Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Februari 24, 2024 na kuona maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali.
.............................................
Na WAF- Dar es Salaam
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya
UKIMWI imeridhishwa na hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili-Mloganzila kuanzia kwa wafanyakazi, vifaa bora na vya kisasa vya
kutolea huduma ambapo pia mazingira yanaridhisha na wagonjwa wanahudumiwa
vizuri.
Hayo yamebainishwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Dkt. Faustine Ndugulile baada
ya ziara ya kamati ya kutembelea hospitali hiyo na kukagua maboresho ya
miundombinu iliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais
Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Ndugulile amesema Serikali imefanya
uwekezaji mkubwa wa kujenga hospitali hiyo ambapo pia kuna kituo kingine cha
utafiti wa magonjwa ya moyo ambacho kimejengwa katika eneo hilo.
“Niipongeze Serikali kwa kuboresha huduma za afya
nchini kwani hivi sasa asilimia 90 ya wagonjwa ambao walikuwa wanakwenda nje ya
nchi kutibiwa wanatibiwa hapa nchini na tumeanza kupata wageni kutoka nje ya
nchi kuja kupata huduma nchini”. Ameeleza Dkt. Ndungulile.
Aidha, ameitaka Serikali kupanua wigo wa utoaji
huduma katika hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwani hospitali hiyo bado
ina eneo kubwa ambapo kuna takribani ekari 3800.
“Tunahitaji upanuzi wa huduma za magonjwa ya
moyo, upanuzi wa huduma za saratani, upanuzi wa huduma za magonjwa mengine ya
mifupa na mfumo wa ubongo ili wananchi waweze kupata huduma bora na rahisi kwa
wepesi zaidi hapa nchini”. Amesema Dkt. Ndugulile.
Vile vile ameongeza kuwa kuna fedha wameambiwa
zimepatikana, ujenzi unashindwa kuendelea kwa sababu ya masuala ya umiliki wa
ardhi hayajakamilika hivyo kamati hiyo imeitaka Serikali kupitia Wizara ya afya
na Wizara ya Elimu kukaa pamoja ili kuweza kufikia muafaka ili uwekezaji uweze
kufanyika kwa sababu wananchi wanahitaji huduma bora zaidi na eneo hilo
linatosha kwa matumizi yote ya elimu pamoja na huduma za afya.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin
Mollel amesema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye sekta ya afya hasa
kwenye miundombinu, teknolojia ya afya pamoja na kwenye wataalamu, kwani kwa
sasa kuna wataalamu wa kutosha kwenye masuala mbalimbali ya utoaji huduma za
afya hapa nchini.
Amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wamezalisha bilioni 8 kwa kufanya tiba urembo ambapo pia wameboresha maeneo mengi huduma ikiwemo mazingira mazuri ya utoaji huduma, ununuzi wa vifaa bora na vya kisasa pamoja na kuboresha chumba cha kuhifadhia maiti.
0 Comments