na kuwashangaza wananchi na wanawake wa kabila la Barbaiq waliokesha siku tisa wakishinikiza kurudishiwa eneo lao la kuabudia katika Kijiji cha Mogitu kilichopo Kata ya Mogitu wilayani humo.

Wakiongea mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye alifika juzi katika kijiji hicho kwa ajili ya kutatua mgogoro huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanawake hao walisema eneo hilo wamekuwa wakilitumia kwa kuabudia tangu enzi na enzi.

Walisema walilazimika kukesha wakishinikiza kurejeshewa eneo hilo baada ya mwanakijiji mwenzao waliyemtaja kwa jina la Gembe Nono kudaiwa kuwauzia wananchi wengine wawili wa kijiji hicho.

Afisa Mtendaji wa kijiji hicho  Linda Darema alisema wanawake hao walilala nje kwa siku tisa kuonesha hasira zao kufuatia eneo lao hilo la kuabudia kumegwa na kuuziwa  watu kinyume na imani za kabila hilo ambalo lilitengwa kwa ajili ya kuabudia na si mashamba wala makazi ya watu.

Akitatua mgogoro huo kwa njia ya mkutano wa hadhara uliowahusisha muuzaji wa eneo hilo na wanunuzi pamoja na wananchi  mkuu wa wilaya hiyo Mayanja  alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haina dini ila watu wake wanadini na kuwa inaheshimu mila na desturi.

Mayanja alimtaka muuzaji wa eneo hilo Gembe Nono kuelezea uhalali wa kuuza eneo hilo ambapo alikiri kuliuza kimakosa ambapo aliwarejeshea fedha aliowauzia.

"Wanunuzi wa eneo hilo walieleza kwamba walinunua bila ya kujua kama lilikuwa likitumika kwa ajili ya kuabudia ambapo tayari wamebomoa nyumba walizokuwa wamejenga baada ya kurejeshewa fedha zao,". alisema Mayanja.

Aidha mkuu wilaya hiyo Janeth Mayanja amelikabidhi eneo hilo kwa viongozi wa kijiji  na kuagiza liendelee kutumika kama jamii ilivyokua inalitumia awali na kuhimiza jamii kuendelea kulinda maeneo hayo ili kudumisha mila na desturi.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho aliyetambulika kwa jina moja la Safari  amemshukuru mkuu wa wilaya kwa kufika kwa wakati na kutatua mgogoro huo ndani ya masaa manne jambo ambalo hawakulitegemea hasa baada ya wanawake kukesha siku tisa wakishinikiza waliouziwa eneo hilo waondoke.

"Tunachukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana mkuu wetu wa wilaya kwa kutatua mgogoro huu kwa wakati na maagizo yake yote alioyatoa tutayatekeleza,". alisema Safari.

Post a Comment

0 Comments