TANESCO SINGIDA YATOA MATOFALI KUSAIDIA UJENZI WA MADARASA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Sunday, December 3, 2023

TANESCO SINGIDA YATOA MATOFALI KUSAIDIA UJENZI WA MADARASA

Afisa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida, Juma Omari (katikati kushoto) akipeana mkono na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mnung'una, Bahati Ramadhani ikiwa ni ishara ya kumkabidhi matofali 300 yaliyotolewa na shirika hilo kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa madarasa katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Disemba 2, 2023. Wengine katika picha ni wafanyakazi wa Tanesco na walimu wa shule hiyo.

..................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia kwa Mkurugenzi wake Mtendaji , Gissima Nyamo-Hanga limekuja kivingine baada ya shirika hilo  Mkoa wa Singida kutoa matofali 300 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Mnung'una iliyopo Wilaya ya Singida mkoani hapa.

Akikabidhi matofali hayo Disemba 2, 2023 kwa uongozi wa shule hiyo kwa niaba ya Meneja wa Shirika hilo Mkoa wa Singida, Afisa wa Tanesco, Juma Omari alisema wametoa matofali hayo ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kusomea kwa kujengewa miundombinu mizuri.

"Hatua hii ya utoaji wa matofali haya ni agizo la Mkurugenzi wetu Mtendaji wa Tanesco  Gissima Nyamo-Hanga alilolitoa kupitia Meneja wetu kuja kutoa msaada huu ambao umelenga kuwasaidia wanafunzi kupata mazingira bora ya kusomea," alisema Omari.

Omari alisema utoaji wa msaada wa namna hiyo utakuwa  endelevu na utafanyika  katika shule zingine za msingi mkoani hapa ambapo alitumia nafasi hiyo kuyaomba mashirika mengine nayo kujitoa kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa miundombinu ya shule zetu.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Bahati Ramadhani akipokea msaada huo alilishukuru shirika hilo kwa kutekeleza ahadi yao waliyoitoa katika mahafali ya darasa la saba ya mwaka huu baada ya kuwaomba kuchangia chochote katika ujenzi wa madarasa.

"Leo tunafuraha kubwa ya kupokea matofali haya ikiwa ni ahadi iliyotolewa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida ahadi yao wameitimiza kikamilifu tunawashukuru sana na tunawaomba waendelee kuwa na moyo huo huo wa kusaidia ujenzi wa shule mbalimbali mkoani hapa," alisema Ramadhani.

Mwalimu Mkuu huyo alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga miundombinu katika shule mbalimbali na kuwa na katika shule hiyo ya Mnung'una amewapa fedha kwa ajili ya kujenga vyoo na kuondoa kabisa changamoto iliyokuwepo ya ukosefu wa vyoo.

Aidha, aliwaomba wadau wengine yakiwemo mashirika ya umma kuiga mfano wa shirika hilo kwa kujitoa kusaidia shughuli za maendeleo ya kijamii badala ya kusubiri kazi hizo kufanywa na Serikali.Wafanyakazi wa TANESCO wakishusha matofali hayo wakati wa kuyakabidhi kwa uongozi wa shule hiyo.

Matofali yakishushwa wakati wa makabidhiano hayo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bahati Ramadhani akisaidia kuyashusha matofali hayo.
Muonekano wa matofali hayo baada ya kukabidhiwa.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad