WIZARA YA ARDHI YAANDAA KLINIKI YA KUSIKILIZA KERO WILAYA YA MANYONI

Subscribe Us

WIZARA YA ARDHI YAANDAA KLINIKI YA KUSIKILIZA KERO WILAYA YA MANYONI

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Shamimu Hoza, akizungumza na wananchi katika moja ya mikutano yake ya kuhamasisha matumizi bora  ya ardhi Wilaya ya Manyoni ambapo pia wananchi walikabidhiwa hati za umiliki wa ardhi.

..........................

Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog)

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa kliniki ya kusikiliza kero za wananchi kuhusu masuala ya ardhi Wilaya ya Manyoni Mkoa wa Singida kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi wa kuzitatua.

Akizungumza na Singidani Blog Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Shamimu Hoza alisema kliniki hiyo itafanyika kwa kuwasikiliza wananchi wote wenye changamoto za ardhi na kuzipatia ufumbuzi.

"Kliniki hiyo inatarajiwa kufanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia Aprili 17, 2024 hadi Aprili 19, 2024 ambayo itafanyika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuanzia saa tatu asubuhi," alisema Shamimu.

Shamimu alisema wahusika watakao kuwa wakisikiliza changamoto za wananchi hao kuhusu ardhi ni wataalamu na viongozi kutoka makao makuu ya wizara hiyo , Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, viongozi wa wilaya ya Manyoni pamoja na wataalamu wote wa ardhi waliopo Mkoa wa Singida.

Shamimu aliwaomba wananchi wote wenye changamoto za masuala ya ardhi kujitokeza kwa wingi kufika kwenye kliniki hiyo ambayo huduma zinatolewa bure.

Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Dkt. Pius Chaya ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wote wa Wilaya ya Manyoni wenye changamoto za masuala ya ardhi kufika kuhudhuria kliniki hiyo ambayo ni muhimu kwa ajili ya kusikilizwa ili kero zao ziweze kuchukuliwa na wahusika na kutafutiwa ufumbuzi. 

Post a Comment

0 Comments