............................
Na Dotto Mwaibale, Singida
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania
(TAKUKURU) Mkoa wa Singida imewataka Wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani hapa
kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na rushwa kwani vinawaharibu vijana
ambao ndio hazina ya nchi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa
Singida Bi Sipha Mwanjala wakati akizungumza na wanafunzi hao katika kongamano
lililoandaliwa na Taasisi hiyo mkoani hapa lililohusu rushwa na dawa za
kulevya.
Alisema lengo la kongamano hilo kwa kundi hilo la
vijana ni kuwaongeza uelewa wa mapambano dhidi ya rushwa na dawa za kulevya
kwani ndilo wapo katika hatari zaidi ya kuathiriwa na vitendo hivyo.
“Mafunzo haya yatasaidia mapambano dhidi ya rushwa
kwa wanafunzi hawa kutoka vyuo vikuu vilivyopo mkoani kwetu hapa ambavyo ni
Chuo cha Maji, Afya, Utumishi na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya
Singida na kuleta matokeo chanya,” alisema Bi. Mwanjala.
Alisema Takukuru imeamua kuwashirikisha vijana
katika kongamano hilo kwa sababu inatambua vijana kuwa ni mtaji usiofilisika na
ni hazina ya taifa kwa maana kwamba vijana wakipata elimu ya masuala ya rushwa
watasaidia katika kuzuia na kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa TAKUKURU pia
kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ambao hawakupata fursa ya kupata elimu hiyo.
Bi. Mwanjala alisema kuwa vijana ni kizazi na wazazi
wa kesho hivyo wakijua umuhimu wa maadili na kuepukana na vitendo vya rushwa
TAKUKURU inaamini kwamba watawafundisha watoto wao kufuata sheria na kanuni na
taratibu na kuepukana na masuala ya rushwa wakiamini kwamba rushwa na maadili
ni sawa na pande mbili za shilingi.
Alisema kunapokuwa na rushwa hakuna maadili na
kukiwa na maadili hakuna rushwa na kueleza kuwa hivi sasa vijana wapo chuoni na
kesho kutwa wao ndio watakuwa maofisini hivyo wakielimishwa na kutambua maadili
watafanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu na watatenda haki na wananchi
watapata huduma stahiki hivyo vitendo vya rushwa vitapungua kama sio kumalizika
kabisa.
Mratibu wa TAKUKURU na SKAUTI (TAKUSKA) Mkoa wa
Singida Bi. Fatma Nkumbi alisema wao kama wadau wa Takuska ni muhimu kuwapa elimu
vijana kwa sababu kundi hilo ni taifa la leo na kesho na kuwa taifa ambalo
vijana wake wanatumia dawa za kulevya nguvu kazi itapungua na uchumi wa taifa
utadorora.
Alisema kutokana na kuwepo kwa vitendo vya rushwa
na matumizi ya dawa za kulevya kundi hilo likipata elimu linaweza kutokomeza
mambo hayo kutokana na uwezo mkubwa walionao vijana.
“ Sisi kama wadau wa TAKUSKA tumepanga mikakati
pamoja na TAKUKURU kupita kila maeneo ya vijijini pamoja na mijini, mashuleni
na maeneo yenye mikusanyikao ya watu kuwapa elimu wakiwemo vijana na warika la
kati, wanafunzi wa shule za msingi na vyuo na wale ambao wanaendesha maisha yao
sehemu mbalimbali,” alisema Bi. Nkumbi.
Kwa upande wake, Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani aliwataka vijana kuwa wazalendo na kuacha kuwa na tamaa ya kuwa na maisha mazuri na kueleza kwamba tamaa hizo ndio kichocheo kikubwa cha wao kujiingiza katika vitendo vya rushwa na dawa za kulevya.
Latifa Hussein Mwanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake aliishukuru TAKUKURU kwa kuwapa elimu hiyo ambayo imewaongezea uelewa wa mambo mengi ya mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na dawa za kulevya.Mtumishi wa Takukuru Mkoa wa Singida, Dorothea Kinyonto akizungumzia madhara ya vitendo vya rushwa.Mtumishi wa Takukuru Mkoa wa Singida, Joseph John, akizungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Mkoa wa Singida.
0 Comments