Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, akizungumza na vijana ambao walilazimika kuandamana hadi ofisini kwake kudai malipo ya fedha zao walizocheleweshewa kupewa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Singida baada ya kufanya kazi ya kuchimba mtaro wakati wa utekelezaji wa mradi wa maji uliopo Kijiji cha Mwiganji.
...........................
Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)
MKUU wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe
amefanikiwa kumaliza mgogoro kwa masaa mawili, uliokuwepo baina ya vibarua
waliokuwa wakifanya kazi ya kuchimba mitaro kwenye mradi wa maji katika Kijiji
cha Mwiganji dhidi ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)
Wilaya ya Singida baada ya kuwacheleweshea kuwalipa fedha zao ambazo walipaswa
kulipwa tangu mwezi Februari, 2024.
Licha ya kuwa ni siku ya mapumziko DC Gondwe
alilazimika kwenda ofisini kuwasikiliza vibarua hao na kumaliza mgogoro huo ambao
ulikuwa na mvutano mkali baada ya kuwaita wahusika wote waliokuwa wakitekeleza
mradi huo kuanzia Mkandarasi, RUWASA na vibarua hao ambao walikuwa wameandamana
wakiwa na mabegi yao hadi ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo kupeleka malalamiko yao
baada ya kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa takribani 35.
"Ninyi ni vijana wazalendo mmeamua kuja kwa
Rais Samia Suluhu Hassan kuleta malalamiko yenu kupitia mimi mwakilishi wake
nawashukuru sana kwani mngeweza hata kuuhujumu mradi huo kwa hasira za kukosa
malipo yenu. Nimesikiliza maelezo ya pande zote ninyi RUWASA ninachowaomba kama
hela yao ipo muwalipe leo hii Aprili 6, 2024 na malipo hayo mkayafanye kijijini
ulipotekelezwa mradi huo ili hata wale Mama Lishe na watu wengine wanaowadai
vibarua hawa baada ya kupatiwa mahitaji mbalimbali nao waweze kupata fedha zao,"
alisema Gondwe.
Gondwe aliwataka RUWASA wanapoanza kutekeleza
mradi wowote baada ya kupatikana mkandarasi kuhakikisha unakuwepo mkataba wa
kazi baina ya wahusika na vibarua badala ya kufanya kazi kiholela bila ya
kuwepo kwa mkataba jambo ambalo litasaidia kuondoa migogoro isiyo ya lazima
wakati wa utoaji wa malipo.
Mhandisi wa RUWASA Wilaya ya Singida, Joel Kabusi
akizungumza kwa niaba ya Meneja wa RUWASA wa wilaya hiyo, Mhandisi Athumani
Mkalimoto alikiri kuwatambua vibarua hao na kueleza ni kweli walikuwa wakidai
fedha zao baada ya kumalizika kwa kazi ya mradi huo wa maji ambao umeanza
kufanya kazi.
"Malipo ya vibarua hawa yalichelewa kutolewa
kwa sababu za mifumo ya kibenki kama mnavyofahamu fedha za Serikali zinataratibu
zake zinavyotolewa na ilikuwa walipwe Ijumaa Aprili 5, 2024 lakini fedha hizo
ziliingizwa kwenye akaunti yetu toka benki jioni hivyo kwa usalama ikawa vigumu
kufanya malipo na ndipo tulipanga tuwalipe leo Jumamosi Aprili 6, 2024,"
alisema Mhandisi Kabusi.
Alisema kabla ya kufanyika kwa malipo hayo ndipo
vibarua hao walilazimika kuja ofisi ya mkuu wa wilaya kulalamika wakati tayari walikuwa
wamekwisha waeleza kuwa fedha zao zipo tayari kwa malipo na kuwa kiasi cha
fedha walichokuwa wakidai ni Sh.Milioni 12.5.
Mwakilishi wa vibarua hao Joshua Msumari kutoka
Mkoa wa Mara alisema walianza kufanya kazi hiyo kwa makubaliano ya kuchimba
mtaro na kufukia wenye urefu wa kilometa 10 ambapo kazi hiyo waliianza rasmi februari
26, 2024 na waliimaliza Machi 18, 2024 chini ya Mkandarasi aliyemtaja kwa jina
la Kajuna.
Alisema makubaliano yao ilikuwa kazi hiyo
waimalize kabla ya Machi 20, 2024 ambayo waliifanya kwa uaminifu mkubwa na
kuimaliza kwa wakati uliopangwa lakini kila walipokuwa wakidai madai yao tangu
wakati huo walianza kupigwa danadana na kuchukua uamuzi wa kwenda kumuona mkuu
wa wilaya ili awasaidie.
Msumari aliiomba Serikali kusimamia malipo baada ya kazi hizo zinazofanywa na vijana wazalendo kumalizika ili waweze kupata fedha zao kwa wakati jambo litakalosaidia kuepusha migogoro isiyo ya lazima na ambayo haina tija kama huo uliotokea.
0 Comments