" />

HABARI ZA HIVI PUNDE

WATAALAMU WA AFYA KUTOKA NCHINI SIERRA LEONE WATEMBELEA MSD KUJIFUNZA

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai, akizungumza na wataalamu wa Afya kutoka Sierra Leone ambao wametembelea MSD kwa lengo kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu shughuli zinazofanywa na Bohari hiyo Aprili 29, 2024.

.......................

Na Mwandishi, Wetu

WATAALAMU wa Afya kutoka nchini Sierra Leone lwametembelea Bohari ya Dawa (MSD) kwa lengo kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu shughuli za Ugavi, Uhifadhi, Uendeshaji, Ununuzi, Huduma kwa Wateja, Sera, Udhibiti Ubora, pamoja na mambo mengine yanayohusu mnyororo wa Ugavi wa bidhaa za afya.

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Afya wakati wa kuukaribisha ujumbe huo nchini, Mfamasia Mkuu wa Serikali Daudi Msasi, amesema ujio wa wageni hao ni ishara kwamba kama nchi tumeboresha na kuimarisha Bohari yetu katika utoaji wa huduma, ndio maana wengine wanakuja kujifunza.

Amesema Tanzania ipo tayari kuwapa ushirikiano wa kutosha kwa maslahi mapana ya wananchi wa Afrika.

“Ukiona mtu amechambua nchi mbalimbali, akaja kajifunza Tanzania inamaanisha tunafanya vizuri na ndio maana ndugu zetu hawa wakachagua kuja hapa kujifunza, hivyo ni ugeni mzito ambao umeongozwa na Mganga mkuu wa nchi yao”.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai, amebainisha kwamba kutokana na mabadiliko ya kiutendaji, MSD imeendelea kuvutia wengi kuja kujifunza na kuimarisha mnyororo wa Ugavi wa bidhaa za afya katika nchi zao.

“Tunakumbuka Sierra Leon ni nchi ambayo ilikubwa na matatizo ya amani ambayo yalivunja vunja mfumo mzima wa afya na sasa wameamka na kujikung’uta na kuanza upya mfumo wao wa afya na sasa wamekuja huku kujifunza namna ya sisi tunavyofanya kazi zetu.

Amesema moja ya kitu kilichowavutia zaidi ni ubunifu ambao MSD wamekuwa nao katika kufanya shughuli zao za kuzalisha, kununua, kutunza na kusambaza dawa lakini pia uhimilivu wa kifedha sambamba na matumizi ya Tehama.

Aidha ameongeza kuwa kupitia ziara hiyo, wamejadiliana jinsi Bohari ya Dawa ya Sierra Leone inavyoweza kushirikiana na wadau wengine ndani ya serikali na nje ya serikali ikiwemo kuunganisha mifumo yao na idara mbalimbali, kama fedha, utumishi, wateja, na wizara ya afya ya nchi hiyo, ili kuwa na mnyororo wa Ugavi imara na endelevu wa Bidhaa za afya.

Kwa upande mmoja wa viongozi waliombatana na ujumbe huo, ambaye ni Mfamasia Mkuu wa Sierra Leone Dkt. Moses Batema amesema kabla ya ujio huo wamefanya utafiti wa kutosha na kuona sehemu ya kwenda kujifunza ni Tanzania hivyo wameridhishwa na majadiliano walioyafanya lakini pia wamejifunza vitu vingi vitakavyowasaidia kuboresha Bohari yao.

Ujumbe huo kutoka Sierra Leone ulioko nchini kwa ziara ya siku 4, chini ya uenyeji wa MSD, unajumuisha Mganga Mkuu (Wizara Ya Afya SL), Mfamasia Mkuu (WAF-SL), Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya NMSA ambayo ina majukumu kama MSD, Mkurugenzi Mkuu NMSA, Msajili wa Bodi ya wafamasia (SL), Mkuu wa Ugavi (WAF SL), Mkurugenzi wa Ununuzi (NMSA), Mkurugenzi wa Ugavi (NMSA), baadhi ya watumishi kutoka Global Fund na UNFPA kutoka nchini SL

Wataalamu wa Afya kutoka nchini Sierra Leone wakiwa kwenye kikao na wenyeji wao  Bohari ya Dawa (MSD)
Wataalamu wa Afya kutoka nchini Sierra Leone wakitembea ghala la kuhifadhi vifaa tiba na dawa la Keko jijini Dar es Salaam.
Utembeleaji wa ghala la kuhifadhia dawa na vifaa tiba ukifanyika.
Picha ya pamoja..
Kikao kikiendelea MSD.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai, akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
 

No comments