BURIANI MCHAPA KAZI HODARI, PETER LISSU MWENDO UMEUMALIZA KAPUMZIKE KWA AMANI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, 10 June 2024

BURIANI MCHAPA KAZI HODARI, PETER LISSU MWENDO UMEUMALIZA KAPUMZIKE KWA AMANI

Mjane wa marehemu, Victoria Mkenga (kushoto) akifarijiwa na rafiki yake kutokana na kifo cha mume Peter Lissu kilichotokea Juni 8, 2024 kwa ajali ya gari eneo la Mkiwa wilayani Ikungi mkoani Singida.

................................ 

Na Dotto Mwaibale, Singidani Blog

 

HUZUNI, Vilio, Simanzi na Majonzi vimetawala kwa ndugu jamaa na marafiki kufuatia kifo kilicho sababishwa na ajali cha mpendwa wao Peter Lissu mdau mkubwa wa maendeleo Mkoa wa Singida ambaye aliwahi kuhudumu katika Shirika lisilo la Kiserikali la Sustainable Environment Management Action (SEMA ) na baadae Shirika la Research And Development Organization – ReDO Tanzania lililopo mkoani Singida.

 

Kifo cha Lissu ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika mashirika hayo ambaye pia alikuwa ni Mjumbe wa Baraza la Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NACONGO) kimetokea usiku wa Juni 8, 2024 kwa ajali ya gari alilokuwa akiliendesha kutoka Manyoni kugongana na gari lingine eneo la Mkiwa lililokuwa likitokea Singida mjini na kusababisha kifo chake papo hapo.

 

Dada wa Marehemu Consolata Lissu akizungumzia ajali hiyo alisema kaka yake Lissu alipata ajali hiyo iliyochukua uhai wake majira ya saa 8 usiku wakati akitokea kwenye sherehe ya harusi ya mpwa wake Maria Kilima ambaye alikuwa anaolewa.

 

“Baada ya sherehe hiyo kaka yangu aliondoka kurudi Singida huku kwenye gari akiwa na rafiki zake wawili na wakiwa njiani walipofika eneo hilo la Mkiwa ndipo alipopata ajali na kufariki papo hapo huku rafiki yake Francis Nikas ambaye alijeruhiwa kwa kuvunjika mguu akipelekwa Hospitali ya Benjamin jijini Dodoma kwa matibabu,” alisema dada yake Lissu.

 

Dada yake Lissu alisema rafiki yake mwingine aliyekuwa naye kwenye gari hilo aliyemtaja kwa jina moja la Matalisi yeye alipelekwa kupata matibabu Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.

 

Consolata alisema mwili wa marehemu ulifikishwa Mjini Singida jana jioni na kuhifadhiwa Hospitali ya Manispaa ya Singida wakati wakisubiri taratibu zingine za mazishi ambayo yatafanyika siku ya Alhamisi Juni 13, 2024 mjini Singida katika makaburi ya Mitunduruni na kuwa marehemu ameacha mjane na watoto watano.

 

Mkurugenzi Mwenza wa Shirika hilo la ReDO , Hudson Kazonta alisema kifo cha Lissu kimetokea wakati akihitajika mno kutokana na mipango mbalimbali waliyokuwa nayo na kuwa kimeacha pengo kubwa na kwamba yale yote mazuri aliyokuwa akiyafanya watayaenzi.

Mwanahabari Leonard Manga akimpa pole mjane wa marehemu, Victoria Mkenga.
Dada wa marehemu Consolata Lissu akimfariji jamaa yake aliyefika nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya msiba huo.
Wakina mama wakiwa kwenye msiba huo nyumbani kwa marehemu eneo la Mwaja Singida mjini.
Mwanahabari Fednand Irunde akitoa pole kwa baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wa marehemu Peter Lissu.
Mwanahabari Abby Nkungu akitoa pole kwa wafiwa.
Ndugu jamaa na marafiki wa marehemu wakiwa kwenye msiba huo.
Muonekano nyumbani kwa marehemu eneo la Mwaja baada ya kutokea msiba huo.
Marehemu Peter Lissu akiwa katika moja ya matukio ya kikazi enzi za uhai wake.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad