Na Dotto Mwaibale,
Iramba
MKUU wa Wilaya ya
Iramba, Suleiman Mwenda amesema umilikaji wa ardhi kiholela ndio chanzo kikubwa
cha migogro ya ardhi nchini.
Mwenda ambaye
alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhi hati za ardhi 100 kwa wananchi wa
Lulumba Kiomboi wilayani humo ambao wamekamilisha zoezi zima la kuzilipia na
kupata mafunzo ya umuhimu wa kupima ardhi zao yaliyotolewa na Ofisi ya Ardhi
Mkoa wa Singida alisema jambo hilo limekuwa ni changamoto kubwa wilayani humo.
Alisema ardhi ni
rasilimali muhimu sana kwani kila kitu kinachofanyika hapa duniani kinafanyika
juu ya ardhi na kuwa masuala
yanayohusu ardhi ni nyeti sana.
Mwenda alisema kuwa
vita vingi vilivyopo duniani chanzo chake ni ardhi ikiwepo ile inayoendelea
kule ukreni na kutingisha uchumi wa dunia.
“Mimi katika kesi
ninazokumbuna nazo ofisini kwangu nyingi ni za migogoro ya ardhi ambazo ni kati
ya asilimia 80 hadi 90 na sababu kubwa inayosababisha hali hiyo ni watu wengi
kumiliki ardhi kienyeji bila ya kufuata utaratibu unaotambulika na Serikali”
alisema Mwenda.
Mwenda aliomba idara
ya ardhi wilayani humo kuhakikisha inaharakisha kupima ardhi ya wananchi wote
jambo litakalosaidia kuleta maeendeleo na kupunguza migogoro hiyo
ambayo imekithiri.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida,
Shamim Hoza akizungumza katika hafla hiyo aliomba ajenda ya ardhi iwe namba
moja kwenye vikao vya baraza la madiwani la halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwa
tukizingatia kuwa ardhi ni sekta wezeshi kwa kuwa kila kitu kinafanyika juu
yake.
“Ardhi hii ni lazima tuithamini, tuilinde na kuitunza kwa nguvu zetu zote na ili tufanikiwe tunapaswa tuwe na ajenda hiyo ya kudumu” alisema Hoza.
Hoza alitaja faida kadhaa za kuwa na hati ya
kumiliki ardhi ni kuwa na uhakika wa
usalama wa ardhi ya muhusika anayomiliki, nyumba au maendeleo yoyote aliyoyafanya
katika ardhi hiyo, hati hiyo kutumika katika kuomba mkopo benki ikitumika kama
rehani na kutumika kama dhamana mahakamani na polisi na hati hiyo inaweza kusaidia
kuhamisha umiliki wa ardhi kiuhalali na kwa uhakika.
Hoza alisema mchakato
huo wa kutoa hati kwa wananchi mkoani hapa unaendelea katika wilaya tatu za
Iramba, Manyoni na Ikungi ambapo maofisa wa ardhi Mkoa wa Singida
wakishirikiana na wenzao katika wilaya hizo wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi
kuhusu umuhimu wa kuwa na hati za umiliki wa ardhi huku muitikio ukiwa mkubwa.
Alisema ofisi yake imejipanga kuhakikisha zoezi hilo litaendelea vizuri katika wilaya zote mkoani hapa na kuwa la mafanikio.








No comments:
Post a Comment