UFAFANUZI KUHUSU ATHARI ZA MAFURIKO YA KIBITI NA RUFIJI KUHUSISHWA NA UJENZI WA BWAWA LA JULIUS NYERERE (JNHPP)
Alhamisi, 11 Aprili 2024
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapenda kutoa ufafanuzi kwa Umma kuhusu athari za mafuriko yanayoendelea katika maeneo ya wilaya za Rufiji na Kibiti ambayo yanahusishwa na ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP)
Tunapenda kuujulisha umma kwamba uwepo wa Mradi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere umesaidia kwa sehemu kubwa kupunguza athari ya mafuriko katika wilaya za Rufiji na Kibiti ukilinganisha na miaka ya nyuma kabla mradi haujajengwa
Historia ya kitakwimu inaonesha kuwa maeneo ya Rufiji na Kibiti yamekuwa yakikumbwa na mafuriko kwa miaka mingi ya nyuma kwa kiwango kikubwa kuliko hali ilivyo hivi sasa. Mwezi Mei 1974 kiwango cha juu cha mafuriko katika mto Rufiji kilifikia mita za ujazo 13,200 kwa sekunde. Mwaka 1988 kiwango cha mafuriko kilifikia mita za ujazo 8,383.9, mwaka 2016 kiwango cha mafuriko kilifikia mita za ujazo 8,974.7, mwaka 2020 kiwango cha mafuriko kilifikia mita za ujazo 7158.5 na tarehe 15 Februari 2024 kabla ya Bwawa la Julius Nyerere kujaa maji, kiwango cha mafuriko ya maji kilichokuwa kinaingia kwenye Bwawa kilifikia mita za ujazo 8,444 kwa sekunde. Hata hivyo mafuriko hayo hayakufikia maeneo ya Kibiti na Rufiji kwa sababu Bwawa halikuwa limejaa, kiufupi ni kwamba Bwawa liliendelea kuhimili maji ya mafuriko tokea mwezi Disemba 2022 lilipoanza kujazwa maji mpaka mwishoni mwa mwezi Februari 2024 lilipojaa.
Baada ya Bwawa kujaa, maji ya mafuriko ya mto Rufiji yaliendelea kupita mtoni kama ilivyo asili yake na hivyo kusababisha mafuriko katika maeneo ya Kibiti na Rufiji jambo ambalo ni la kawaida kwa kila msimu wa mvua kwa mto huu.
Hivyo, kama Mradi wa JNHPP usingejengwa basi maji haya yangefika moja kwa moja kwenye maeneo ya Rufiji na Kibiti na hivyo kusababisha athari kubwa zaidi ya mafuriko na kwa vipindi virefu kuliko tulivyoshuhudia sasa.
Lakini kwa kuwa maji hayo ya mafuriko yalikuwa yakimezwa kwanza na Bwawa la Mradi na kutunzwa kwa muda mrefu, jambo hilo lilisaidia mafuriko kutotokea au kuonekana kwa mapema katika maeneo hayo ya Kibiti na Rufiji.
Ikumbukwe kwamba moja wapo ya sababu ya kuanzishwa Mradi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) katika maeneo ya Rufiji ni kwa sababu ya uwepo wa maji ya mafuriko katika bonde la mto Rufiji hali iliyopelekea Serikali kuamua kuyatumia mafunko hayo ya maji kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Kama eneo hilo la Bonde la Mto Rufiji lisingeonekana kuwa na maji mengi ya mafuriko kila mwaka basi hata Serikali isingeamua kuwekeza mradi wa Bwawa katika eneo hilo.
Tunapenda Umma ufahamu kwamba mwaka huu kumekuwepo na mvua kubwa za El-nino ambazo zimepelekea kuwepo kwa mafuriko makubwa katika maeneo mengi ya nchi yetu ikiwemo maneo ya yanayopeleka mtirinko wa maji ya mvua kwenye Bonde la Mto Rufiji, Hivyo kiwango kikubwa cha mafuriko katika maeneo hayo ya Kibiti na Rufiji kimesababishwa na mvua kubwa za El-nino zinazoendelea kunyesha.
Na kwa sehemu nyingine kumesababishwa na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi ambapo kutokana na kupanda kwa vina vya bahari, kumekuwepo na upungufu wa spidi ya maji ya mito kuingia baharini hasa wakati maji ya bahari yanapokuwa yamejaa yaani "High Tide".
Hivyo kwa maelezo yaliyopo kwenye taarifa hili, Shirika la Umeme Tanzania inakanusha taarifa zozote za upotoshaji zinazohusisha Bwawa la Julius Nyerere na mafuriko ya Kibiti na Rufiji na linakemea upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu wasio na nia njema kubeza juhudi za Serikali katika kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini kwa ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere.
Shirika linaendelea kuwasihi wananchi kuwa watulivu na kuendelea kufuatilia taarifa sahihi zinazotolewa na mamlaka husika ili kuendelea kujiweka katika hali ya usalama na kuondoa taharuki isiyo na ulazima
Imetolewa Na
KURUGENZI YA MAWASILIANO NA UHUSIANO KWA UMMA TANESCO-MAKAO MAKUU
DODOMA
0 Comments