DC ITUNDA AHAMASISHA WANANCHI KUJIUNGA NA MPANGO WA HIARI -NSSF KWA MANUFAA YAO

Subscribe Us

DC ITUNDA AHAMASISHA WANANCHI KUJIUNGA NA MPANGO WA HIARI -NSSF KWA MANUFAA YAO

Na Mwandishi Wetu – Mbeya

16,Oktoba, 2025

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, ameushukuru uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kumshauri kuendelea kuchangia kupitia Mpango wa Hiari badala ya kutoa mafao yake, hatua ambayo amesema imekuwa na manufaa makubwa kwake binafsi.

Akizungumza katika hafla ya kugawa majiko ya gesi kwa baadhi ya mama lishe, baba lishe, wastaafu na wanachama wa NSSF mkoani Mbeya, Itunda alieleza, alihamasika kutoa fedha zake za NSSF alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Songwe, lakini ushauri alioupata kutoka kwa viongozi wa NSSF ulimsaidia kufanya uamuzi sahihi.

“Nilikuwa mwanachama wa NSSF, baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Songwe, nilihamasika kutoa mafao yangu kwa ajili ya kuwekeza kwenye biashara. 

Hata hivyo, viongozi wa NSSF walinishauri nisitoe fedha hizo, bali niendelee kuchangia kupitia Mpango wa Hiari, nilifuata ushauri huo, na sasa ninaendelea kuwa mchangiaji mzuri wa NSSF,” alisema Itunda.

Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mageuzi makubwa katika sekta ya hifadhi ya jamii, ambayo yamewawezesha wananchi waliojiajiri kujiunga na kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na NSSF.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, aliwahimiza wananchi waliojiajiri kujiunga na kuchangia katika Mfuko huo ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali yakiwemo ya matibabu, uzee, uzazi na mengineyo muhimu kwa ustawi wa jamii.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, aliwahimiza wananchi kujiwekea akiba kupitia NSSF kwa ajili ya maisha ya sasa na ya baadaye, akisisitiza kuwa hifadhi ya jamii ni nguzo muhimu ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


Post a Comment

0 Comments