.........................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya
Singida inapopima viwanja vya makazi ya watu kuwasiliana na Wakala wa Barabara
Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) ili kuondoa migogoro inayoweza kutokea baina ya Serikali na wananchi kwa kubomolewa nyumba zao ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Serukamba alitoa ombi hilo Februari 22, 2024 wakati akikagua ujenzi wa
miundombinu ya barabara ya Mungumaji na Mnung’una mradi unaotekelezwa na
Manispaa hiyo na TARURA kwa kiwango cha lami nyepesi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba.
........................
“Mkipima viwanja vyenu kwa kuwashirikisha TARURA itasaidia kupunguza
migogoro ya kubomolewa nyumba za wananchi pale itakapo takiwa kujengwa
miundombinu ya barabara,” alisema Serukamba.
Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu
.........................
Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu alisema manispaa hiyo ili
kufungua mtandao wa barabara kwa mwaka huu wa fedha wa 2024/ 2025 imetenga
jumla ya Sh.Milioni 85 kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kazi
hiyo.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Ibrahimu Kibasa.
...............................
Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Ibrahimu Kibasa akizungumzia
ujenzi wa mradi wa barabara ya Mungumaji ambayo inajengwa kwa kiwangocha lami nyepesi
na ile ya Mnung’una / Imbelee ambayo nayo inajengwa kwa kiwango cha lami alisema
zitakuwa ni mkombozi kwa wananchi kwani zitawarahisishia kusafiri kwa haraka na
kuzitumia kwa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Aidha, Kibasa alisema TARURA imekusudia kujenga barabara hiyo yenye urefu
wa meta 700 inayounganisha barabara ya lami ya Mwenge inayoelekea Stendi Kuu ya
Mabasi ya Isuna na barabara ya lami ya Singida eneo la Majengo.
Alisema barabara ya Mungumaji ni moja ya barabara muhimu katika Manispaa ya Singida na inaunganisha kata tatu ambazo ni Majengo, Misuna na Mungumaji yenye urefu wa kilometa 8.56.
Akizungumzia barabara ya Mnung’una /Imbelee alisema pia ni moja ya barabara
muhimu katika Kata ya Minga na ni barabara kuu ya kuingia katika Mtaa wa
Mnung’una yenye urefu wa kilometa 1.45 na kuwa TARURA imekusudia kuijenga
barabara hiyo kwa urefu wa mita 460.
Alisema TARURA katika Wilaya ya Sigida una mtandao wa barabara wenye jumla
ya kilometa 1,335.789 ambazo zimesajiliwa kwenye mfumo wa mtandao wa barabara
ambao unajumuisha barabara Mkusanyo zenye urefu wa kilometa 656.403 na barabara
Mlisho zenye urefu wa kilometa 648, 283 na barabara za Jamii zenye urefu wa
kilometa 31,103.
Barabara nyingine iliyokaguliwa ni ile ya Kinyeto-Darajani-Sagara, Njiapanda Merya-Merya ambayo itatumia fedha kiasi cha zaidi ya Sh. Milioni 284.
0 Comments