DKT. MAHERA AKEMEA TABIA YA WAZAZI WANAOWAFICHA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Sunday, 22 September 2024

DKT. MAHERA AKEMEA TABIA YA WAZAZI WANAOWAFICHA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahera akifunga maadhimisho hayo kwa niaba ya waziri wa elimu .
------------------------------

Na Mwandishi wetu ,Arusha .
Arusha .Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahera, amekemea vikali tabia  ya wazazi wenye tabia ya kuwaficha watoto wenye mahitaji maalumu  na kuwanyima  haki zao za msingi kuacha tabia hiyo mara moja kwani watoto wote wana haki  kama wengine .
Ameyasema hayo mkoani Arusha wakati akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda katika  ufunguzi wa  Maadhimisho ya Miaka ya 30 ya Elimu Jumuishi hapa nchini  yaliyofanyika katika chuo cha elimu maalumu Patandi .
Amesema kuwa,  watoto wenye mahitaji maalumu wamekuwa wakipitia changamoto  mbalimbali  zinazosababishwa na wazazi ama walezi wenyewe ikiwemo ya kunyanyapaliwa na kunyimwa haki zao za msingi.
“Nawaombeni wazazi mshirikiane  pamoja na serikali kuwaripoti  watoto wote wenye mahitaji maalumu  waliopo kwenye maeneo yenu ili waweze kupata haki zao za msingi kwenye vituo maalumu ambavyo vimeainishwa na serikali kwani wana haki kama walivyo watoto wengine.”amesema Dkt.Mahera.
Dkt. Mahera amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa lengo naomba 4 la malengo ya milenia ya mwaka 2030 linalosisitiza usawa pamoja na kutekeleza Azimio la Musoma la mwaka 1974, ambalo lililochagiza kila Mtanzania kupata fursa ya elimu.
“Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi Serikali imefanikiwa kuyafikia makundi yote ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo wanafunzi wenye ulemevu, magonjwa ya kudumu pamoja na wanafunzi wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini.”amesema Dkt .Mahera.
“Tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa miongozo inayoelekeza wadau wa elimu kutoa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji Maalumu hususani wenye kiwango kikubwa cha ulemavu” amesema Dkt. Mahera.
Naye  Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anaye shughulikia elimu Atupele Mwambene amewaasa Maafisa Elimu Maalum wa Wilaya kuhakikisha wanaelewa vyema mikakati na miongozo ya utekelezaji wa elimu Jumuishi ili kuwa na ufanisi mzuri wa majukumu yao.
Mwambene amesema Serikali itaitekeleza kwa vitendo na kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanajengewa maadili mazuri kwa kuimarisha vituo vya malezi, ushauri na unasihi ili viweze kutoa huduma nzuri.
“Tutaendelea kusimamia utekelezaji wa zoezi la ubainishaji wa Watoto wenye mahitaji maalumu na kuhakikisha wanaandikishwa shule na kupatiwa afua stahiki kulingana na mahitaji waliyonayo”. amesema Mwambene.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad