Mfamasia Mkuu wa Serikali Daud Msasi akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wakati akifungua semina ya siku mbili ya Wahariri wa vyombo vya habari Aprili 5, 2023, iliyoandaliwa na MSD ambayo inafanyika mkoani Dodoma.
Na Dotto Mwaibale,
Dodoma
BOHARI ya Dawa (MSD)
inatarajia kujenga maghala matano kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza,
Kagera, Dodoma na Mtwara ili kuboresha huduma za utendaji wa kazi zao.
Hayo yamebainishwa
na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai wakati akizungumza na wahariri wa
vyombo vya habari katika semina iliyoandaliwa na MSD ambayo inafanyika mkoani Dodoma.
“Maghala haya
yatasaidia kuboresha huduma zetu za kusambaza dawa na vifaa tiba kwa wananchi
hasa katika mikoa ambayo ina watu wengi kama Mwanza, Dar es Salam na Kagera”
alisema Tukai.
Tukai alitaja mikoa
ambayo yatajengwa maghala hao kuwa ni Kagera, Mwanza, Dodoma, Dar es Salaam na
Mtwara.
Akizungumzia
maboresho ya utendaji kazi wa MSD alisema wameanzisha mfumo wa kufanya kazi kwa
njia ya mtandao na kuachana na ule wa kutumia makaratasi jambo ambalo
litaongeza ufanisi wa kazi na kila jambo kuwa wazi.
“Tumeanza kufanya
majaribio kwa kufanya kazi kwa njia ya mtandao tena kwa uwazi ambapo kila
mtumishi wetu atakachokuwa akikifanya kitaonekana jambo ambalo litasaidia
kuondoa changamoto na urasimu kazini” alisema Tukai.
Alisema hakuna
sababu ya kuficha taarifa za umma kwani kila mtu anatakiwa kuziona na kupitia
mfumo huo wa njia ya mtandao wataweza kuwabaini wafanyakazi wao pale
watakapokuwa wakifanya kazi chini ya kiwango.
Aidha Tukai alisema
MSD inatarajia kufungua Kampuni Tanzu ambayo itasimamia viwanda vya uzalishaji
ambavyo vitaendeshwa na MSD na wadau wengine.
Mfamasia Mkuu wa
Serikali Daud Msasi akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya
wakati akifungua semina hiyo alisema Serikali imetoa fedha Sh.Bilioni 200 kwa
ajili ya kununua dawa na vifaa tiba lakini fedha ambazo zimepokelewa na MSD ni
Sh. Bilioni 145.9.
Aidha Msasi
aliwataka wahariri wa vyombo vya habari
kuwasiliana na wahusika kabla ya kutoa habari ambazo zinaweza kuleta taharuki
kwa wananchi hasa zile zinazohusisha afya za watu.
Msasi alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai kwa kuboresha mambo kadhaa ya MSD kwa muda wa miaka miwili ya ufanyaji kazi wake tangu ateuliwe na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo.
Msemaji wa Serikali, Geryson Msigwa akizungumza katikasemina hiyo.
Mkurugenzi, Uendeshaji Huduma wa Mamlaka ya Ukaguzi wa Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Chrispin Severe akizungumza kwenye semina hiyo.
0 Comments