Na Dotto Mwaibale
MKURUGENZI
Mpya Manispaa ya Singida (MD), Joanfaith
Kataraia ameanza kazi rasmi kwa kutaja
vipaumbele ambavyo ameona ni vya muhimu
wakati wa kutekeleza majukumu ya kazi.
Kataraia
amevitaja vipaumbele hivyo wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya
Singida katika hafla fupi ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkurugenzi wa
Manispaa hiyo Jeshi Lupembe ambaye amehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya
Morogoro baada ya kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na yeye kuhamishiwa
Manispaa ya Singida.
Kataraia ametaja
kipaumbele chake cha kwanza kuwa ni ukusanyaji wa mapato ambayo ndio jicho la
halmashauri, kusimamia miradi na kuhakikisha inamalizika kwa wakati na kwa
viwango kulingana na fedha halisi zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan.
Alitaja vipambele
vingine kuwa ni watumishi kuwa wabunifu katika kazi zao ili kuongeza ubora wa
kuzijibu hoja za Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali (CAG) na akaeleza kuwa kuwa na hoja nyingi ni changamoto.
“Tunachotakiwa ni
kuzipunguza kabisa hoja hizo na kama zitabaki basi ziwe zile zinazoshughulikiwa
na mamlaka za Serikali ambazo zipo juu yetu
ni wajibu wetu kuzisimamia” alisema Kataraia.
Kipaumbele chake
kingine aliwaomba watumishi wa manispaa hiyo kusimamia fedha za Serikali na
kuhakikisha mikopo ya asilimia kumi inayotolewa inarudi na wakuu wa idara hiyo
ndio kazi yao na kuwa fedha zote zinazokusanywa kutoka vyanzo vya mapato
mbalimbali zipelekwe benki pasipo kuwa na sababu yoyote.
Alitaja jambo
linguine ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi kwa nguvu zote ni kutoa huduma bora
kwa wananchi kwani Rais Samia amekwisha boresha mazingira kwa kujenga madarara,
vituo vya afya na miradi mingi kilichobaki ni watumishi kutoa huduma.
Aliwataka
watumishi hao kupendana na kufanya kazi kwa kushirikiana hasa kwa wakuu wa
idara kuwasaidia wenzao wa chini ili nao waweze kufurahia kufanya kazi Manispaa
ya Singida jambo ambalo litampendeza hata Mwenyezi Mungu.
Aidha,
Kataraia alihimiza kudumisha mauhusiano
mazuri baina ya chama na Serikali na kueleza kuwa chama ndio chenye ilani na
wao ni watekelezaji na jambo hilo linatakiwa kudumishwa kwa mustakabari wa nchi
yetu.
Kwa upande wake
aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Jeshi Lupembe alitaja baadhi ya mafanikio
yaliyopatikana kuwa ni Halmashauri hiyo kupata mradi
mkubwa wa kuwa na jengo jipya la Manispaa ambalo litakidhi vigezo na mahitaji
ya sasa katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema jengo
hilo lina gharama ya Sh.3,000,000,000.00 na mpaka sasa wamepokea Sh.2,000,000,000.00
ujenzi bado unaendelea. ambapo baadhi
ya vifaa vya umaliziaji kama mabati na Gpysum 150, Mabati 600, Ndoo za
rangi 334 mbao za paa
1,460, Tiles box 1,026 vimeshanunuliwa na kuhifadhiwa katika Stoo.
Ujenzi wa Nyumba ya Mkurugenzi unaendelea na wamepokea
kiasi cha Sh. 180,000,000 kwa ajili ya utekelezaji. Hadi kufikia Agosti
19,2024 ujenzi umefikia hatua ya kupiga
ripu ili waanze hatua ya ukamilishaji ambapo kiasi cha Sh. 169,045,066 kimeshatumika. vifaa vya ukamilishaji
ambavyo ni mabati, mbao za paa na rangi vimeshanunuliwa na kuhifadhiwa stoo.
Halmshauri hiyo imefanikiwa kupokea fedha za ukamilishaji kwa Ofisi ya Kata ya Minga
shilingi 10,000,000.00 pamoja na fedha za ukarabati wa Ofisi ya Kata ya
Mughanga iliyoharibiwa na mvua kipindi cha masika April, 2024 shilingi
1,700,000.00.
Aidha kwa
mwaka wa fedha 2024-2025 wametenga kwenye bajeti fedha kwa ajili ya
ukamilishaji wa Ofisi za Kata za Mtipa na Mitunduruni, Ofisi za Vijiji viwili
vya Kinyakaya na Ughagha ‘A’ na Ofisi za Mitaa ya Mahembe, Myituka, Mwenge na
Isomia yote kwa pamoja ikiwa na thamani ya shilingi 132,000,000.00.
Baadhi ya viongozi wengine waliopata nafasi ya
kuzungumza katika hafla hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin
Gondwe,Mstahiki Meya, Yagi Kiaratu, Naibu Meya, Hassan Mkata, Naibu Meya
aliyemaliza muda wake Geofrey Mdama, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya
Singida na Katibu Tawala Wilaya ya Singida, Naima Chondo ambao wote kwa pamoja walimshukuru
Jeshi Lupembe kwa kazi kubwa aliyoifanya na kumtakia kazi njema katika kituo
chake kipya cha kazi.
Aidha viongozi hao walimkaribisha Mkurugenzi Mpya wa Manispaa ya Singida, Joanfaith Kataraia na kuahidi kumpa ushirikiano kama walivyokuwa wakifanya kwa Jeshi Lupembe.
Mkurugenzi Mpya wa Manispaa ya Singida, Joanfaith Kataraia akizungumza na watumishi wa manispaa hiyo (hawapo pichani)Mkurugenzi Mpya wa Manispaa hiyo, Joanfaith Kataraia , akiwa katika picha ya pamoja na Aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo ambaye amehamishiwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Jeshi Lupembe.
0 Comments