TUNDU LISU KUUNGURUMA MKUTANO WA HADHARA SINGIDA KESHO KUTWA
..........................
Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)
BAADA ya vikao vya siku mbili mfululizo baina ya
viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Singida na
Jeshi la Polisi Wilaya ya Singida na Mkoa hatimaye chama hicho kimepatiwa kibari cha kuruhusiwa kufanya
maandamo ya amani na kuhitimishwa kwa kufanya mkutano wa hadhara Aprili 27,
2024 Stendi ya Mabasi ya Zamani mjini hapa ambapo Makamu Mwenyekiti wa chama
hicho Taifa Tundu Lisu atazungumza na wananchi wa Mkoa wa Singida.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Singida, Mutta Adrian
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandamano hayo alisema yatakuwa na
msafara mmoja utakaopita barabara ya Sepuka kuanzia Uwanja wa Maonesho wa
Mandewa kupitia Gineri, Uhasibu, Mataa ya FM Filling Station na maeneo mengine
ya katikati ya mji kama barabara ya Arusha kupitia Serengeti, eneo la Ubungo na
TCB na kuingia kwenye Stendi hyo ya
mabasi ya zamani.
Alisema maandamano hayo pamoja na mkutano huo wa hadhara utaanza saa.2; 00 hadi
saa 12;00 jioni na kuwa mkutano huo utahutubiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema
Taifa Tundu Lisu atakayeambatana na viongozi wengine mbalimbali.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida Jingu
Emmanuel alisema mkutano huo ni muhimu kwa wakazi wa Singida kwani utakuwa na
ajenda tano ambazo ni kuitaka Serikali kufanya marekebisho madogo ya katiba
iliyopo, kuendeleza madai ya katiba mpya ya wananchi kuitaka Serikali kushusha
gharama za maisha kwa kutumia mpango wa dharura.
Emmanuel alitaja ajenda nyingine kuwa ni kuitaka
Serikali kufuta au kurekebisha sheria mbovu
zilizopitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais na kuwa sheria rasmi na
kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.
Mwenyekiti huyo wa Chadema Mkoa wa Singida alitumia nafasi hiyo kuwaalika wananchi, maafiwa wa Serikali, viongozi wa dini, vyama vya siasa na makundi mengine yote kufika kwenye mkutano huo ambao utakuwa na mambo mengi ya muhimu ya kujadili mustakabari wa Taifa la Tanzania.
No comments