Na Mwandishi Wetu, OWMS, Dodoma
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
(OWMS) imeendelea kuiwasilisha Serikali katika kusimamia mashauri ya madai na
usuluhishi ambapo imefanikiwa kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi 6,043
kwa kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwa OWMS mwaka 2018.
Hayo yameelezwa na Naibu
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende wakati akizindua Baraza la
kwanza la wafanyakazi wa OWMS lililofanyika jijini Dodoma na kusema kuwa OWMS
imeendesha mashauri hayo kwa niaba ya Serikali kwa umakini mkubwa na umahiri ili
kuendelea kutekeleza majukumu ya OWMS ili kufikia na hata kuzidi matarajio ya
Serikali.
Ameongeza kuwa OWMS
imeendelea kuiwakilisha Serikali Mahakamani na katika mabaraza ya usuluhishi
ambapo tangu kuanzishwa kwake imeendesha mashauri ya madai yapatayo 5,885 na
mashauri ya usuluhishi 158 na kufanya jumla ya mashauri kuwa 6,043.
“Mashauri ya Madai
yaliyomalizika katika kipindi cha miaka minne ni mashauri 582 na ya Usuluhishi
ni mashauri 60 ambapo kati ya hayo, Serikali imeshinda mashauri 530 ya madai na
Mashauri ya Usuluhishi 31”, amesema Dkt. Luhende
Amesema kuwa kama alivyoagiza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, OWMS imeendelea
kuhakikisha inaiwakilisha vyema Serikali na kuvutia wawekezaji nchini kwa kumaliza
migogoro mbalimbali dhidi ya wawekezaji na wafanyabiashara kwa njia ya majadiliano
jambo ambalo limesaidia kupunguza idadi ya migogoro dhidi ya Serikali iliyofunguliwa
kwenye Mahakama na mabaraza nje na ndani ya nchi; kuokoa fedha za Serikali
ambazo zingetumika katika kuendesha migogoro tajwa; kudumisha uhusiano kati ya
Serikali na wawekezaji; kujenga imani kwa wawekezaji kuhusu hali ya utoaji haki
nchini; na kukuza diplomasia ya uchumi.
“Mfano wa shauri la usuluhishi
lililomalizika kwa njia ya majadiliano ni baina ya G.S Engineering
&Construction Corporation ya Korea ya Kusini dhidi ya TANROADS likihusiana na
ujenzi wa daraja la Tanzanite na mgogoro ulikuwa umepelekwa ICC na shauri
lilimalizika na sasa daraja linaendelea kutoa huduma kwa wananchi,” amesema
Dkt. Luhende.
Pia, amewapongeza watumishi
wa OWMS ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa ufanisi ili kuhakikisha maslahi ya
Taifa yanalindwa kwa ulinzi mkuu pamoja na kukuza diplomasia ya uchumi wa nchi.
Mmoja wa Wajumbe wa Baraza
hilo, Wakili wa Serikali, Rashid Mohamed amesema siri ya mafanikio yaliyopatikana
ni uongozi thabiti wenye kutoa maelekezo sahihi ya namna ya kutekeleza majukumu
ya Ofisi ambapo Mawakili wenyewe wamekuwa na jitihada za kujifunza kile
wanachokifanyia kazi ili kuweza kuleta mafanikio kwenye kazi wanazozifanya.
Naye Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Bi Jenipher Kaaya ambaye pia ni mjumbe wa Baraza hilo amesema kuwa OWMS
inafanikiwa kumaliza mashauri nje ya mahakama au mabaraza ya usuluhishi kwa
kufanya majadiliano na wale wanaoidai Serikali kwa kuweka masuala ya kisheria
pembeni na kujadili hoja kama watu wa kawaida na hatimaye kufika mwafaka na
kuweza kushinda mashauri hayo.
“Katika majadiliano hayo
kuna sehemu kadhaa tunatumia sheria kwa kutegemeana na aina ya kesi na hivyo
kwa kutumia usuluhishi tumefanikiwa kumaliza migogoro mingi kwa wakati na kwa muda
mfupi tofauti na mahakamani ambapo historia inaonyesha kuwa migogoro inakaa
mwaka mmoja au miaka miwili tu na kumalizika,” amefafanua Kaaya.
Mkurugenzi wa Utawala na
Utumishi wa OWMS, James Kibamba ametoa rai kwa wajumbe hao kuhakikisha kuwa
masuala wanawakilisha vema watumishi wengine na kuwapatia mrejesho kwa kuwa sio
rahisi kwa watumishi wote kuwa wajumbe wa Baraza.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini,
Ofisi ya Wakili
Mkuu wa Serikali
No comments:
Post a Comment