Na Leandra Gabriel, Dar es Salaam
KAMATI ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar limepongeza jitihada za
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) katika utekelezaji wa miradi ikiwemo
kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mawasiliano pamoja kutoa elimu kwa
shirika la Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA.) katika kuhakikisha watanzania
wanapata huduma za mawasiliano.
Akizungumza leo wakati wa ziara ya kamati hiyo katika ofisi za Makao Makuu
ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa
Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mwanaasha Juma amesema
wametembelea TTCL na kujifunza namna wanavyofanya kazi na taratibu za
kiutendaji pamoja na kujadiliana namna ya kukabiliana na kutatua changamoto
ndani ya taasisi.
“Tumejifunza vitu vingi sana, Zanzibar katika wizara yetu ya Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi inahusika na usimamizi ikiwemo miundombinu ya TEHAMA na
uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano na kwa upande wa Tanzania bara Wizara
ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia TTCL na wadau wengine
wanatekeleza majukumu hayo pia ya kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaimarika
zaidi.” Amesema.
Aidha kuhusiana na sheria inayoiruhusu TTCL kutoa gawio kwa Serikali Bi.
Mwanaasha amesema ikifika hatua hiyo wanaweza kutoa gawio ili fedha hizo
zielekezwe katika miradi mbalimbali ya maendeleo itakayowanufaisha wananchi.
Amesema, wamefurahi namna Fedha zinazotolewa na Serikali kwa TTCL pamoja na
vyanzo vyao vya mapato zinavyoelekezwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo
ambapo pia wanafanya kazi kwa upande wa Zanzibar hususani katika mikongo ya
Taifa kwa kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya mawasiliano.
Aidha amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu
Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hussein Ali Mwinyi kwa
kuweka miundombinu imara na kuhakikisha sekta ya mawasiliano inaleta tija kwa
wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,)
CPA. Moremi Andrea amesema; ujio wa kamati hiyo umelenga kujifunza pamoja na
kukagua shughuli zinazofanywa na shirika hilo.
“Tumepata fursa ya kutoa wasilisho kwa kamati linalohusu masuala ya
kiutendaji, mikakati na biashara na tumepokea maelekezo na menejimenti
tutayafanyia kazi….Tunashukuru kwa ujio huu na tutaendelea kushirikiana na
wenzetu waliopo upande wa Zanzibar ili kukuza sekta ya mawasiliano.
Wajumbe wa kamati hiyo pia wametembelea Kituo cha Uangalizi na Uendeshaji
wa Mtandao (NOMC,) pamoja na Miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
0 Comments