POLISI SINGIDA YAKAMATA WATUHUMIWA 137, YAMFIKISHA MAHAKAMANI MGANGA WA KIENYEJI KWA TUHUMA ZA MAUAJI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, 19 September 2024

POLISI SINGIDA YAKAMATA WATUHUMIWA 137, YAMFIKISHA MAHAKAMANI MGANGA WA KIENYEJI KWA TUHUMA ZA MAUAJI

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mayunga Mayunga akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani( pikipiki zilizokamatwa kwa makosa mbalimbali.

....................................

Imeandaliwa na Dotto Mwaibale

(0754-362990)

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida katika kuimarisha ulinzi na usalama limeendelea kufanya doria na misako ili kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu ambapo katika kipindi cha Mwezi Julai-August 2024 limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 137 waliojihusisha na makosa mbalimbali ya jinai pamoja na vielelezo vinavyowaunganisha na makosa yao.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mayunga Mayunga akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa hiyo alisema watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya kutenda makosa tofauti tofauti.

Alitaja makosa hayo kuwa ni pamoja na mauaji watuhumiwa 21, watuhumiwa 34 kwa kukutwa na pikipiki 31 zidhaniwazo kuwa ni za wizi, watuhumiwa 21 wakiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi zenye uzito wa gramu 8773, watuhumiwa 4 wamekamatwa na dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa gramu 19,842 na mtuhumiwa 01 akiwa na dawa za kulevya aina ya Heroini yenye uzito wa gramu 0.5.

Alisema vilevile, walikamatwa watuhumiwa 15 wakiwa na Pombe ya Moshi lita 78, watuhumiwa 05 kwa makosa ya kubaka, watuhumiwa watatu walikamatwa kwa wizi wa kompyuta mbili, watuhumiwa watano wamekamatwa na Simu ndogo za batani 30,watuhumiwa wane wamekamatwa na mitungi miwili midogo ya gesi.

Watuhumiwa wengine ni aliyekamatwa na Tv  mbili, aina ya Rising ,mtungi wa gas mdogo mmoja , Redio subufa moja , Remote za tv tatu , m tuhumiwa mmoja amekamatwa kwa wizi wa mifugo; mbuzi nane , watuhumiwa watatu kwa kukutwa na nyara za serikali ambazo ni; ngozi ya mnyama aina ya Insha moja, kichwa cha mnyama aina ya Pofu  mmoja, jino la mnyama aina ya Ngiri moja na kucha moja ya mnyama aina ya Muhanga na mtuhumiwa 01 kwa kosa la kuchezesha kamali bila kibali na mtuhumiwa mmoja akikamatwa Tv inchi 32 flat screen aina ya zune moja.

Aidha, Kamanda Mayunga alisema baadhi ya watuhumiwa hao  wameshafikishwa mahakamani akiwemo Kamba Kasubi ambaye ni Mganga wa Kienyeji na wenzake 13 wanaotuhumiwa kwa mauaji ya watu watatu katika Kijiji cha Makuro Singida na mauaji ya watu saba katika Kijiji cha Porobanguma, Wilaya ya Chemba Dodoma huku wengine upelelezi dhidi yao ukiendelea ambapo watafikishwa mahakamani mara baada ya taratibu hizo kukamilika.

Mayunga alisema katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limepata mafanikio ya kesi zilizofikishwa mahakamani ambapo kwa mwezi Julai-August 2024 washitakiwa 43 walihukumiwa baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi uliowasilishwa kuhusiana na makosa ya jinai waliyoyatenda.

Hukumu hizo ni pamoja na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa washitakiwa watano wa makosa ya mauaji, washitakiwa wawili kwenda jela maisha kwa kulawiti, mshitakiwa mmoja  akihukumiwa jela maisha kwa kosa la kubaka na washitakiwa wengine watano wakihukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa makosa ya kubaka. 

ACP Mayunga alisema kwa upande wa kudhibiti makosa ya usalama barabarani, wapo madereva waliofungiwa leseni miezi mitatu kwa makosa makubwa ya kuendesha magari kwa mwendo kasi usioruhusiwa kisheria ambao ni hatari kwa maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.

Madereva hao ni Raphael Emmanue Gusha wa Kampuni ya Katarama , Habiee Neema Sule wa Kampuni ya Mwanakwetu, Emmanuel Wilson Madaha wa Kampuni ya Katarama  Luxury, Emmanuel Laizer Malambala wa Kampuni ya Happy Nation na Jofu Mnison Kanyika wa Kampuni ya Frester ambao waliendesha magari yao kwa mwendo wa zaidi ya Km 100 kwa saa badala ya km 80 kwa saa.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linawashukuru wananchi kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kubaini na kuzuia uhalifu na wahalifu kwa kutoa taarifa na linawaomba kufika mahakamani kutoa ushahidi ili kesi zote ziweze kupata mafanikio.

Pia linawataka madereva kuzingatia taratibu, kanuni na Sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali ambazo zinaweza kuzuilika. 

ACP Mayunga akionesha madumu ya pombe ya moshi (GONGO) iliyokamatwa na jeshi hilo maeneo mbalimbali Mjini Singida.
Mayunga akionesha simu za aina mbalimbali zilizokamatwa baada ya kuibiwa.

Kaimu Kamanda Mayunga, akionesha misokoto bhange iliyokamatwa.
Hapa akionesha Redio aina ya subufa iliyokamatwa.
Hapa akionesha TV za aina mbalimbali zilizokamatwa.
Muonekano wa Pikipiki zilizo kamatwa na jeshi hilo.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad