Mafundi umeme wakiwajibika sehemu ya mafunzo.
Na Mwandishi Wetu, Iringa
ZAIDI ya mafundi 1800 wa aina mbalimbali wanatarajia kukutana pamoja katika
kongamano kubwa litakalo fanyika Mjini Iringa lengo kubwa likiwa kupanua wigo
wa ajira na kuongeza fursa kwenye kundi hilo muhimu kwenye jamii.
Meneja wa FundiSmart, Fabian Mwiga amesema kongamano hilo litafanyika Machi
17, 2023 katika ukumbi wa Masiti, Manispaa ya Iringa.
Kiuhalisia, mafundi ni kati ya kundi lililoachwa pembeni licha ya kuwa vitu
vingi zinavyoizunguka dunia vinatokana na uwepo wa fundi.
“Tunawakutanisha mafundi mbalimbali
bila kujali aina ya ufundi wao, mpaka sasa tunao mafundi 1800
waliojiandikisha,” amesema Mwiga.
Amesema kwenye kongamano hilo mafundi watapata fursa ya kujua umuhimu na
thamani ya kazi yao, elimu ya afya na bima, fedha, sheria, akiba na huduma bora
kwa wateja.
“Sekta ya ufundi ni nyeti na mafundi wanazo ndoto zao, sasa wanaweza
kufikia ndoto zao ikiwa tutawaonyesha mlango wa kupita, FundiSmart imekuja kwa
ajili hiyo,” amesema Mwiga.
Amesema kwa sababu kundi hilo limekuwa likilalamikiwa zaidi na wateja hasa
kwenye suala la uaminifu, elimu kuhusu sheria na huduma kwa wateja itawasaidia
zaidi.
Kwa upande wao baadhi ya mafunzi wamesema hakuna siku waliketi pamoja na
kutambuliwa kama sekta nyeti.
‘Hata tukifanya kazi mtu anakulipa atakavyo bila kujali kazi kubwa
unayofanya, naamini hii ni fursa kwetu kutambua kazi yetu na kuipatia
kipaumbele,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hilo.
0 Comments