*Inadaiwa alipoteza maisha kwa kucheleweshewa huduma, kisa hela ya mafuta ya ‘ambulance’
Na MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka amelazimikia kuunda kamati maalumu kuchunguza chanzo cha kifo cha mjamzito ambacho kinadaiwa kusababishwa na kucheleweshewa huduma.
Uamuzi huo alifanya baada ya kupokea malalamiko ya kutoka kwa Seleman Makuani, ambate alidai mke wake Zaituni Mayuga alipoteza maisha baada ya kucheleweshewa huduma akitakiwa kutoa sh. 180,000 kujaza mafuta gari la wagonjwa (ambulance) litakalomsafirisha mkewe kwenda Hospitali ya Mtakatifu Kizito, Mikumi.
Akielezea uamuzi huo Shaka ambaye alilazimika kukatisha mkutano wa kusikiliza kero za wananchi katika Kata na Kijiji cha Kidodi, juzi, alisema lengo lake ni kubaini ukweli ili haki iweze kutendeka itakapobidi sheria ichukue mkondo wake ili kukomesha matukio ambayo yanaondoa huruma, utu na ubinadamu.
Katika mkutano huo wa hadhara Familia ya Marehemu kupitia kwa Makuani (Mume wa marehemu) alidai mke wake alicheleweshewa huduma ya kusafirishwa kutoka Kituo cha Afya Kidodi kwenda Hospitali ya Mtakatifu Kizito.
Makuani alidai ucheleweshwaji huo ulitokana na kukosa sh. 180,000 alizotakiwa kutoa kwa mafuta ya gari la kusafirisha wagonjwa baada ya kupewa rufaa kutoka katika kituo hicho cha afya kwenda Mikumi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Makuani, walipatiwa huduma hiyo ya baada ya kutoa sh. 100,000 ndipo aliposafirishwa lakini muda mrefu ukiwa umepita.
“Makuani alilalamika mke wake kucheleweshwa kupatiwa usafiri wa gari la wagonjwa kwa kukosa fedha hiyo katika Kituo cha Afya Kidodi baada ya kupewa rufaa hadi alipotoa sh. 100,000 ndipo akapatiwa usafiri huo na badaye kufariki dunia baada ya kufikishwa Mtakatifu Kizito Mikumi zaidi ya saa tano tangu afikishwe katika kituo hicho cha afya,” alisema.
Kutokana na malalamiko hayo Shaka alilazimika kusitisha mkutano wa hadhara kwa muda alipokuwa akisikiliza kero za wananchi na kulazimika kuitisha kikao cha kamati ya usalama ya wilaya kwa dharura kutafakari kadhia hiyo na kuja na majibu ambayo wananchi waliyapokea, kuridhia na kuyafurahia.
Shaka aliipa siku tatu kamati hiyo inayoundwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo kutoka vyombo vya ulinzi na Usalama kwa kuitaka kuchunguza jambo hilo na kumkabidhi ripoti yake ndani ya siku tatu ambapo kamati imeanza kazi rasmi siku hiyo hiyo jioni na ripoti itaakabidhiwa na kutolewa na mkuu wa Wilaya siku ya Ijumaa.
0 Comments