Na Dotto Mwaibale, Singida
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Singida
imeokoa zaidi ya Sh.Milioni 156 baada ya kufuatilia utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo.
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Sipha Mwanjala akitoa taarifa kwa
waandishi wa habari Januari 31, 2024 ya utendaji kazi kwa kipindi cha Oktoba
hadi Desemba 2023 alisema miradi iliyofuatiliwa ilikuwa ni 11 yenye thamani ya zaidi ya Sh.Bilioni 5 katika sekta za Elimu na
Afya.
Mwanjala alisema miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa Shule za Sekondari za kutwa na za Kata iliyotekelezwa kupitia mradi wa kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP)
ambao unahusisha ujenzi na ukarabati wa Shule za Sekondari na kuwa fedha hizo pia zinahusisha ujenzi wa vituo vya
Afya.
"Katika ufuatiliaji huo, fedha kiasi cha Sh. 10,220,000/= ziliokolewa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika ujenzi wa Kituo cha Afya Gumanga na Ilunda kutokana na milango aina ya 'flash door' iliyokuwa imewekwa awali
kukosa ubora uliokuwa unatakiwa kwa mujibu wa BOQ, hivyo kulazimika kuiondoa na kuweka milango aina ya 'Hard wood' doors yenye ubora uliotakiwa kwa mujibu wa BOQ,"
alisema Mwanjala.
Aidha, Mwanjala alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni fedha kiasi cha fedha Sh. Milioni 110.5 ziliokolewa, kutokana na kufanya malipo ya vifaa vilivyoagizwa kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa
Singida Solya kabla ya Mzabuni huyo kupeleka vifaa hivyo ili
vikaguliwe, vikubaliwe na kupokelewa.
Alisema baada ya TAKUKURU kufuatilia, mzabuni huyo alipeleka vifaa vyote vilivyokuwa vimeagizwa.
Mwanjala alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi fedha kiasi cha Sh. 1,100,000/= ziliokolewa kutokana na kodi ya zuio ambayo ilikatwa kwa wazabuni waliotoa huduma katika ujenzi wa Shule ya Sekondari Iyumbu kwa ajili ya kupelekwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) lakini hazikupelekwa na baada ya ufuatiliaji uliofanywa na TAKUKURU fedha hizo zimepelekwa TRA.
Katika kipindi hicho Mwanjala alisema TAKUKURU ilifanya chambuzi sita za mifumo ili kubaini mianya ya rushwa iliyopo katika maeneo mbalimbali na kisha kushauri namna ya kuiziba ambapo pia walifanya warsha tano kujadili mianya ya rushwa iliyobainika katika chambuzi zilizofanyika na kuweka mikakati ya kuziba.
Alisema kutokana na uchambuzi wa mfumo wa ulipaji na ukusanyaji kodi ya zuio uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi,fedha kiasi cha Sh. Milioni 25 kiliokolewa Manyoni na fedha kiasi cha Sh. Milioni 9.9 ziliokolewa Itigi kutokana na kodi ya zuio ambayo ilikatwa na Halmashauri hizo kwa watoa huduma mbalimbali muda mrefu kwa ajili ya kupelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA) lakini hazikupelekwa na baada ya uchambuzi huo fedha hizo zimepelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA)
Mwanjala alisema TAKUKURU Mkoa wa Singida iliendelea na utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwa kufanya vikao 23 katika kata 23 na makundi mbalimbali ya wadau na kuwa kupitia vikao hivyo wadau waliibua kero 102 na kueleza kuwa kati ya kero 102 zilizoibuliwa, kero 79 zimetatuliwa na kero 23 zinaendelea kutatuliwa.
Akizungumzia kuhusu Elimu kwa Umma TAKUKURU Mkoa wa Singida iliwaongezea wananchi uelewa kuhusu rushwa ambapo wananchi 13,601 (wanaume 6,971 na wanawake 6,630) walipata elimu hiyo kupitia Semina 61 kwenye makundi mbalimbali wakiwemo watumishi wa Umma, mikutano ya hadhara 53, maonesho 7, Kutembelea na kuimarisha Klabu za Wapinga Rushwa 58 katika Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo.
Mwanjala akizungumzia uchunguzi na
mashtaka alisema malalamiko 69 yalipokelewa kwa kipindi hicho
ambapo malalamiko 34 yalihusu vitendo vya rushwa na
malalamiko 35 hayakuhusu vitendo vya rushwa.
"Malalamiko 34 yaliyohusu rushwa uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali, malalamiko 35 ambayo hayakuhusu rushwa walalamikaji walishauriwa kadiri malalamiko yenyewe yalivyokuwa yakiendelea,"
alisema Mwanjala.
Alisema katika kipindi cha miezi hiyo kesi 10 zilifunguliwa mahakamani, kesi 7 ziliamuliwa, kesi 3 zilishinda na kesi 4 zilishindwa na jumla ya kesi 27 zinaendelea
Mahakamani.
Akielezea mikakati ya TAKUKURU Mkoa wa Singida ya utendaji kazi kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2024 wataendelea kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali zinazoelekezwa Mkoa wa Singida kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wataendelea kuwaongezea uelewa wananchi kuhusiana na masuala ya rushwa ili wananchi washiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo vya Rushwahasa katika miradi ya maendeleo inayoendelea katika maeneo yao na kuendelea kutekeleza Programu ya TAKUKURU – Rafiki.
Mwanjala alitoa wito kuwa TAKUKURU Mkoa wa
Singida inatoa RAI kwa wananchi wote kujiepusha na
vitendo vya rushwa na kushiriki kikamilifu katika kuzuia
vitendo hivyo vinavyotokea katika maeneo mbalimbali ya kutolea
huduma za kijamii na hasa katika utekeleaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Alisema kwa taarifa ya vitendo vya rushwa wasiliana nao kwa njia zifuatazo:
i. Fika Ofisi za TAKUKURU (M) Singida na Wilaya za Iramba, Ikungi, Mkalama na Manyoni.
ii. Kupiga simu ya bure 113 au simu ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa na Wakuu wa TAKUKURU wa Wilaya kwa
namba zifuatazo:
Na Mkoa /Wilaya NAMBA YA SIMU
1 RBC –SINGIDA 0738150208
2 DBC - Mkalama 0738150 212
3 DBC - Ikungi 0738150213
4 DBC - Iramba 0738150 210
5 DBC - Manyoni 0738150 211
iii. Kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kushiriki kutoa ushahidi Mahakamani. Maafisa wa Takukuru wakiwa kwenye kikao hicho.Kikao na waandishi wa habari kikiendelea.Mkutano na waandishi wa habari kikiendelea.Taswira ya kikao hicho.Muonekano wa Jesho la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida.
0 Comments