.........................................
Na Dotto Mwaibale, Singidani Blog, Arusha
WAKAZI wa Mkoa wa Arusha wameeleza hisia zao
chanya kuhusu ujio wa mkuu mpya wa mkoa huo, Paul Makonda, wakisema huenda kero
ndogo ndogo zilizokuwa zikizembewa kutolewa uamuzi zitashughulikiwa.
Makonda, ambaye Jumapili, Machi 30, 2024
aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha akichukua
nafasi ya John Mongella ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara)
iliyoachwa wazi na Anamringi Macha aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Wakazi hao wa Arusha wanasema, utendaji wa
Makonda alipokuwa Katibu wa NEC ya CCM Itikadi, Uenezi na Mafunzo, haukuwa na
mawaa na ndiyo maana mara kadhaa Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia alikuwa
akimtolea mfano kila alipowahimiza watendaji wengine wa serikali wawajibike
katika maeneo yao.
Katika kipindi chake cha takriban miezi mitano
akiwa Mwenezi wa CCM, Makonda aliweza kuibua madudu mengi kuanzia ngazi za
wilaya hadi mkoa kutokana na kero nyingi za wananchi kutopatiwa ufumbuzi licha
ya maeneo hayo kuwa na watendaji ambao ni wateule wa Rais wanaohitaji kumsaidia
kutatua kero hizo za wananchi.
Motika Paul ole Saitabau, mkazi wa Kisongo,
anasema Makonda alijitahidi kurejesha Imani ya wananchi kwa Serikali ya CCM
kutokana na staili yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuwahoji watendaji wa
maeneo husika na kuagiza utekelezaji na utatuzi wa kero hizo.
“Wananchi wengi tuna kero, lakini ukienda kwa
ofisa mtendaji wa Kijiji au Kata hupati ufumbuzi, ukienda halmashauri nako
hakuna utatuzi kwa sababu baadhi ya madiwani ambao mara nyingi ndio wanaohusika
na kero hizo wanawatisha wakurugenzi wa halmashauri kwenye mabaraza yao na
wakurugenzi nao kwa hofu ya kuharibiwa kibarua wanaamua kukaa kimya huku
wananchi wakiumia,” anasema Motika.
Kwa upande wake, Bi. Nashpai Mollel, mkazi wa
Majengo, anasema, Makonda ni kiongozi ambaye anapenda kuona utekelezaji na siyo
blaa blaa, hivyo wanaamini hata maendeleo mkoani humo yanaweza kushika kasi
maradufu.
Nashpai anasema, utendaji wa Makonda ndio
ulioibua kero nyingi katika jamii ambazo hazikuwa zikifahamika, hatua iliyomfanya
Rais Samia kutangaza kwamba sasa atakuwa akikutana na wananchi mmoja mmoja
kusikiliza kero zao.
“Hata alipotangaza uamuzi huo alipigia mfano utendaji wa Makonda kwenye mikutano yake, yote hiyo ilikuwa kuwakumbusha wateule wake kwamba wanao wajibu wa kuwatumikia wananchi, sasa kwa sababu amekuwa mkuu wa mkoa, tunaamini kero zilizokuwa zikiwatesa wananchi zitapatiwa ufumbuzi na watendaji wa chini wataacha uzembe,” alisema Nashpai.
0 Comments