CHADEMA YAWATAKA WANANCHI SINGIDA KUPAZA SAUTI DHIDI YA SERIKALI KUKITHIRI VITENDO VYA UTEKAJI WATU
................................
Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)
WANANCHI Mkoa wa Singida wametakiwa kupaza sauti kwa Serikali ili kukomesha
kukithiri kwa vitendo vya utekaji wa watu vilivyoshamiri mkoani hapa.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lisu wakati akiwahutubia mwishoni mwa
wiki wananchi wa Mkoa wa Singida kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika Stendi ya Mabasi ya Zamani ulioandaliwa na chama
hicho baada ya kufanyika kwa maandamano ya amani yaliyopita katika maeneo
kadhaa ya mji wa Singida.
Lisu alitoa ombi kwa wananchi hao huku akiinyoshea kidole Serikali kwa kuwa kimya dhidi ya
vitendo vya utekaji na upoteaji wa watu wakiwemo wafanyabiashara wawili wa Mkoa
wa Singida ambao alidai walipotea
mwishoni mwa mwaka jana na kuwa walichukuliwa na maafisa wa Jeshi la Misitu
(TFS)
"Hawa wasiojulikana hatuwajui majina lakini tunajua ni kinani na
tunajua wanatokea wapi, ni wao na askari polisi wao na usalama wa taifa
wao"
Lisu alisema chama hicho kinafanya maandamano nchi nzima baada ya Serikali
kuwa kimya kufuatia kupanda kwa gharama za maisha, kutaka katiba mpya,
kukithiri kwa tozo na kuwekwa kwa kikotoo.
Alisema wanafanya maandamano baada ya kuona ardhi ya watanzania ikiuzwa kwa
watu wanaoitwa wawekezaji kutoka nje ya nchi, kukithiri kwa kuuza rasilimali za
nchi kama bandari na ubadhirifu mkubwa unaofanyika akitolea mfano kuwa kila
mwaka ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imekuwa
ikibaini kupotea kwa zaidi ya Sh.Trilioni 2,
lakini hakuna hatua yoyote inayochukuliwa dhidi ya wahusika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida, Jackson Jingu aalisema katika muendelezo wa
wimbi hilo la utekwaji na ushambuliaji wa watu wiki iliyopita chama hicho kimempoteza mwanachama
wao Peter Mtinangi ambaye aliuawa na watu wanaoitwa wasiojulikana na
kumuhusisha mmoja wa wanasiasa katika wilaya hiyo ya Ikungi.
"Hakuna watu wasiojulikana, tulimsikia Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa
Bukoba akisema watu wanaomtukuna Rais watawapoteza na polisi
wasiwatafute," alisema Jingu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Sera Chadema Kanda ya Kati, David Djombe alisema wanaandama kuishinikiza
Serikali kubadili mfumo na kuacha kuleta wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi
wa halmashauri kwa kuteuliwa badala yake wanataka viongozi wanaowataka wenyewe.
"Nchi hii ina mambo ya ajabu sana, mkuu wa mkoa analetwa, mkuu wa
wilaya analetwa, mkurugenzi, tunaandamana kudai katiba mpya ambayo itatuletea
wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi tunaowataka sisi" alisema
Kwa upande wake Wakili Msomi wa kujitegemea kutoka Mkoa wa Mbeya, Boniface
Mwambukusi alisema watu wanapotea nchini lakini mtu akihoji juu ya hilo
anaambiwa anashusha hadhi ya jeshi la polisi.
Mwabukusi alisema kuwa Mkoa wa Singida unaweza kuendelea bila ya kuwepo kwa
wakuu wa wilaya mkoa kutokana na waliopo majukumu yao kutoeleweka.
"Tunataka katiba mpya ambayo italinda maslahi ya kila mwananchi, sio
watu wanapotea ukihoji unaambiwa unashusha hadhi ya jeshi la polisi, hawa
askari wakijengewa mazingira bora ya maisha yao hizi kesi za kusingizia
zitatoka wapi?, " alihoji Mwabumkusi huku akishangiliwa.
Katika mkutano huo baadhi ya wananchi akiwemo Juma Mwiru ni miongoni mwa
waliojitokeza kutoa kero zao na kueleza kutekwa kwa ndugu zake wawili walitekwa
tangu Desemba 28, 2023 na mpaka leo hawajapatikana wala hawana taarifa yoyote
ya mahali walipo na kama wapo hai au wamekufa na kuwa wamekuwa changamoto kubwa
wanapozitembelea familia za ndugu zake hao kutokana na watoto kuishi maisha
magumu na kuuliza maswali kila wakati wakiuliza walipo baba zao na siku
watakayorudi.
"Tunaomba msaada jamani, familia inateseka mno, ndugu zangu wamepotea
tokea mwezi wa 12 mpaka sasa hakuna taarifa yoyote kuhusu walipo" alisema.
Wananchi walioudhuria maandamano na mkutano huo walijitokeza kwa wingi huku
wakiwa na mabango yaliobeba jumbe mbalimbali huku asilimia kubwa yakidai katiba
mpya pamoja na kupungua kwa gharama za maisha.
Maandamano ya namna hiyo ni ya kwanza kufanyika katika Mkoa wa Singida na nimuendelezo wa maandamano mengine kwani tayari yamekwisha fanyika kwenye mikoa mingine ikiwa ni ajenda ya chama hicho ya kudai mambo ya msingi ya wananchi wa Tanzania.
No comments