Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro (katikati) akiongoza dua maalumu ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan, Hayati Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Taifa iliyofanyika Aprili 7, 2024 katika viwanja vya Ikulu ndogo mkoani Singida.
.....................................
Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)
WAZIRI wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kwamba Rais Samia Suluhu
Hassan amewavusha Watanzania katika kipindi kigumu hivyo tuendelee kumuombea.
Mwigulu aliyasema hayo wakati akitoa salamu za Rais katika futari iliyo
andaliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa waislamu na wananchi wa Mkoa wa
Singida ambayo ilikwenda sanjari na dua ya kumuombea Rais, Hayati Rais Mstaafu
Ali Hassan Mwinyi na Taifa iliyoongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa
Nassoro akishirikiana na viongozi wengine
wa kiislamu kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Taifa.
"Mazingira ambayo Rais wetu aliachiwa nchi baada ya Rais wa Tano
Hayati John Pombe Magufuli kufariki yalikuwa magumu huku dunia ikipita katika
mtikisiko wa kiuchumi na hayakuzoeleka katika nchi yetu kwani baada ya kifo hicho
hakuna alichokabidhiwa na miradi mingi ilikuwa chini ya asilimia 35 lakini
alisimama kidete na miradi hiyo imeendelea bila kukwama hadi kufikia asilimia zaidi ya 95 huku
mingine ikiwa imekwisha kamilika," alisema Mwigulu.
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu Rais Samia ameweza kutoa fedha
nyingi ambazo hazina mfano katika sekta za afya, ujenzi, elimu, umeme, kilimo
na mingine mingi kiwango cha fedha ambacho akijawahi kutolewa katika awamu zote
za marais waliotangulia.
Sheikh Swed Twaribu ambaye ni Mratibu wa Ofisi ya Mufti Kanda ya Kati
alisema mtu ambaye ameshindwa kusikia juu ya mambo makubwa aliyofanya Rais
Samia katika kutekeleza miradi hiyo
mbalimbali basi anaweza kuiona kwa macho zikiwemo barabara, miradi ya
maji, umeme, Reli ya Kisasa ya SGR na mingine mingi ambayo inajieleza yenyewe mbele
za wananchi.
Alisema katika kipindi chake hicho cha uongozi demokrasia imekuwa kubwa
hapa nchini kwani ameruhusu shughuli za kisiasa kufanyika kwa uhuru mkubwa
jambo ambalo limeleta utulivu wa nchi ikiwemo watu kuabudu pasipo kubughudhiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego akitoa salamu za mkoa na mafanikio
lukuki yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha
uongozi kwa miaka mitatu alisema ni mengi mno yamefanyika.
Dendego alitaja kwa ujumla wa mambo yaliyofanyika katika kipindi hicho kuwa
ni ukusanyaji wa mapato, kuwawezesha wananchi kuchumi na kutoa mikopo ya
asilimia 10 ambayo inatolewa katika Halmashauri, mpango wa kuhudumia kaya
maskini TASAF, Maendeleo ya kilimo na mifugo.
Alitaja maeneo mengine yaliyopata mafanikio kuwa ni upimaji wa ardhi,
misitu, maliasili na mazingira, viwanda na biashara, uvuvi, madini, maendeleo
ya elimu, huduma za afya, maji, ujenzi, mawasiliano na uchukuzi na barabara
(TANROADS na TARURA)
Dendego alitaja mafanikio mengine yaliyopatikana ni kwenye Shirika la
Nyumba na Makazi, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Nishati ya Umeme, Michezo
na Utamaduni, Mapambano dhidi ya Rushwa na Dawa za kulevya, Mapambano ya
Ukimwi, Malaria na ziara za viongozi.
Kwa niaba ya Wananchi Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego alimshukuru
Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake anayoingoza kwa kazi kubwa ya maendeleo aliyoifanya
mkoani hapa katika kipindi cha miaka mitatu chini ya uongozi wake ambapo mkoa ulipokea Sh.Trioni 1.7 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya shughuli za uendeshaji pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Katika futari hiyo Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego amemwagiwa pongezi
nyingi na wadau mbalimbali ambao wameeleza kuwa licha ya kuwepo mkoani hapa kwa
muda mfupi tangu ahamishiwe akitoka Mkoa wa Iringa amekuwa na ushirikiano
na makundi mbalimbali na kufanikisha kuandaa futari hiyo kwa niaba ya Rais
Samia.
Hafla ya Futari hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini ya kiislamu na kikristo, viongozi wa kisiasa, Serikali, Wafanyabiashara, watumishi wa umma na sekta binafsi, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya zote, wabunge na Waumini wa dini zote na wananchi.Waziri Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba akitoa salamu za Rais wakati wa futari hiyo.
0 Comments