Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akiswaga ng'ombe katika hafla ya kukabidhi madume bora 40 ya ng'ombe kwa vikundi vya wafugaji wilayani Mkalama mkoani Singida Aprili, 6, 2023.
Na Dotto Mwaibale, Mkalama
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amekabidhi madume bora 40 ya
ng'ombe kwa vikundi vya wafugaji wilayani Mkalama mkoani Singida ukiwa ni
mkakati wa serikali wa kufanya mabadiliko ya sekta mifugo wenye lengo la
kuboresha mbari za mifugo ili kuwa na mifugo yenye tija zaidi.
Akikabidhi ng'ombe hao jana katika hafla iliyofanyika Kijiji Cha Iguguno
wilayani hapa, alisema serikali imenunua madume ya ng'ombe 366 kwa thamani ya
zaidi ya Sh.Milioni 878.4 ambao watagawiwa wafugaji kwenye halmashauri nane nchini.
Ulega alisema baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufungua milango, nchi
nyingi zimekuwa zikihitaji nyama kutoka Tanzania lakini bahati mbaya ng'ombe za
asili zinazofugwa na wafugaji hapa nchini hazina uzito nyingi zinakuwa kati ya
kilo 80 hadi 120 tu.
Alisema madume bora ng'ombe ambayo yamenunuliwa na serikali watoto
watakaozaliwa wa Zebra na Boran watakuwa na uzito wa kati ya kilo 150 hadi 200
na ubora unaotakiwa.
Aidha, Ulega aliwataka wafugaji nchini kuachana na fikra za kuwa na makundi
makubwa ya mifugo ambayo mingi inaishia kufa kwa ukame na badala yake wawe na
utaratibu wa kuivuna na kuiuza ili kuimarisha kipato chao na kuepukana na
hasara zinazoweza kuzuilika.
Alisema wafugaji wabadilike waachane na ufugaji kama wa enzi za mababu zetu wa kuwa na makundi mengi ya
ng'ombe ambao inapotokea ukame wanakufa na kusababisha hasara kwa mfugaji.
Aliongeza kuwa wafugaji waanze kumiliki maeneo yao kwa ajili ya malisho na
Halmashauri za Wilaya zihakikishe wafugaji ambao wana maeneo ya malisho
wanapimiwa na kupewa hati ili kuepusha migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza kati
ya wakulima na wafugaji.
Mkurugenzi Msaidizi Uzalishaji
Mifugo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Simon Lyimo alisema serikali imenunua madume
bora ya ng'ombe ambayo yamesambazwa kwenye halmashauri za Mkalama ambayo imepewa madume 40,Msalala
50,Chato 50,Maswali 50, Chamwino 50,Buchosa 46,Mvomero 40 na Halmashauri ya
Wilaya ya Mkulanga ambayo imepewa madume 50.
Lyimo alisema serikali imenunua madume hayo ikiwa ni mpango wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi katika mabadiliko ya
sekta mifugo ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuboresha mbari za mifugo
ili kuwa na mifugo yenye tija zaidi.
Afisa Mifugo Wilaya ya Mkalama, Joseph Michael, alisema madume hayo 40
yatagawiwa kwa kila kikundi dume mmoja na atatumika kwa wanakikundi wote ambapo
kikundi kitawajibika kumtunza,kumlisha na matibabu ili kumlinda ubora na
ufanisi wake.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali ameahidi kuwa wao kama wilaya
watahakikisha Madume hayo ya ng'ombe yanazalisha ng'ombe bora kama serikali
ilivyokusudiwa.
Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Isack , ameomba serikali kuongeza
kujenga majosho ya ng'ombe ili wilaya hiyo isikumbwe na magonjwa mbalimbali ya
mifugo.
Amesema kuwa endapo kutakuwa na majosho mengi mifugo itakuwa haina magonjwa
na hivyo kuzalisha nyama bora ambayo inakidhi masoko ya nje.
Baadhi ya wafugaji waliokabidhiwa Madume hayo ya ng'ombe kwa ajili ya
mbegu wameishukuru serikali kwa kutoa Madume hayo ambayo kwa sasa yatawasaidia
kuzalisha g'ombe bora.
Wamesema kupitia madume hayo watakuwa na mifugo bora itakayokuwa na mazao bora yanayotokana na mifugo, na hatimaye watainuka kiuchumi katika kaya zao.
0 Comments