Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Ally Mwanga (katikati) akiongoza kikao cha kawaida cha baraza la madiwani cha robo ya tatu kuanzia Januari hadi Machi 2023 kilichoketi wilayani humo May 18, 2023.Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Diwani wa Kata ya Mkiwa Stephen Mtyana na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Haika Masawe.
Na Dotto Mwaibale, Ikungi
HALMASHAURI ya Wilaya ya Ikungi inatarajia
kuanzisha vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea chanzo cha mazao ya
kilimo pekee ambacho sio cha uhakika.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa halmashauri
hiyo Ally Mwanga wakati akifanya majumuisho katika kikao cha kawaida cha robo
ya tatu kuanzia Januari hadi Machi 2023 kilichoketi May 18, 2023.
Hatua ya Mwenyekiti huyo kuzungumza hivyo
ilifuatia maombi ya baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo kuwataka watalaam wa
wilaya hiyo kubuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitaisaidia halamshauri
kupata fedha za kuiendesha badala ya kutegemea ushuru wa mazao pekee na samaki.
Diwani wa kwanza kutoa ombi hilo alikuwa ni
Innocent Makomelo Diwani wa Kata ya Mang’onyi ambaye alisema halmashauri hiyo
haiwezi kutegemea chanzo cha mazao badala yake iangalie vyanzo vingine kama
stendi za mabasi ambazo zikihimalishwa kitakuwa ni chanzo cha mapato cha
kudumu.
“ Mheshimiwa Mwenyeki ifike mahala stendi yetu ya
mabasi ya Ikungi ianze kufanya kazi na maeneo mengine ambayo tulipendekeza
ziwepo kwani kila siku magari na watu wanasafiri tukitengeneza hizi stendi zetu
na tukiweka utaratibu mzuri hizi stendi zitakuwa ni chanzo kizuri cha mapato
kuliko hivi vyanzo vingine,” alisema
Makomelo.
Alisema katika kikao hicho kila diwani ambaye alikuwa
akisisimama na kuulizwa mapato yaliyokusanywa anasema msimu haukuwa mzuri hivyo
aliomba ombi lake la kuhimarisha vyanzo vipya vya mapato litiliwe maanani.
Hata hivyo Makomelo alisema mjini Singida
halmashauri hiyo inaeneo lao ambalo waneweza kuweka uwekezaji hata wa hoteli lakini
kila wanapokutana haoni wataalam wa halmashauri hiyo wakija na mawazo na
mikakati mizuri ya kueleza jinsi ya kuliendeleza na kulifanya kuwawezesha wapate
fedha na kuwa mwaka huu na ujao utapita wataendelea kupewa mipango bila ya kuja
na maamuzi.
“Tunawaomba waje na maamuzi tuone kama baraza
hili litashindwa mheshimiwa Mwenyekiti maeneo haya ni ya kwetu hakuna mtu
atakayekuja kutuamlia tunashindwa wapi’” alihoji Makomelo.
Alisema shida anayoiona hapo ni ndogo kwani
mfanyabiashara anaweza kupewa Sh.Milioni 10 akafanya biashara kubwa lakini sio
hao wataalam ambao wakipata bilioni moja hela hiyo itaishia kwenye mipango
mikakati na michakato na mwisho kuletewa makaratasi yanayoelezea mambo
mbalimbali yaliyofanyika sijui walifanya hiki na kile.
Diwani mwingine aliyechangia jambo hilo alikuwa
ni Diwani wa Kata ya Iyumbu Peter Kweligwa ambaye kata yake ni maarufu kwa
kilimo cha mpungu na ndio ni tegemeo kubwa la halamshauri ya Ikungi kwa kupata
mapato Ikiwemo kata ya Mgungila.
Kweligwa aliomba kujengwa kwa miundombinu ya
umwagiliaji kutokana na eneo lake kuwepo kwa mito mikubwa na hiyo itasaidia
sana kuliko kutegemea mvua ambazo zina msimu wake.
Diwani wa Kata ya Mungaa, Gabriel Dulle aliungana
na Diwani Makomelo kuhusu ujenzi wa stendi za mabasi akitolea mfano stendi ya
mabasi ya Makiungu ambayo alisema inauwezo wa kuingiza zaidi ya Sh.Milioni 12
kwa mwezi lakini bado hawakioni kama ni chanzo cha mapato cha kudumu.
Diwani mwingine aliyehoji kuhusu stendi kuwa ni
chanzo cha mapato cha kudumu ni Diwani wa Kata ya Ntuntu, Omari Toto ambaye
alihoji fedha inayokusanywa katika stendi hiyo inachukuliwa na nani.
Wakitoa taarifa ya mapato katika kata zao baadhi
ya madiwani walisema changamoto kubwa inayosababisha mapato kushuka ni kuwa na
mashine chache za kukatia ushuru yaani POS na vitendea kazi vingine kama
usafiri wa pikipiki na vijiji vingi kukosa watendaji wa kusimamia ukusanyaji wa
mapato hayo.
Akijibu kuhusu changamoto hiyo Kaimu Mkurugenzi
wa Halmashauri hiyo, Haika Masawe alisema mashine ya POS walizokuwa nazo ni 50
na sasa zimekwisha nunuliwa 10 nyingine zitakazo kwenda kuongeza nguvu ya
ukusanyaji wa mapato na kuwa wamepata watendaji wapya wengine 10 ambao watapangwa kimkakati kwenye vijiji ambavyo hawakuwa nao kutokana na sababu mbalimbali wakiwepo
walioenda masomoni.
Masawe alisema mambo yote yaliyojiri kwenye kikao
hicho yatafanyiwa kazi ili kuifanya halamshauri hiyo kuwa juu kimapato.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Ally alisema halmashauri yoyote haiwezi kupiga
hatua ya maendeleo bila ya kuwa na mapato ya kutosha hivyo madiwani wanakila
sababu ya kuwa mstari wa mbele katika kukusanya mapato kwenye maeneo yao ikiwa
ni pamoja na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato.
Aidha Mwanga alisema mtendaji yeyote
atakayebainika kuhujumu zoezi zima la ukusanyaji wa mapato kwa njia moja ama
nyingine hawatamvumilia na kuwa atachukuliwa hatua kali.
Alisema hivi sasa ajenda yao kubwa iwe ni
kukusanya mapato tena kwa nguvu zao zote ili halmashauri hiyo iwe kinara kwa
kukusanya mapato mkoani hapa.
Alisema mapato ndio injini ya halmashauri hivyo
ni jukumu la kila mmoja wao kuhakikisha yanakusanywa kutoka katika vyanzo
mbalimbali kwani ndiyo yanayosaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kutoka vyanzo vya ndani.
Katika baraza hilo madiwani walipata fursa ya
kutoa taarifa mbalimbali ya matumizi ya fedha katika miradi na kujadiliana
mbinu za ukusanyaji wa mapato huku kata za Mgungila, Mwaru, Ikungi na Iseke
zikiwa vinara kwa ukusanyaji mapato ambapo zikipongezwa huku zile ambazo
zilionekana kushuka kimapato zikitakiwa kuongeza bidii kwa kujifunza kutoka kwa
zile zilizofanya vizuri.
Baadhi ya watendaji wa Kata, Vijiji na Watumishi
wa halmashauri ya wilaya hiyo wakiwa kwenye baraza hilo.
Baadhi ya watendaji wa Kata, Vijiji na Watumishi na wataalam mbalimbali wa wilaya hiyo wakiwa kwenye bazaza hilo.
Diwani wa Kata ya Mtunduru Ramadhan Mpaki akichangia
jambo kwenye baraza hilo. Kushoto ni Diwani wa Viti Maalum, Subira Kitiku.
Diwani wa Kata ya Mungaa Gabriel Dulle akichangia jambo kwenye baraza hilo.








No comments:
Post a Comment