RC SINGIDA KUWASWEKA NDANI VIGOGO WANAOSIMAMIA MASHAMBA YA KOROSHO MANYONI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, October 3, 2022

RC SINGIDA KUWASWEKA NDANI VIGOGO WANAOSIMAMIA MASHAMBA YA KOROSHO MANYONI

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza na wadau wa zao la kilimo cha korosho , wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama na kamati inayoratibu mashamba ya Korosho Wilaya ya Manyoni katika kikao kilifofanyika jana. Kulia ni Afisa Tawala Wilaya ya Manyoni, Leila Sawe na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Melkzedeki Humbe.
Afisa Tawala Wilaya ya Manyoni, Leila Sawe akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Melkzedeki Humbe akizungumza kwenye kikao hicho.
Wajumbe wa kamati ya kuratibu kilimo cha korosho Wilaya ya Manyoni wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Mkulima Sunga Kusweka kutoka Kampuni ya Sundy Merchants Co.Ltd akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Wadau wa kilimo cha zao la korosho wakiwa kwenye kikao hicho.
Mkulima Shija Kazozo akizungumza.
Mkulima Domitilla Bashemera akichangia jambo kwenye kikao hicho. 

Na Dotto Mwaibale, Manyoni 

MKUU wa Mkoa Singida, Peter Serukamba  ameitaka kamati inayoshughulikia kilimo cha zao la korosho wilayani Manyoni mkoani hapa kuhakikisha ifikapo Novemba 30, 2022 iwe imesafisha mashamba na kuwapa wakulima ambao walikwisha ya yalipia lakini bado hadi leo hawajakabidhiwa.

Serukamba alitoa agizo hilo jana  wakati akizungumza na wadau wa kilimo cha zao hilo , wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama na kamati inayoratibu mashamba hayo kuwa hadi ifikapo tarehe hiyo iwapo watashindwa kufanya hivyo  atawasweka ndani akiwepo na Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.

“Hadi ifikapo Novemba 30 kama hamtakuwa mmetekeleza maagizo haya nitatumia sheria ya kuwaweka ndani na siku hiyo nikija Takukuru, Polisi mjiandae” alisema Serukamba.

Serukamba ameitisha  kikao hicho ili kumaliza sintofahamu ya jambo hilo linalohusisha mashamba waliopewa wakulima hao yaliyopo Itigi-Njilii, Kaminyange, Masigati na Mkwese ambapo kuna makundi manne ya wakulima ambao wapo kwenye mgogoro huo ulianza kutatuliwa na Serikali mkoani hapa kwa kushirikiana na bodi ya korosho.

Makundi hayo ni la wakulima ambao walilipia mashamba hayo na wameanza kulima, wapo wenye mashamba lakini ni mapori, wapo wenye mashamba lakini hawajakabidhiwa rasmi na wale ambao walilipia lakini wapowapo tu na hawajui hatima yao.

Katika kikao hicho baadhi ya wakulima walipewa  nafasi ya kujieleza na kutoa masikitiko yao ya kupoteza muda mwingi wakisumbuliwa kwa zaidi ya miaka mitatu bila ya kupewa mashamba hayo licha ya kutoa fedha zao Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Melkzedeki Humbe. akizungumza kwenye kikao hicho alisema kazi kubwa inayofanyika hivi sasa ni kuyahainisha mashamba yote ambayo yalipimwa lakini hayakusafishwa na ili kuanza kumaliza mchakato huo wanatafuta fedha Sh.Milioni 450 kukamilisha kazi hiyokwa ekari zaidi ya 3120.

Mkuu wa Mkoa mstaafu wa mkoa huo Dk. Binilith Mahenge naye aliwahi kuitisha kikao cha namna hiyo ambacho kiwahusisha Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) na kilitoa baadhi ya maazimio kuwa ndani ya mwezi mmoja mvutano huo uwe umemalizika na kabla ya Oktoba 1, 2022 wakulima wote waliolipia fedha zao na kukamilisha taratibu zote wakabidhiwa mashamba yao na kuanza kulima.

Azimio lingine lilikuwa ni kutumika kwa akaunti moja ya mradi huo na kuundwa kwa kamati mpya itakayosimamia baada ya zile mbili za awali kuvunjwa na kuomba wahusika wa kamati hizo zilizovunjwa kutoa ushirikiano kwa kamati mpya na watakaoonekana wanashindwa kutoa ushirikiano watachukuliwa hatua.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad