" />

HABARI ZA HIVI PUNDE

TAKUKURU TANGA YAOKOA SH. MILIONI 439. 2 FEDHA ZA MAREJESHO MIKOPO 10%

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Victor Swella,

............................

Na Mashaka Kibaya, Tanga

TAASISI ya Kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Tanga imeokoa kiasi cha Shilingi 439,279,300/= ikiwa ni fedha za marejesho kutoka kwa wanufaika wa mikopo ya asilimi 10% katika halmashauri ya Jiji Tanga. 

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Victor Swella, aliyasema hayo leo Aprili 25 wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa Umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari juu ya utendaji kazi wao kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024.

Katika taarifa yake, Swella alisema, miongoni mwa kazi zilizofanywa na TAKUKURU kwa kipindi cha Januari - Machi 2024 ni ufuatiliaji wa ufanisi kwenye utekelezaji mkakati utoaji mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. 

Alisema kwamba,moja ya mambo yaliyobainika kwenye ufuatiliaji huo ni kutokuzingatiwa kwa masharti ya urejeshaji wa mikopo hiyo kwa wakati kutoka kwa Wanufaika.

Swella alitanabaisha kuwa, kabla ya ufuatiliaji kufanyika kiasi cha Shilingi 2,152,229,900 zilikuwa hazijarejeshwa kutoka kwa wanufaika wa mikopo hiyo huku muda wa kufanya marejesho ukiwa umepita.

Alisema kwamba, Takukuru baada ya kubaini hali hiyo,iliwakutanisha wadau na kuweka mapendekezo ya kurejesha fedha hizo na hadi kufikia Februari 2024 Shilingi 439,279,300.00 zilirejeshwa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga na kufanya fedha zisizorejeshwa kuwa Shilingi 1,712,950,600.00.

Kuhusu Programu ya Takukuru Rafiki Mkoani Tanga, Swella alisema, katika utekelezaji wameweza kuzifikia Kata 25, kero 284 zikitambuliwa na kuchambuliwa ambapo kero 163 zimetatuliwa na kero 121 zipo katika hatua mbalimbali za utatuzi. 

Pia taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), imeendelea na kufanya ufuatiliaji utekelezaji wa miradi ya maendeleo 46 iliyogharimu Shilingi 8,041,998,680.00 kwenye sekta za kipaumbele elimu, maji, afya na barabara. 

Katika ufuatiliaji huo, miradi 22 yenye thamani ya Shs. 4,866,068,966.00 ilibainika kuwa na mapungufu na ushauri umetolewa wa kuweza kurekebisha mapungufu hayo kupitia vikao vya wadau husika huku uchunguzi ukianzishwa kwa miradi ambayo ilibainika uwepo wa tuhuma za rushwa.

Miongoni mwa miradi inayochunguzwa ni manunuzi ya Shs. 6,400,000.00 ya uwekaji milango kwenye mradi wa ujenzi nyumba za wakuu wa idara katika Halmashauri ya wilaya ya Korogwe uliogharimu Shilingi 245,000,000.00.

Mradi mwingine ni ujenzi wa madarasa mawili, matundu 18 ya vyoo na mfumo wa uvunaji maji ya mvua uliyogharimu Shilingi 70,000,000.00 na uchunguzi unaofanyika ni ubadhilifu wa Shs. 30,000 000/= ujenzi wa matundu 18 ya vyoo na mfumo wa uvunaji maji ya mvua.

Kwa upande wa uelimishaji, Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Tanga alisema,katika utekelezaji jukumu hilo wamewafikia wananchi 586,485 kupitia mikutano ya hadhara 39.

Vilevile kumefanyika maonesho 11, wanafunzi wa shule na vyuo wanaofikia 28,364 kupitia uimarishaji klabu 70 za wapinga rushwa, pia makundi wadau watoa huduma yamefikiwa wakiwemo watumishi 1975 wa sekta binafsi na waliojiajiri katika fani mbalimbali zinazohusika na huduma za jamii.

No comments