MAKAMU WA RAIS AZINDUA MPANGO JUMUISHI WA WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII

Subscribe Us

MAKAMU WA RAIS AZINDUA MPANGO JUMUISHI WA WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akizindua Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya ya Jamii Jijini Dar es Salaam Januari 31, 2024.

................................................................................

HOTUBA YA UZINDUZI WA MPANGO HUO ILIYOSOMWA NA MAKAMU WA RAIS

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Napenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na kutuwezesha kushiriki tukio hili la kihistoria la uzinduzi wa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (Integrated and Coordinated Community Health Workers’ Program). 

Pili, namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan – ambaye ndiye aliyealikwa kuwa Mgeni Rasmi lakini kutokana na majukumu mengi ya Kitaifa yanayomkabili – amenipa heshima ya kumwakilisha katika tukio hili. Nawashukuru Viongozi, Wageni Waalikwa, Wananchi na Wadau kwa kutenga muda wenu ili kushiriki katika tukio hili. 

Aidha, naipongeza kwa dhati Wizara wa Afya kwa kuratibu na kutekeleza mipango mbalimbali inayolenga kulinda na kuimarisha afya ya wananchi. Waheshimiwa Viongozi na Wageni Waalikwa; Serikali kupitia Wizara ya Afya inashirikiana na Wadau mbalimbali katika kutekeleza mikakati ya kuimarisha huduma za afya nchini ili kufikia azma ya Afya kwa Wote (Universal Health Coverage) ifikapo mwaka 2030. 

Mpango huu pia ni sehemu ya mkakati mahususi wa kuleta uwiano katika upatikanaji wa huduma za afya na lishe bora kwa wote pamoja na kukabiliana na upungufu wa Watumishi katika sekta ya afya. Ili kufikia azma hii, Serikali kupitia Wizara ya Afya imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha ubora na upatikanaji wa huduma za afya nchini kwa kuwekeza katika miundombinu ya afya, vifaa tiba, dawa, huduma za kinga na rasilimali watu katika ngazi mbalimbali.

Mathalan, uwekezaji mkubwa umefanyika katika eneo la miundombinu kwa kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia Hospitali ya Taifa, Hospitali Maalum, Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati katika Mikoa yote nchini. 

Halikadhalika, Serikali imeongeza bajeti ya dawa pamoja na kuhakikisha fedha za ununuzi wa dawa zinatolewa kikamilifu kila mwezi. Katika azma hiyo, Serikali imenunua jumla ya magari ya wagonjwa (ambulances) 589, vitanda vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU beds) 375 na vifaa vya uangalizi kwa watoto wachanga (Neonatal Intensive Care Units, NICU) 123. 

Waheshimiwa Viongozi na Wageni Waalikwa; Rasilimaliwatu ni muhimu katika kuimarisha ubora wa huduma za afya zinazotolewa katika ngazi mbalimbali nchini. 

Pamoja na umuhimu huo, kuna upungufu mkubwa wa rasilimaliwatu katika Sekta ya Afya kwani uhitaji uliopo hivi sasa ni mkubwa (takriban 64%), ambapo uhitaji mkubwa upo katika Vituo vya kutolea huduma za afya kwa ngazi ya msingi. 

Ili kuhakikisha ubora na upatikanaji wa huduma za afya hususan huduma za afya ya msingi (Primary Health Care, PHC) kwa wananchi wote, ni muhimu kuimarisha mifumo ya huduma za afya ya jamii ikiwemo kuwatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (Community Health Workers). 

Wahudumu hawa watasaidia kutoa huduma za afya ya msingi na uchunguzi wa awali ngazi ya jamii, huduma za kinga, elimu ya afya na uhamasishaji wa masuala mbalimbali ya afya kulingana na miongozo iliyopo na itakayoandaliwa kulingana na mahitaji.

 Katika muktadha huo, Mpango huu wa huduma za afya jamii unatekeleza kwa vitendo dhana ya ‘kinga ni bora kuliko tiba’ ambayo pamoja na faida nyingine utaipunguzia Serikali gharama kubwa za ununuzi wa dawa, ambapo kwa mwaka 2023/24 imefikia takribani shilingi bilioni 200. 

Waheshimiwa Viongozi na Wageni Waalikwa; Kama alivyozungumza Waziri wa Afya, Tanzania ina historia ndefu katika utekelezaji wa huduma za afya ngazi ya jamii. 

Historia hii inaanzia miaka ya 1970 ambapo utekelezaji wa huduma hizi ulifanyika kupitia kwa Wahudumu wa Afya vijijini (Village Health Workers, VHWs) ambao walitekeleza afua za afya katika maeneo ya afya na usafi wa mazingira, kuzuia na kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kama vile Kifua Kikuu (TB), Afya ya Mama na Mtoto na masuala mengine yahusuyo elimu ya afya na uhamasishaji jamii ili kujenga uelewa, kuchochea mabadiliko ya tabia na kuzingatia kanuni za afya na lishe bora. 

Waheshimiwa Viongozi na Wageni Waalikwa; Pamoja na umuhimu wa Wahudumu hawa katika utoaji wa huduma za afya nchini, bado kumekuwepo na changamoto za uratibu, usimamizi na mafunzo hususan kwa Wahudumu wanaotekeleza afua za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii. 

Changamoto hizi zimekuwa zikiathiri mifumo ya utoaji wa huduma za afya katika jamii zetu. Utekelezaji wa Mfumo wa watoa huduma za afya ngazi ya jamii unaoendelea hivi sasa unaambatana na changamoto ambazo zinaweza kuchangia kuathiri jitihada za Serikali kufikia azma ya Afya kwa Wote ifikapo mwaka 2030. 

Waheshimiwa Viongozi na Wageni Waalikwa; Katika kukabiliana na changamoto zilizopo hivi sasa, Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na Wadau mbalimbali imeandaa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (Integrated and Coordinated Community Health Workers’ Program) ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya ya msingi nchini. 

Mpango huu unalenga kuboresha taratibu za kuwachagua Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, kurasimisha mafunzo na usimamizi na kuboresha ushiriki wa jamii katika hatua zote za utekelezaji. Jitihada hizi zikifanikiwa zitaimarisha kwa kiasi kikubwa afua jumuishi za afya-kinga nchini. 

Waheshimiwa Viongozi na Wageni Waalikwa; Ili kutekeleza mpango huu, Serikali ya Awamu ya Sita imepanga kuajiri na kuwajengea uwezo jumla ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wapatao 137,294 katika Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara. 

Utekelezaji wa Mpango huu utafanyika katika kipindi cha miaka mitano kwa awamu ambapo katika mwaka wa kwanza (2023/24) zaidi ya Wahudumu 28,000 watafikiwa na baadaye wastani wa Wahudumu 27,324 kila mwaka kwa kipindi cha miaka minne (4) mfululizo kuanzia mwaka 2024/25 hadi 2027/28. 

Wahudumu hawa watachaguliwa katika ngazi ya Kitongoji katika maeneo ya vijijini na Mtaa katika maeneo ya mijini na wanatakiwa kuwa ni wakazi wa sehemu husika. 

Kila Kitongoji na Mtaa utakuwa na Wahudumu wawili (Mwanaume na Mwanamke) na Mpango huu utatekelezwa katika Vitongoji vyote 64,384 na Mitaa yote 4,263 ya Tanzania Bara. Hii ni fursa adhimu, hivyo natoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kuchangamkia fursa hii muhimu ya ajira na huduma kwa jamii. 

Aidha, katika hili Wizara ya Afya na TAMISEMI, ziangalie idadi ya wahudumu kwa Mtaa/Kitongoji ili kuendana na idadi ya watu badala ya utaratibu uliowekwa wa Wahudumu wawili kwa kila Kitongoji na Mtaa. 

Kulingana na Sensa ya 2022, msongamano wa watu katika Taifa letu unatofautiana kutoka 12/km2 katika mikoa yenye wakazi wachache, kama vile Katavi, hadi 3,133/ km2 katika mikoa yenye wakazi wengi, kama vile Dar es Salaam. 

Waheshimiwa Viongozi na Wageni Waalikwa; Nimefahamishwa kuwa katika mpango huu tutakaouzindua leo, Wahudumu wa afya ngazi ya jamii watatoa aina 4 za huduma za afya ambazo ni elimu ya afya, huduma za afya-kinga, huduma tembezi na mkoba na baadhi ya huduma za awali za tiba (Basic Curative Services at community level) kabla ya kutoa rufaa. 

Pamoja na kuchangia utatuzi wa changamoto mbalimbali za Sekta ya Afya nchini, Mpango huu umeweka kipaumbele zaidi katika Huduma za Lishe, Afya ya Mama, Mtoto, Vijana na Uzazi wa Mpango, Magonjwa ya Kuambukiza hususan (Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu); Magonjwa Yasiyoambukiza, Usafi na Afya ya Mazingira, Magonjwa ya Mlipuko na Dharura, Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na masuala ya Ustawi wa Jamii. Utekelezaji wa Mpango huu utazingatia kanuni, taratibu na miongozo iliyopo. 

Hivyo, ninawaelekeza Viongozi wote wanaohusika katika ngazi zote kuhakikisha zoezi la kuwachagua Wahudumu hawa linafanyika kwa kufuata vigezo na taratibu zilizowekwa, ili kupata Wahudumu wenye sifa stahiki watakaotekeleza majukumu haya. Kwa wale watakaopewa jukumu la kutekeleza mpango huu, nawasihi wajiepushe na vitendo vya upendeleo, rushwa au ukiukwaji wa taratibu. 

Waheshimiwa Viongozi na Wageni Waalikwa; Katika kutekeleza Mpango huu, Serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh. 899,473,291,955.64 kwa kipindi cha miaka mitano. 

Aidha, kiasi cha Sh. 99,678,320,000 zinahitajika katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji. Huu ni uwekezaji mkubwa sana, unaohitaji rasilimali fedha nyingi zitakazowezesha utekelezaji wa Mpango huu. 

Naishukuru Taasisi ya Susan Thompson Buffet Foundation ya Marekani iliyoahidi kuchangia utekelezaji wa Mpango huu kila mwaka. Natoa wito kwa Wadau wa Maendeleo katika Sekta ya Afya na wadau wengine wa ndani na nje kutuunga mkono. 

kwa kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha za kutekeleza Mpango huu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. Waheshimiwa Viongozi na Wageni Waalikwa; Ninapoelekea mwisho wa hotuba yangu napenda kutumia fursa hii kwanza, kuhimiza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Mamlaka nyingine zinazohusika kuhakikisha usimamizi madhubuti wa Mpango huu ili uweze kufikia malengo yake. 

Ni lazima kuweka mfumo mzuri wa uratibu wa shughuli za Mpango huu na kuhakikisha taarifa za utekelezaji zinapatikana. 

Aidha, mnaweza kujifunza na kupata uzoefu kutoka Zanzibar, ambayo imeanza kusimamia na kutekeleza Mpango huu kwa kutumia mifumo ya kidigitali tangu Desemba 16, 2023. Pili, Wizara ya Afya itoe hamasa na elimu ya kutosha kwa jamii kuhusu Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ili kurahisisha utekelezaji wake. 

Tatu, natoa rai kwa jamii kuupokea Mpango huu na kuthamini huduma za wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kuwapa ushirikiano wa kutosha ili kulinda na kuboresha afya katika jamii zetu. Nne, nawasihi wahudumu wa afya watakaopewa dhamana ya kutekeleza jukumu hili kuzingatia weledi na kujituma. 

Tano, naiomba Jumuiya ya Kimataifa, Wadau wa Maendeleo na Wadau wengine kuunga mkono juhudi za Serikali pamoja na vipaumbele vya Mpango huu vilivyoainishwa, wakati wote wa utekelezaji. 

Mwisho, natoa rai kwamba masuala ya lishe bora na usafi wa mazingira yasiachwe nyuma katika kutekeleza Mpango huu, kama njia mojawapo ya kujenga afya na kudhibiti magonjwa ambayo yanatokana na uchafuzi wa mazingira, kwa mfano kipindupindu na malaria. 

Waheshimiwa Viongozi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana; Mwisho kabisa, nawashukuru tena kwa ushiriki wenu na natumaini kwamba baada ya uzinduzi wa Mpango huu, nchi yetu itakuwa imeanza safari mpya kuelekea katika kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma za afya kuanzia katika ngazi ya kaya. 

Baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa nipo tayari kwa ajili ya kufanya uzinduzi rasmi wa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii. Viongozi mbalimbali wakiwa meza kuu wakati wa ufunguzi wa mpango huo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akizindua Mpango huo.
Uzinduzi huo ukifanyika.
Wadau mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi wa mpango huo.

 Uzinduzi ukifanyika.

Post a Comment

0 Comments