WANANCHI WILAYA MOMBA WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI KIPINDI HIKI CHA MVUA
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Momba Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Kennedy Msukwa, akitafakari jambo baada ya kutoa elimu ya madhara ya mvua zinazoendelea nchini na wilayani humo.
...............................
Na Issa Mwadangala (Polisi Songwe)
WANANCHI wa Kata Mkulwa Tarafa ya Kamsamba Wilaya
ya Momba mkoani Songwe wametakiwa kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha
mvua nyingi zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali wilayani humo.
Rai hiyo imetolewa Aprili 25,2024 na Mkuu wa
Polisi Wilaya ya Momba Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Kennedy Msukwa wakati
alipokuwa akitoa elimu juu ya madhara ya mvua nyingi zinazoendelea kunyesha
maeneo mbalimbali wilayani humo.
Msukwa amewataka wazazi na jamii kwa ujumla
kuongeza umakini katika malezi ya watoto hasa katika kipindi hiki cha mvua
nyingi zinazoendelea kunyesha ikiwa ni pamoja na kuwakataza kucheza michezo
hatarishi kama kucheza na kuogelea kwenye maji yaliotuama (madimbwi) mabwawa na
mito.
“Wazazi na walezi shughuli za kutafuta nguvu ya
tumbo ziende sambamba na malezi ya watoto msiwaache watoto wajilee wenyewe
kitendo ambacho kinapelekea watoto kusombwa na maji au kudumbukia kwenye
mabwawa, mito na visimani kitendo hiki kinapunguza kizazi cha kesho ambacho ni
hazina kwa taifa letu” alisema (SSP) Msukwa.
“Wavuvi mnatakiwa kufuata sharia na utaratibu wa
shughuli zenu za kila siku ikiwa ni pamoja na kufanya uvuvi salama pia
kuangalia hali ya hewa kabla ya kuingia kwenye shughuli zenu ili kujiepusha na
madhara ambayo yanaweza kuepukika ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uhalifu
na wahalifu pindi muonapo au mfanyiwapo kwa Jeshi la Polisi ili zishughulikiwe
kwa haraka ili maeneo yenu yaendelee kuwa salama” alisisitiza SSP Msukwa.
Baada ya elimu hiyo miti zaidi ya 100 ilipandwa katika Shule ya Sekondari ya Mkulwa iliyopo katika kata hiyo kwa lengo la kutunza mazingira shuleni hapo.
No comments