........................................................
Na Dotto Mwaibale, Mbeya
BOHARI ya Dawa (MSD) imewatambua na kuwapongeza wadau wake wa
Kanda ya Mbeya kwa ushirikiano na umahiri wao kwenye suala zima la kuboresha
upatikanaji wa bidhaa za afya kwenye maeneo yao.
Akizungumza Februri 9, 2024 katika mkutano huo wa wadau na MSD,
Meneja wa MSD Kanda ya Mbeya, Marco Masala alisema mkutano kazi huo umelenga
kuweka mkakati wa pamoja wa kudumu na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya
katika mikoa hiyo unaboreshwa na unaimarika.
Akisistiza katika mkutano huo ulioambatana na
tukio hilo la utoaji vyeti kwa wateja wote na utambuzi wa wadau waliofanya
vizuri kwenye maeneo kadhaa kwa kuwapatia tuzo maalumu kutoka mikoa ya Mbeya,
Rukwa, Songwe na Halmashauri ya makete iliyopo mkoani Njombe, Masala alisema
lengo la mkutano huo ni kuweka mikakati ya pamoja ya kutekeleza majukumu yao na
kutatua changamoto zinapojitokeza kwa pamoja.
Akizungumzia tukio la kuwatambua na kuwapongeza
wadau hao mahiri alisema hatua hiyo ilifikiwa kutokana namna wanavyotoa ushirikiano dhabiti katika
kufanikisha kazi mbalimbali na MSD.
"Wadau hawa tunaowatambua leo ni pamoja na
vituo ambavyo havina madeni ndani ya MSD,
vinatumia vyanzo vyao vingine kununua bidhaa za afya kutoka MSD, lakini
zaidi wanatimiza wajibu ipasanyo wa kuwezesha usambazaji wa vifaa tiba kwa
wakati," alisema Masala.
Aidha Meneja huyo aliongeza kwamba kwa sasa MSD
inaendelea kujipambanua kwa ufanisi wa utoaji wa huduma zake kwa kuzingatia
mahitaji halisi kuzunguka kanda yote ya Mbeya hivyo kupunguza malalamiko ya
wananchi kuhusu kupata vifaa tiba na dawa.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera
aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa aliwaomba wadau kutambua
kuwa jukumu kubwa walilo nalo ni kuvisimamia vituo vya kutolea huduma za afya katika
maeneo yao ili viweze kukusanya mapato ya kutosha yanayotokana na uchangiaji wa
huduma za afya ili viweze kununua bidhaa za afya, sambamba na kusimamia
mnyororo wa ugavi wa bidhaa hizo.
“Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kuongeza fedha inayotengwa kwa ajili ya
bajeti ya kununulia bidhaa za afya ili kuboresha utoaji wa huduma za afya.
Hivyo, kila mmoja ana jukumu la kusimamia matumizi sahihi ya bidhaa za afya ili
kuleta tija kwa wananchi,” alisema Malisa.
Aidha, Malisa aliwataka wadau hao kuhakikisha
wananchi watapata huduma bora zaidi katika vituo vya kutolea huduma za Afya
bila manung’uniko na kupitia mkutano huo aliwakumbusha wadau wa MSD kupitia
Wizara ya Afya, kufanya maoteo ya bidhaa za afya kwa usahihi na kwa wakati.
Alisema kwa kufanya hivyo itaiwezesha MSD kuwa na
takwimu sahihi katika kuagiza kutoka kwa wazalishaji na washitiri hivyo
kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya.
Malisa aliwakumbusha wadau hao kusimamia matumizi
sahihi ya takwimu za mnyororo wa ugavi ili ziwasaidie kufanya maamuzi sahihi
juu ya bidhaa za afya katika maeneo yao.
Meneja Huduma kwa Wateja wa MSD, Dkt. Pamella
Sawa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai alisema
lengo lingine la kikao kazi hicho ni kupeana maelekezo au kutatua changamoto
zilizopo baina ya wadau wao na MSD na kuelimishana namna bora ya kufanya kazi
kwa kushirikiana na pale watakapo zibaini watafute njia bora ya kuboresha.
Alisema kikao hicho kinahusisha wadau wa mikoa ya
Mbeya, Rukwa, Songwe na Halmashauri ya Makete wanaohudumiwa na MSD wakiwemo
viongozi mbalimbali wa sekta ya afya na Serikali.
“Sasa hivi kuna mabadiliko na maboresho makubwa
yanayoendelea kufanyika ndani ya MSD na ninyi wateja wetu ni mashahidi hasa
katika majukumu yetu kwenye eneo la usambazaji kutoka mara nne hadi mara sita ya
mzunguko na upatikanaji wa bidhaa za afya unakuja kwa wakati,” alisema Dkt.
Sawa.
Kwa upande wake Dkt. Enock Mwambalaswa ambaye ni
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma ambayo imepata cheti cha pongezi
na tuzo tatu ambazo Halmashauri hiyo imepata ikiwa ni Halsmashauri pekee
iliyopata tuzo zote tatu.
Alisema kuwa pia Halmashauri hiyo imeibuka
kidedea kwa kupata tuzo kwa kutumia vyanzo vingine vya mapato tofauti na vyanzo
vinavyotolewa na Serikali kama ruzuku kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa
tiba.
Dkt. Mwambalaswa alitumia nafasi hiyo kuipongeza
Serikali kwa kutoa kipaumbele kwenye mgawanyo wa mapato ambao unaelekeza
halmashauri kutoa msukumo kwa kutenga kila asilimia 50 ya mapato yake na kuyapeleka
kwenye huduma za afya.
Halmashauri tatu zilizoibuka kidedea kwa kutumia
vyanzo vingine vya fedha mbali ya zile zinazo tolewa na Serikali kwa ajili ya
kununua bidhaa za afya ni Mbeya mji,
halmashauri ya Mji wa Tunduma na
Halmashauri Mbeya.
Halmashauri tatu za kwanza ambazo vituo vyake vya afya havina madeni au madeni yake kidogo ni Ileje, halmashauri ya mji Tunduma na Busokelo na zote hizi zimetunukiwa tuzo za umahiri.Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje , Joyce Wilson akipokea cheti.cha umahiri.Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa akizungumza kwenye mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera.Meneja Huduma kwa Wateja wa MSD, Dkt. Pamella Sawa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai Meneja wa MSD Kanda ya Mbeya Marco Masala, akizungumza kwenye mkutano huo.
0 Comments