Na Calvin Gwabara, Njombe
KIONGOZI wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi Bw.
Dixon Waruinge ambaye ndiye Msimamizi wa Utekelezaji wa Mradi wa Mfano
wa Tathimini ya Maji kwa Mazingira (EFLOWS) amesema mradi huo umetekelezwa
vizuri zaidi ya vile walivyotarajia na
matokeo yake yameshaanza kunufaisha baadhi ya nchi za Afrika.
Kiongozi huyo ameyasema hayo mkoani Njombe kwenye wilaya ya Wanging`ombe
mara baada ya yeye na timu ya maafisa wengine wa sekretarieti hiyo ya Azimio la
Nairobi kumaliza kazi ya kukagua na kuona kazi mbalimbali zilizofanywa na
zinazoendelea kufanywa naMradi huo unaotekelezwa na Watafiti wa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo kwa kushirikiana na Baraza la Hifadhi ya Mazingira NEMC
kwenye Wilaya za Mbarali na Wangingombe mkoani Njombe na Mbeya.
“La muhimu au kubwa zaidi ni kusema
kuwa Tanzania mmefanikisha kuzidi kiasi ambacho tulitarajia, utafiti umefanyika
vizuri sana na tayari kuna nchi zimenufaika na masomo (leasons) kutoka Tanzania
maana Prof. Japhet Kashaigili amesafiri kwenda Madagasca kuwapa masomo
yaliyopatikana Tanzania, na sisi hapa tumezishuhudia na baada ya hapa nchi
nyingine nyingi zitajifunza kutokana na mambo waliyofanya Tanzania”, alifafanua
Bw. Waruinge.
Kiongozi huyo wa Azimio la Nairobi amesema umuhimu wa azimio hilo ambalo
linaundwa na nchi 10 za Afrika Mashariki na Visiwa vya Madagascar, Seychelles
na Comoros, Mauritius na Reunion ambayo ipo Ufaransa wakutane kama nchi
wayaangazie masuala yote ya mazingira ya maji ya Bahari na wanapoangalia hayo
lazima wazingatie na kutazama maji ya mito kwa kuwa maji yake pia yanaingia
baharini.
Bw. Wariunge amesema kutokana na hilo wakaona ni vyema kuangalia ni kwa
namna gani mito inahifadhiwa kwa ajili ya Mikoko na Samaki na baada ya kufikia
hatua hiyo wakajiuliza suala la mito inayopita nchi moja na nyingine na mito ya
ndani ya nchi moja kujua changamoto zake na namna inavyotunzwa.
“Kwa hiyo tukakubaliana tuwe na mradi ambao utaangazia masuala hayo kwa
kuwa matatizo yanayogusa mito ya nchi moja yanalingana na ya nchi nyingine
ndipo mradi huu ukaanzishwa na tukaona hatuwezi kuanzisha mradi kama huu nchi
zote 10 ndipo Tanzania ikachaguliwa kutekeleza mradi huu wa mfano kupitia mto
Rufiji na Mbarali kama chanzo cha utafiti na maarifa ya yale yatapatikana kama
mafunzo Tanzania yasaidie kusambazwa kwenye serikali za nchi zingine zilizobaki
Afrika”, alieleza Kiongozi huyo wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Makamu wa Rais upande wa
Bionuai Bw. Thomas Bwana amesema kwenye eneo la mazingira kuna eneo kubwa
wanaliangalia ambalo ni Vyanzo vya maji eneo ambalo maji yake yanakwenda kwenye
mito na mwisho wake ni baharini hivyo lazima maeneo hayo yapewe kipaumbele.
“Eneo hili hapa tuliposimama ni chanzo kikubwa tu cha maji ambacho kilikuwa
kimeharibiwa na shughuli mbalimbali za binadamu lakini kupitia kazi kubwa ya
kutoa elimu kupitia mradi huu na wataalamu wengine unaweza kuona sasa
limepandwa miti rafiki wa maji na linatunzwa hata zile shughuli za kibinadamu
hazifanyiki tena mahali hapa na maji yanaendelea kutiririka na hii inatufundisha
kuwa kumbe inawezekana wananchi kutunza vyanzo hivi vya maji kwa faida yao na
taifa kwa ujumla”, alisema Bw. Thomas.
Ameongeza kuwa Mradi huu wa Utafiti wa EFLOWS unasaidia jamii na Tanzania
kujihakikishia upatikanaji wa maji na utiririkaji salama kwa ajili ya matumizi
ya kilimo kupitia umwagiliaji, Uzalishaji wa umeme kwenye maeneo mengine, Maji
kwa ajili ya matumizi ya nyumbani katika maeneo yaliyo eneo la chini la mto na
hilo ndio lengo kubwa kwa Ofisi ya Makamu wa Rais upande Mazingira.
Mkurugenzi huyo Msaidizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais upande wa Bionuai
amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na watafiti wa SUA na NEMC katika kutekeleza
mradi huo mzuri wa mfano na kuahidi kuendelea kushirikiana nao ili matokeo
mazuri ya mradi huo yaweze kutumiwa pia kwenye maeneo mengine ya Tanzania yenye
vyanzo vya maji na mito.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kutoka SUA Prof. Japhet
Kashaigili amesema chimbuko la mradi huo linaungana na utekelezaji wa Sheria ya
Maji na Mazingira ambayo katika kugawana maji kuna vipaumbele vitatu ambavyo ni
maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu, maji kwa ajili ya Mazingira na maji kwa
ajili ya shughuli zingine.
“Ukiangalia mgawanyo huo wa maji ni rahisi kujua maji kwa ajili ya binadamu
umetumia kiasi gani kwa siku lakini maji kwa ajili ya matumizi mengine kama
vile kilimo pia ni rahisi kujua lakini maji kwaajili ya mzingira kutunza
bionuai kwaajili ya sasa na baadae ni kama ilikuwa haijulikani au Sayansi yake
haikuwepo lakini sasa utaalamu huu tunao na tumefanya kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali na duniani sasa nchi mbalimbali zinaweza kufanya tathmini hii ya
maji kwa mazingira”, alifafanua Prof. Kashaigili.
Amesema kupitia utaalamu huo sasa wameweza kufanya tathimini hiyo kwenye
mto Mbarali kuanzia juu kwenye vyanzo vya mto kufika katikati ambako jamii
inatumia maji kwa kazi mbalimbali za kilimo, kuingia kwenye ardhi oevu, kuingia
mto Rufiji hadi kwenye hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kwenda kwenye mabwawa ya
uzalishaji umeme ya Kidatu na Mwl.Julius Nyerere na mwisho kuingia baharini.
Mtafiti huyo Mkuu amesema Mradi huo ni mfano kwa kuwa unamaanisha athari zitokanazo na shughuli za kibinadamu kwenye mtiririko wa maji kwenye mito na namna ya kupunguza athari hizo na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambao wana mahusiano ya moja kwa moja na maji hayo ya mto ikiwemo Jumuiya za watumia maji, Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji, TANAPA, TANESCO na wengine ikiwemo wakulima.
0 Comments