PASS Trust yawaasa wadau wa Kilimo Biashara Singida kufanya Kilimo rafiki kwa Mazingira Kunufaika na dhamana ya hadi 80% ya mikopo

Subscribe Us

PASS Trust yawaasa wadau wa Kilimo Biashara Singida kufanya Kilimo rafiki kwa Mazingira Kunufaika na dhamana ya hadi 80% ya mikopo

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akiwa na Meneja Maendeleo ya Biashara wa PASS Trust, Herman Bashiri wakati wa mkutano wa wadau wa kilimo Mkoa wa Singida kwenye uzinduzi wa kampeni ya Kijanisha Maisha na Programu ya ukuaji wa kijani shirikishi Kanda ya Kati na Mashariki. 

Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA 

TAASISI ya Kusaidia Sekta Binafsi ya Kilimo (PASS Trust) imezindua kampeni ya Kijanisha Maisha na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo mkoani Singida kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji unaozingatia ukuaji wa kijani shirikishi ili kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Uzinduzi huo umefanyika Leo Machi 32, 2023 katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Social Training Center mjini Singida.

Katika mkutano  huo mambo kadhaa yalijadiliwa na washiriki likiwamo suala la njia za kuharakisha na kuimarisha maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa kutilia mkazo Ajenda ya Ukuaji wa Kijani  Shirikishi kwa kilimo endelevu kitakachotosheleza mahitaji ya kujikimu kibiashara na kuhakikisha usalama wa chakula cha uhakika na kilimo stahimilivu.

Kwa mujibu wa PASS Trust, usalama endelevu wa chakula utafikiwa kupitia mapinduzi ya kilimo yenye uthabiti na uendelevu kwa kuzingatia kanuni za Ukuaji wa Kijani Shirikishi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo katika mkutano huo, Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa PASS Trust, Herman Bashiri, alisema, PASS Trust ina mchango mkubwa katika kuchochea na kuwezesha ukuaji wa kilimo nchini Tanzania.

Alisema taasisi hiyo inatoa  kipaumbele kwa vijana na wanawake ambao wanapewa dhamana ya mikopo na huduma za maendeleo ya biashara ili waweze kufikia malengo yao.

Bashiri alisema kuwa wakulima wananufaika na PASS Trust kwa kuwekewa dhamana ya mikopo ya kilimo, mifugo na uvuvi kupitia benki mbalimba zilizopo hapa nchini.

  “Tunatoa dhamana ya hadi asilimia 80 ya mikopo kwa wakulima, wavuvi, wafugaji na wenye viwanda wanaozalisha kwa kufuata kanuni za uhifadhi  wa Mazingira na kupitia kampuni yetu tanzu ya PASS Leasing piaa tunawezesha upatikanaji wa zana za kilimo,” alisema.

Akifafanua kuhusu ushirikishwaji wa wadau wengine wa kilimo katika mkutano huo, Bashiri alisema  PASS Trust imekuwa na ushirikiano na mashirika mengine yanayohudumia sekta ya kilimo na ndiyo maana imewaalika wadau wengine wa sekta hiyo kwa ajili ya kujadili na kubainisha njia mbalimbali zinazoweza kusaidia sekta ya kilimo kupitia ajenda ya Ukuaji wa Kijani Shirikishi ambayo inalenga kuhimiza ukuaji wa kilimo kwa kujali uhifadhi wa mazingira asilia.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, ambaye alikuwa mgeni rasmi aliipongeza PASS Trust kwa kuja na Mpango wa Kukuza Uchumi kupitia ajenda ya Ukuaji wa Kijani Shirikishi na kwamba hiyo ni njia bora ya kuchochea kilimo endelevu.

“Naipongeza PASS Trust kwa ubunifu na kuanzisha ajenda ya Ukuaji wa Kijani Shirikishi ambayo kwa hakika inachochea maendeleo endelevu ya kiuchumi ambayo yanaenda sambamba na utunzaji wa mazingira na kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo”, alisema Serukamba.

Awali katika ukaribisho wa mkutano , Mkurugenzi wa Maendeleo ya biashsra wa PASS Trust, Adam Kamanda,alisema lengo kuu la PASS Trust ni kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha  kwa wakulima wa kilimo biashara nchini Tanzania ambao wamegawanyika katika makundi matatu, ambayo ni watu binafsi, vikundi na makampuni yanayojihusisha na kilimo kwa kutoa dhamana ya hadi asilimia 80 kwa kilimo kinachozingatia ukuaji wa kijani shirikishi .

“PASS Trust ilianzishwa mwaka 2000 kama asasi yenye lengo la kuwezesha uwekezaji na ukuaji katika kilimobiashara na sekta zinazohusiana. Hadi sasa PASS inatimiza miaka 23 tangu ilipoanzishwa huku ikiwafikia waufaika milioni 3.4 nchi nzima na kuzalisha zaidi ya ajira milioni 2.7 huku biashara zipatazo 66077 zikinufaika,” alisema Kamanda.

PASS inatoa huduma katika mikoa yote nchini Tanzania kupitia ofisi za kanda katika mikoa sita ambayo ni Kanda ya nyanda za juu kusini (Mbeya) kanda ya kati na mashariki(Morogoro) kanda ya magharibi(Tabora),Kanda ya Kusini (Ruvuma),Kanda ya Kaskazini(Arusha),Kanda ya ziwa (Mwanza) na Ofisi kuu Dar es Salam.

PASS pia inapatikana kwa urahisi katika mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, YouTube, Twitter na kupitia Tovuti yenye jina la PASS Trust. Kwa maelezo zaidi inapatikana pia kwa namba ya huduma kwa wateja kwa namba ya bure 0800750037.

Meneja Maendeleo ya Biashara wa PASS Trust, Herman Bashiri akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizindua mpango huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa PASS.Trust.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akiwa katika picha ya pamoja viongozi wa PASS Trust.

 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akiwa na baadhi ya washiriki wa mkutano huo.

Post a Comment

0 Comments