Na Dotto Mwaibale, Singida
WAKALA wa Barabara Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Mkoa wa Singida
wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya
ujenzi wa miundombinu ya barabara ukiwemo ujenzi wa daraja la Kata ya Minyughe
ambao ujenzi wake utagharimu jumla ya Sh.Bilioni 2.
Daraja hilo mara baada ya kukamilika linakwenda kuwanufaisha wananchi zaidi
ya 20,000 wa kata za Minyughe na Makilawa wilayani Ikungi ambao kwa muda mrefu sasa wamekosa mawasiliano ya
uhakika kutokana na kukatika kwa daraja hilo.
Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Mkoa wa
Singida, Mhandisi Ibrahimu Kibasa alisema kuna kila sababu ya kumshukuru Rais
Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ambalo ni
muhimu sana kwa wananchi wa kata hizo.
“Ebu tuangalie gharama za ujenzi wa
daraja hili ni zaidi ya Sh.bilioni 2
ambalo litahudumia kata mbili tu pesa kama hizi tulizoea kuona zinatumika
kujenga madaraja ya kuunganisha wilaya moja hadi nyingine au mkoa kwa mkoa
lakini rais wetu Samia Suluhu Hassan ili kuharakisha maendeleo ya nchi kila
kona ameona atoa fedha hizo tunamshukru,” alisema.
Mhandisi Kibasa akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba kuhusu
ujenzi wa daraja hilo kuwa daraja hilo alisema ujenzi wake umefikia asilimia 60
na linatakiwa kukamilika Mei 18, 2024.
Alisema hadi sasa kazi zilizofanyika ni kutengeneza njia ya
mchepuko,kupanga mawe na kusuka nondo,kumwaga zege la chini na la juu na
ulindaji wa daraja kwa kutumia mawe ambapo mkandarasi wa kampuni ya JP Traders
Ltd aliyepewa kazi ya kulijenga kwa gharama ya Sh.Milioni 556.140, ameshalipwa
Sh.milioni 224.770 sawa na asilimia 40.4 ya thamani ya mkataba wote.
Kibasa akitoa mchanganuo alisema gharama za kununua vyuma vitakavyowekwa
juu ya daraja hilo vinagharimu Sh.Milioni 939 hivyo jumla ya mradi ni
Sh.bilioni 1.4 ambao zikijumlishwa gharama za kodi bandarini na usafirishaji
kutoka Dar es Salaam hadi kufika Singida gharama zote za mradi zitafikia jumla
ya Sh.bilioni 2 au pungufu kidogo.
Kibasa alisema daraja hilo litakapokamilika zitajengwa barabara za kiwango cha changarawe kutoka Mtamaa-Minyughe hadi Mtavira ambapo katika
mwaka wa fedha wa 2024/2025 unaoanza Julai mwaka huu zimetengwa Sh.milioni 360.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Serukamba akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa
daraja hilo alisema daraja hilo litakuwa halina umuhimu wa kujengwa kama
wananchi watakuwa wakifanya kilimo kisicho na tija cha kulima ekari moja na kupata magunia
matatu.
Alisema tija ya daraja hilo itapatikana kwa wananchi kulima kilimo cha kuzingatia
mbolea kama wanavyo elekeza wataalamu ambapo kwa ekari moja kutoa mahindi
kuanzia magunia 30 hadi 35.
Serukamba aliiagiza TARURA kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi
mkubwa na kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika nayo.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Minyughe, Nelson Kiwesi, aliishukru
serikali kwa hatua iliyoichukua ya kujenga daraja hilo ambalo ni muhimu sana
kwa uchumi wa wananchi wa kata hizo na kwamba kukamilika kwa ujenzi wake
itakuwa ni mkombozi mkubwa kwao.
Miradi mingine iliyotembelewa Februari 27, 2024 na kukaguliwa Mkuu wa Mkoa
wa Singida Peter Serukamba katika Wilaya ya Manyoni na Itigi ni wa barabara ya
Iseke, Kipanduka ya kilometa tatu ambayo ipo wilayani Manyoni na inaunganisha
kata tisa za Mkwese, Solya, Makuru, Chikuyu, Isajila, Sasilo, Iseke na Kintinku
inayojengwa na Mkandarasi JP Traders kwa thamani ya Sh.Milioni 900.8.
Barabara nyingine iliyokaguliwa ni ya Hospitali inayejengwa kwa lami
nyepesi yenye urefu wa mita 450, Kipondoda, Tambukareli mita 3.10 mradi ambao
unaunganisha Kata ya Manyoni mjini, Mhalala na Mkwese.
Mradi mwingine uliokaguliwa ni wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi ambao ni barabara ya kiwango cha lami kutoka Msikitini wenye thamani ya Sh.Milioni 474.72.
0 Comments