Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman (wa pili kulia), Mbunge wa Dodoma Mjini, ambaye pia ni Waziri wa Madini (katikati), Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Alhaji Jabiri Shekimweri (wa pili kushoto) waakimkabidhi mtungi ya gas Mama Lishe Elizabeth Chiute katika hafla ya kuwakabidhi mitungi hiyo Mama Lishe na Baba Lishe wa Mjini Dodoma iliyofanyika Januari 13, 2024. Kulia ni Naibu Meya wa Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma Mjini, Asma Karama.
.................................................................
Na Mwandishi Wetu Dodoma
KAMPUNI ya Oryx Gas kwa kushirikiana na Mbunge wa
Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Waziri wa Madini wamegawa bure mitungi ya
gesi 500 pamoja na majiko yake kwa Baba na Mama Lishe wa Jimbo hilo kwa lengo
la kuwawezesha kurahisha shughuli zao za kuandaa chakula sambamba na kulinda
afya zao.
Akizungumza leo Julai 13,2024 wakati wa kugawa
mitungi hiyo, Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema mitungi
hiyo 500 ya gesi ya oryx na majiko yake yamegharimu Sh.milioni 41 na kwamba
wataendeela kufuata maelekezo ya serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu
Hassan inayohamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuendeela kugawa
mitungi hiyo kwa wananchi wa makundi mbalimbali.
Amesema Oryx Gas wanaamini kupika kwa gesi
kunalinda mazingira kwa kuacha kukata kuni na mkaa lakini inalinda afya kwa
kuwaepusha kuvuta moshi na mvuke unaoathiri mapafu na afya yao unaotokana na
kuni na mkaa hivyo Baba na Mama Lishe ni kundi ambalo wanalipa kipaumbele kwa
kutambua ndilo linatumia zaidi kuni na mkaa kila siku kwa shughuli zao za
kuandaa chakula.
Pia amesema kwa kutumia nishati safi ya kupikia
inayotokana na gesi wanawake wanatumia muda mchache kupika, hivyo wanapata
nafasi kufanya shughuli nyingine za maendeleo na kuepuka kugombana na wenza wao
kwa kuchelewesha chakula.
“Katika ngazi ya familia tunafahamu kuna watoto
ambao wamekuwa wakienda kutafuta kuni na hivyo kutumia muda mwingi kusaka kuni
na kukosa muda wa kutosha wa kusoma na kwenda darasani, hivyo kutumia gesi
kutasaidia watoto kupata muda wa kusoma na kulinda afya zao.kwa miaka mingi
Oryx Gas tumekuwa kiongozi katika kukuza matumizi ya gesi nchini.
“Kuanzia Julai mwaka 2021 tumekuwa mstari wa
mbele kutekeleza maelekezo ya Serikali tulioyapokea kutoka kwa Rais Dk. Samia
Suluhu Hassan kuwa ifikapo mwaka 2023 asilimia 80 ya wananchi watumie nishati
safi ya kupikia,” amesema na kusisitiza kupitia mipango hiyo, Oryx Gas inataka
kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini
Athony Mavunde amesema wanashukuru kwa kupata majiko hayo huku akieleza na wao
wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaenzi kampeni ya kutunza mazingira hasa kwa
kuwa na mipango mbalimbali ili wananchi wengi wasitumie nishati ya kuni na mkaa
ambayo kwa kiwango kikubwa inaharibu mazingira.
Amesisitiza anaishukuru anawashukuru Kampuni ya
Oryx chini ya uongozi wa Araman Benoite kwa kukubali ombi lao la kuwashika
mkono Baba na Mama Lishe wa Dodoma Mjini kwa kuwapatia majiko ya gesi na majiko
yake , hivyo kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanalinda mazingira.
“Pia nichukue fursa hii kumshukuru Rais Dk.Samia
Samia Suluhu Hassan ambaye yeye ndio muasisi wa utunzaji mazingira kwa kutumia
nishati safi na alitoa maelekezo kwamba ifikapo mwaka 2032 basi asilimia 80 ya
wananchi wawe wanatumia nishati safi ili kuondokana na uchafuzi wa mazingira
ambao umesababisha mabadiliko ya tabianchi kwa kiwango kiwango kikubwa.
“Tunamshuku Rais Samia kwa kuweka kipaumbele na
kuwa kidede kusimamia jambo hili na kama mnavyoweza kuona mitingu ambayo
imetolewa hapa itapunguza matumizi ya mkaa na tukipunguza matumizi ya kuni na
mkaa tututakuwa tumepunguza uharibifu wa mazingira pamoja na kulinda afya zetu
kwani tunatambua watumiaji wa kuni na mkaa wamekuwa wakipata madhara ya kiafya
kwa kuvuta moshi na hasa baba na mama lishe.”
Amesema kampeni ya Rais Samia kuhamasisha nishati
safi inakwenda kuokoa maisha ya baba na mama lishe ambao kwa sehemu kubwa muda
wao mwingi unatumika kupika na wengi wao wanatumia kuni na mkaa, hivyo kupitia
nishati hiyo wanakwenda kuepukana na madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi
ya kuni na mkaa.
Wakati huo huo Mbunge wa Viti Maalum Tanzania
Bara anayewakilisha kundi la Asasi za Kiraia kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM)
Neeema Lugangira amesema anaelewa changamoto ambazo wanawake wanazipitia katika
kuandaa chakula nyumbani.
“Kunachangamoto za akina mama kutumia muda mwingi
kwenda kutafuta kuni , watoto wanatumia muda mwingi kwenda kutafuta kuni.Kuna
kadhia nyingi ambazo tunazipitia wakati wa kwenda kutafuta kuni ikiwemo ukatili
wa kijinsia , muda mwingi tunaotumia kutafuta kuni muda ule tungeweza kufanya
shughuli nyingine za kiuchumi.
“Kwahiyo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alipokuja na
ajenda ya kutafuta nishati safi na salama ya kupikia moja ni kuokoa afya zetu
kwani akina mama na watoto wanapata madhara makubwa kutokana na moshi ule ambao
tunavuta wakati wa kupika,”amesema.
Awali Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini Alhaj Jabiri
Shekimweri amepomngeza Waziri Mavunde kwa jinsi anavyojitoa kwa ajili ya
wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini wakiwemo Baba na Mama Lishe huku akitumia
nafasi hiyo kusisitiza ni vema walipewa mitungi ya gesi na majiko yake
kuhakikisha wanaitumia vema gesi hiyo ili wasipate madhara.
“Nitoe rai kwa wote ambao wamepatiwa gesi
hii,kabla ya kuitumia wapate elimu kuhusu namna nzuri ya kutumia gesi bila
kupata madhara.Nimefurahi kusikia Oryx pamoja na kutoa mitungi hii wameamua
kutoa na elimu kuhusu matumizi sahihi ya mtungi wa gesi.”
Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman, akizungumza wakati wa kukabidhi mitungi hiyo.
Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman (katikati) akiwa meza kuu na viongozi mbalimbali wakati wa hafla hiyo ya kukabidhi mitungi hiyo. Kulia ni Mbunge wa Dodoma mjini, Anthony Mavunde ambaye ni Waziri wa Madini na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Alhaj Jabiri Shekimweri.
Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman, akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ambaye pia ni Waziri wa Madini wakati wa hafla hiyo.
Hafla ya makabidhiano ya mitungi hiyo ya gas ikiendelea kufanyika. Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ambaye pia ni Waziri wa Madini, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Alhaj Jabiri Shekimweri.na Mbunge wa Viti Maalum Tanzania Bara anayewakilisha kundi la Asasi za Kiraia kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Neeema Lugangira.










No comments:
Post a Comment