Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, akihutubia katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Vijana Kimataifa 2024, yaliyofanyika Golden Tulip Hotel, Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
..............................
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali
Mwinyi amesema tayari Serikali imeshatenga kiasi cha shilingi bilioni 31.8
kupitia Wakala wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, ikiwemo kuwawezesha vijana.
Tayari shilingi milioni 338.6 zimetolewa kwa makundi mbalimbali.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Vijana
Kimataifa 2024, yaliyofanyika Golden Tulip Hotel, Airport, Mkoa wa Mjini
Magharibi, Unguja.
Aidha, Dk. Mwinyi ameeleza kuwa tayari vijana 500,000 wanaendelea kupata
mafunzo ya stadi za maisha, mafunzo ya matumizi ya TEHAMA, na ujasiriamali.
Rais Mwinyi ameridhia maombi yaliyotolewa na vijana katika maadhimisho
hayo, ikiwa ni pamoja na kuzingatia suala la maendeleo ya vijana katika mipango
yao na kuongezwa kwa bajeti ya wizara katika masuala yanayohusu vijana na
taasisi za mikopo ili kuwawezesha vijana kupata mikopo kwa wepesi na kwa
urahisi.
Aidha, Dk. Mwinyi amewataka vijana kushiriki kwa wingi na kugombea katika
uchaguzi mkuu ujao na kuahidi kuongeza idadi ya vijana katika uteuzi wa
nyadhifa mbalimbali Serikalini.
Naye, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, na Michezo Mhe. Tabia Maulid
Mwita amesema juhudi zinaendelea za kuimarisha vituo vya stadi za maisha na
tayari Serikali imetenga shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa kituo
kikubwa cha kuwawezesha vijana.
0 Comments