Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa na Mkurugenzi wa Msowoya Foundation, Dkt Tumaini Msowoya,akiwafundisha wanafunzi namna ya matumizi ya kompyuta.
Na Mwandishi wetu, Iringa
MJUMBE wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa na Mkurugenzi wa Msowoya Foundation, Dkt Tumaini Msowoya amesema ipo haja kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari kujua kompyuta na kuzitumia kwa ajili ya kujifunzia.
Akizungumza Jana baada ya kupita katika baadhi ya Shule ambazo wanafunzi wake wanatumia Kompyuta, Dkt Msowoya alisema huo Ni mfano wa kuigwa na shule nyingine.
Alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Justine Nyamoga kwa kugawa kompyuta na kuhamasisha matumizi yake kwenye shule.
"Kumbe inawezekana, Wilaya ya Kilolo shule nyingi watoto wanajifunza kompyuta na hii ndio dunia iliko sio mtoto anamaliza kidato cha sita anaanza kuhangaika kutuma maombi," alisema Dkt Msowoya na kuongeza;
"Jamii, viongozi na Wadau mbalimbali tunaweza kusaidia katika kuichangia sekta ya elimu. Tusingoje Serikali peke yake,"
Alimpongeza Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha njia na kuhakikisha kila mtoto anakaa darasani bila kujali Mazingira yake.
"Zamani madarasa yalikuwa hayatoshi lakini kila shule ina madarasa mengi. Rais wetu anachapa kazi kwelikweli," alisema Dkt Msowoya.
Awali baadhi ya wanafunzi wanaosoma kompyuta walisema wanalifurahia somo hilo kwa sababu linawaka uhakika wa kujua masomo mengine.
Walisema kupitia kompyuta wanaweza kujisomea wenyewe na kutafuta notisi zaidi kwa ajili ya masomo.
0 Comments