...................................
Na Mwandishi Wetu, Singidani Blog.
WACHUNGAJI Wanafunzi zaidi ya 60 kutoka Chuo Kikuu cha
Teofilo Kisanji (TEKU) cha Kanisa la Moravian Tanzania kilichopo Mkoa wa Mbeya wanatarajia
kufika Mjini Singida kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za uinjilisti.
Mchungaji Oscar Falanga wa Kanisa hilo Jimbo la
Magharibi Tabora ambaye ni Msimamizi wa kanisa hilo Mkoa wa Singida alisema
kuwasili kwa wachungaji hao mkoani Singida ni neema kubwa kwa wananchi wa mkoa
huo.
Alisema mara baada ya kuwasili wachungaji hao
watapata fursa ya kutoa mafunzo mafunzo ya ujasiriamali, uchumi, makuzi ya
watoto haki zao na za wanawake.
Alisema ziara hiyo ya mafunzo itafanyika nyumba
kwa nyumba na pia kutakuwa na matendo ya huruma ambapo watasaidia makundi
yasiyojiweza na watoto yatima kwa kutoa zawadi mbalimbali.
Mchungaji Falanga alisema pamoja na mafunzo hayo
wachungaji hao watafanya mikutano ya neno la Mungu kila siku katika viwanja vya
Kanisa la Moraviani la Mandewa ambalo lipo nyuma ya Hospitali ya Rufaa ya
Mandewa.
"Jumapilin ya Mei 19, 2024 wachungaji hao
wataendesha semina na kushiriki ibada katika Kanisa Kuu la Moravian lililopo
Mjini Singida.
Pamoja na mambo mengine wachungaji hao
watakapokuwa mjini Singida watapata fursa ya kuonana na viongozi wa Serikali ya
Mtaa na Afisa Mtendaji ambao watashirikiana nao katika masuala mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kupata idadi ya watu kutoka
makundi maalumu wakiwemo watoto yatima, wajane, wagane na wengineo kwa lengo la
kuwa na idadi yao ili pindi kanisa hilo likipata nafasi liweze kuwasaidia kwa
namna moja au nyingine kulingana na mahitaji watakayokuwa nayo kwa wakati
husika.
Mchungaji Falanga alitumia nafasi hiyo kuwaalika wana Singida na madhehebu mengine kwenda kushirikiana na wachungaji hao kwa mambo mbalimbali kwani huduma itakayotolewa ni ya bure.








No comments:
Post a Comment