Na Issa Mwadanga-Songwe
WANAWAKE Mkoa wa Songwe wametakiwa kuwashirikisha
wenza wao wakati wanapochukua mikopo ya Ujasiriamali ili kuepusha matokeo hasi
yanayotokea kwa baadhi yao wanaposhindwa kulipa mikopo hiyo.
Hayo yalisemwa na Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP ) Theopista Mallya, Februari 24, 2024 alipokuwa akifungua Kongamano la Nishati Mbadala lililofanyika Vwawa Wilayani
Mbozi lililoandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali Tanzania Women Empowerment Network (TAWEN) ambayo imeingia mkataba na kampuni ya usambazaji Gesi ORXY kwa
lengo la kuunga juhudi za serikali kumtua mwanamke kuni kichwani.
Kamanda Mallya alisema “Kuna baadhi ya wanawake
huchukua mikopo hatarishi bila kumjulisha mwenza wake ambayo mnashindwa kumudu
malipo yake kitendo hicho kinapelekea kuwa na msongo wa mawazo na baadhi yao
uanza kuua watoto wao kwa kuhisi
watapata shida kisha anajiua na yeye, hiyo ni mbaya wanawake wenzangu
mnatakiwa kuchukua mikopo yenye tija ambayo mnaweza kumudu kuilipa ikiwa ni
pamoja na kumshirikisha mwenza wako” alisema Kamanda Mallya.
Sambamba na hayo amewaasa wanawake wa mkoa
huo kutumia nishati mbadala ili kuepuka
athari zitokanazo na matumizi ya nishati ya kuni.
Naye Mratibu wa Kongamano hilo kutoka TAWEN Dar
Es Salaam Levina Mlokozi akizungumza katika kongamano hilo ambaye ni mwakilishi
wa Mkurugezi wa TAWEN alisema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuhakikisha mama
anatuliwa kuni kichwani ili kusababisha mazingira yanatunzwa na kuwa salama.
“Tumeandaa kongamano hili kuunga juhudi za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuwafanya
wanawake wa Mkoa wa Songwe watumie nishati safi ambayo ni salama kwa afya yao”
alisema Mratibu Mlokozi.
Kongamano hilo lililobeba kauli mbiu isemayo "Kumtua mama Kuni Kichwani" ambapo jumla ya mitungi ya gesi 100 ilitolewa kwa wanawake Mkoani hapa kwa lengo la kuendelea kuiweka Tanzania ya kijani.
0 Comments