...............................................
Na Moses Mabula -Tabora
WAKULIMA wa zao la tumbaku Wilayani Kaliua Mkoani
Tabora wamemwomba Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kuwachukulia hatua kali
ikiwemo kuyafutia usajili makampuni yanayosambaza mbolea iliyochakachuliwa kwa
wakulima.
Wametoa ombi hilo jana walipokuwa wakiongea na
Waandishi wa habari waliotembelea vijiji vya Usindi na Usimba katika kata za
Ushokola na Usimba Wilayani humo ili kujionea maendeleo ya kilimo cha zao hilo
kabla ya masoko.
Baadhi yao wamekiri kupata mafanikio makubwa
katika kipindi cha msimu uliopita wa 2022/2023 kutokana na juhudi kubwa za
serikali ya awamu ya 6 zilizowezesha mbolea kupatikana kwa wakati na wanunuzi
kununua kwa bei nzuri.
Joseph Ntahondi mkulima, mkazi wa Kijiji cha
Usimba na Mwenyekiti wa Chama Cha Msingi Usimba amemshukuru Rais Dkt Samia
Suluhu Hassan na wasaidizi wake kwa kusimamia vizuri sekta ya kilimo, sasa
manufaa yanaonekana.
Amebainisha kuwa msimu uliopita walivuna kilo
laki 9 za zao hilo na kuuza kati ya dola za kimarekani 2.4 hadi 3 kwa kilo na
matarajio yao kwa mwaka huu ilikuwa kuvuna kilo milioni 1au zaidi lakini wana
wasiwasi kama watafikia kiwango hicho.
Ameafanua kuwa msimu huu baadhi ya wakulima
tumbaku yao haikustawi vizuri, mbolea waliyotumia haikuwa na ubora hivyo
kudumaza zao hilo, tofauti na iliyotumiwa na wenzao katika maeneo mengine.
‘Baadhi ya makampuni yanatuletea mbolea
iliyochakachuliwa, ambayo ni feki, hawa hawatutakii mema, tunaomba Waziri Bashe
awachukulie hatua stahiki na ikiwezekana wafutiwe usajili au leseni ya kuuza
mbolea za pembejeo’, ameeleza.
Peter Daniel mkulima, mkazi wa Kata ya Usimba
amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya 6 kupitia Waziri
mwenye dhamana za kuinua wakulima, ila akasikitishwa na baadhi ya makampuni
kufanya mchezo mchafu wa kuwauzia mbolea feki.
‘Mwaka jana tulipata mbolea za pembejeo kwa
wakati na kwa bei nzuri na tukapata kilo za kutosha, ila haya makampuni
yanataka kuturudisha nyuma kimaendeleo, tunamwomba Waziri au Mama yetu awapige
marufuku kuuza mbolea’, amesema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Usindi, Haji
Masudi amekiri kuwa zao la tumbaku limeleta neema kubwa kwa wananchi kwani kila
aliyelima mwaka jana amejenga nyumba nzuri na wengine wamenunua pikipiki na
magari.
Ameshukuru
serikali kwa kukomesha vitendo vya ubadhirifu vilivyokuwa vikifanywa na baadhi
ya viongozi wa Amcos na kuongeza kuwa kila mkulima sasa anapata stahiki zake
kulingana na kilo alizozalisha ila akasikitishwa na baadhi ya makampuni
yanayochakachua mbolea.
Meneja wa Chama Cha Msingi Usindi, Mohamed
Abdallah amesema kuwa serikali imetoa mwongozo wa usimamizi thabiti wa vyama
vya msingi hivyo hakuna Kiongozi yeyote anayeweza kudhulumu mkulima, akithubutu
cha moto atakiona.
Mwakilishi wa Meneja Mkuu wa Chama Cha Ushirika
Milambo, Lucas Kalonga amempongeza Rais Samia kwa kutafuta makampuni mengi ya
kununua zao hilo, thamani ya tumbaku sasa imerudi, inauzwa kati ya sh 4800 hadi
6000 kwa kilo.
Amebainisha kuwa uzalishaji wa zao hilo katika
Wilaya za Urambo na Kaliua umeongezeka mara dufu kwani mwaka juzi jumla ya kilo
mil 17 zilizalishwa, mwaka jana kilo mil 32 na mwaka huu wanatarajia kuvuna
zaidi ya kilo mil 60.
Amesisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na serikali katika kusimamia zao hilo ili wakulima waendelee kunufaika zaidi, aliomba Waziri mwenye dhamana ya kilimo kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuuza mbolea feki.
0 Comments