MSD YAANZA USAMBAJI VIFAA TIBA VYA BILIONI 14.7 MAJIMBONI MOROGORO VILIVYOTOLEWA NA SERIKALI

Subscribe Us

MSD YAANZA USAMBAJI VIFAA TIBA VYA BILIONI 14.7 MAJIMBONI MOROGORO VILIVYOTOLEWA NA SERIKALI

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima (katikati) akiwaongoza viongozi mbalimbali kukata utepe kuashiria upokeaji wa vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Januari 17, 2024.

....................................................

Na Mwandishi Wetu,Morogoro 

BOHARI ya Dawa (MSD) imeanza usambazaji wa vifaa tiba majimboni vilivyonunuliwa na Serikali vyenye  thamani ya zaidi ya Sh bilioni 14.7 kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati  lengo likiwa ni kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Meneja wa MSD, Kanda ya Mashariki yenye mikoa ya  Dar es Salaam, Pwani ,Morogoro na Visiwani Zanzibar, Betia Kaema alisema hayo wakati wa makabidhiano ya  vifaa hivyo na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro , Adam Malima kwa ajili ya majimbo 11 ya mkoa huo.

Kaema alisema , Mkoa wa Morogoro umepatiwa vifaa aina tisa vyenye thamani ya sh milioni 759  na kuanza kusambazwa  katika majimbo yote 11 na  kila jimbo litapokea vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 69.

 “ Kama tunavyofahamu Serikali yetu inayoongozwa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan , imenunua vifaa kwa ajili ya kupunguza vifo vya mama na mtoto vyenye thamani ya sah bilioni 14.7  na vifaa hivyo vilizinduliwa na Waziri wetu wa Afya  kwa ajili ya majimbo ya Tanzania nzima” alisema Kaema.

Kaema alivitaja  vifaa vilivyokabidhiwa kwa kila jimbo la mkoa huo  na idadi yake kwenye mabano ni Drip stand  (330), vitanda vya kawaida vya wagonjwa (330), vitanda vya kujifungulia mama wanajawazito (220) na seti (220) za kujifungulia mama wajawazito.

Alitaja vingine ni shuka (1,320), magodoro (330), Examination table (220), meza ndogo za wagonjwa kuwekea vifaa vyao pale wanapokuwa wamelazwa (165) na Bed side Locker (330).

Kaema alisema hizo zote ni juhudi za serikali katika kuondoa kabisa ama kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

“ Kwa sasa serikali imetoa kipaumbele kuimarisha  na kuwezesha hospitali zote mikoani ambazo zimeanishwa katika majimbo mbalimbali kuwa  na vifaa hivi ili kuweza kuondokana kabisa na vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua” alisema Kaema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, alisema serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya sekta ya afya na kwa sasa imejielekeza katika uboreshaji wa viwango vya utoaji wa huduma za afya nchini.

“ Malengo yetu sisi mkoa baada ya kupokea kwa vifaa tiba hivi ni kwenda kuboresha utoaji wa huduma za afya  kwa wananchi na hili tumekuwa tukilihimiza nyakati zote “ Malima.

Mkuu wa mkoa huyo alisema licha ya kupokea vifaa tiba hivyo, mkakati wa mkoa ni kuendelea kutoa elimu kuhusiana na kujikunga na magonjwa mbalimbali na namna ya utumiaji wa vifaa hivyo kwa wagonjwa.

Hivi karibuni Waziri wa Afya ,Ummy Mwalimu alizindua usambazaji wa vifaa vya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto vyenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 14.9 ambavyo vitasambazwa katika majimbo 214 na halmashauri nchi nzima.

Ummy alisema usambazaji wa vifaa vya hivyo umelenga kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto na kuimarisha uzazi salama nchini.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima (juu ya gari) akivikagua vifaa hivyo wakati wa makabidhiano hayo.
Makabidhiano yakiendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akizungumza na vyombo vya habari baada ya kupokea vifaa hivyo.
Meneja wa MSD, Kanda ya Mashariki, Betia Kaema akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo.
Wafanyakazi wa MSD wakishiriki kubeba vifaa hivyo.
Picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima (katikati) baada ya kupokea vifaa hivyo.
Vifaa vikishushwa kwenye gari la MSD tayari kwa makabidhiano.

Gari la MSD likiwa tayari kwa kushushwa vifaa tiba hivyo.

Post a Comment

0 Comments