Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)
SHEREHE ya Eid El-Fitr mkoani Singida
imesherehekewa kwa amani na utulivu kufuatia jeshi la polisi mkoani hapa kuweka
usimamizi mzuri katika maeneo mbalimbali yaliyokuwa na shamrashamra.
Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na eneo
maarufu sana la Ubungo ambalo wakati wote kunakuwepo na mahitaji ya vyakula
mbalimbali kama vile, nyama choma ya kuku,mbuzi, ng'ombe, chips, ndizi na
vyakula vingine vikiwepo vinywaji vya aina zote.
Katika eneo hilo pia zina patikana Ice Cream za Bakhresa zinazotengenezwa kupitia Kampuni ya AZAM na
vinywaji vyepesi vinavyotumiwa na watoto kama vya ukwaju vikiwepo vitafunwa vya aina mbalimbali, kaukau,
sambusa, maandazi na vichangamsha mdomo kama vile pipi za aina zote, ubuyu, chokureti na
vingine vinavyofanana na hivyo.
Mbali ya kupatikana kwa vitu hivyo pia katika
eneo hilo siku za sikukuu imekuwa ikipatikana huduma ya upigaji picha ambazo
zinasafishwa papo kwa papo jambo ambalo watu wengi kutoka maeneo mbalimbali ya
Manispaa ya Singida wamekuwa wakifika kupiga picha na familia zao na kuwa
kivutio kikubwa kwenye eneo hilo la Ubungo ambalo lipo katikati ya mji wa Singida.
Kivutio kingine kikubwa cha watu kuwapeleka
watoto wao kusherehekea katika eneo hilo ni usalama uliopo kwani askari polisi
wanakuwepo kwa ajili ya kuangalia fujo zisitokee na kuwavusha watoto kutoka
upande mmoja kwenda upande mwingine na kuweka vizuizi vya magari kutopita
katika eneo hilo.
Baadhi ya wananchi wameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwa kuruhusu eneo hilo kutumika kwa ajili ya biashara hizo ambapo waliomba liporeshwe zaidi kwa kuweka miundombinu rafiki kama vyoo na maji na wametumia nafasi hiyo kulipongeza jeshi la polisi kwa kupeleka askari wake kwa ajili ya kuhimarisha usalama.Hivi ndivyo ilivyokuwa kwenye eneo hilo.
0 Comments