Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Al- Firdaws Investment Co Ltd kutoka nchini Jordan, Ahmed Al Khatib (katikati mwenye shati jeupe) jinsi kifaa cha kisasa cha kutafutia maji ardhini kinavyofanya kazi wakati wa ziara yake ya siku moja ya kikazi alipotembelea kwenye eneo la uwekezaji la kampuni hiyo lililopo Kijiji cha Choda Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Julai 28, 2024.
...........................
Na Dotto Mwaibale, Singida
SERIKALI kushirikiana na Kampuni ya Al- Firdaws Investment Co Ltd kutoka nchini Jordan kwa ajili ya kupata maji kutoka ardhini yatakayotumika kwa shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wakati akizungumza na wataalamu kutoka Sekta ya maji alipokuwa katika ziara ya kikazi ya siku moja katika Kijiji cha Choda kilichopo wilayani Ikungi mkoani Singida baada ya kupata maelezo ya upatikanaji wa maji kutoka ardhini kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayofanywa na kampuni hiyo.
Waziri Aweso alifika katika kijijini hicho kuona uanzishwaji wa shamba la umwagiliaji linalomilikiwa na kampuni hiyo walilopatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Aidha, Aweso alisema kuwa changamoto kubwa tuliyonayo hapa nchini ambayo inasababisha kukosekana kwa maji ni kuwa na teknolojia duni hivyo kupitia kampuni hiyo chini ya mwekezaji huyo wanakwenda kufanya mapinduzi makubwa ya upatikana wa maji na kupata suluhisho.
" Kuwa na watu wa aina ya Firdaws ni neema kubwa” alisema Aweso.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mwajuma Waziri alisema kuwa Tanzania ina changamoto nyingi za maji hivyo ni vizuri kuiga mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini Jordan kwa kutumia teknolojia hiyo mpya ya upatikanaji wa maji kutoka ardhini.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Al-firdaws, Ahmed Al Khatib alisema wao wana uzoefu wa kutosha na kuwa kama wataaminiwa na kupewa kazi hiyo wataona matunda yatokanayo na kazi hiyo kutokana na huduma bora watakayoipata kutoka kwa mwekezaji huyo.
Akimzungumzia Mwekezaji huyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi alisema kuwa tayari halmashauri hiyo imempatia Mwekezaji huyo ekari 11,700.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi, Shabani
Muhimbani alisema uwekezaji mkubwa unaofanywa na kampuni hiyo ni utekelezaji wa
ilani ya chama hicho chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na kuwa una kwenda kutoa
ajira kwa makundi mbalimbali hasa vijana.









No comments:
Post a Comment