HABARI PICHA / DOTTO MWAIBALE NA PHILEMON SOLOMON
( 0744 362990 )
MJUMBE wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
(INEC), Dkt. Zakia Abubakar amewataka Maafisa Uandikishaji Ngazi ya Jimbo,
Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa Teknolojia ya Habari (TEHAMA) wa
Halmashauri kuzingatia maelekezo yote yatakayo tolewa na Tume ili waweza
kufanya kazi kwa wakati pindi zoezi la uandikishaji wapiga kura kwenye Daftari
la Kudumu litakapoanza.
Dkt. Abubakar ameyasema hayo wakati akifungua
mafunzo kwa watendaji hao ngazi ya mkoa kuhusu uboreshaji wa Daftrai la Kudumu
la Wapiga Kura kwa maafisa waliotajwa hapo juu mafunzo yaliyoanza Septemba 14,
2024 katika Ukumbi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida.
“Matokeo bora ya zoezi hili yatategemea uwepo
wa ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji Serikali, Vyama vya
Siasa na Wadau wengine wa uchaguzi,” alisema Abubakar.
Abubakar aliwasihi maafisa hao kuwa na
ushirikiano wa karibu na Tume wakati wote ambao watakuwa wakitekeleza majukumu
yao na watakapokuwa na jambo ambalo
watahitaji ufafanuzi au changamoto yoyote wasisite kuwasiliana na Tume,”
alisema Abubakar.
Mafunzo hayo yanawajengea umahiri wa
kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata ambapo nao watatoa
mafunzo hayo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi
ambao ndio watahusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
Aidha, Maafisa TEHAMA watapatiwa mafunzo
maalum ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi endapo
zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
“ Nimejulishwa kuwa, baadhi yenu mlibahatika
kushiriki katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za
Tume ikiwemo uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura katika awamu
zilizopita kwa kutumia uzoefu mlionao na mafunzo mtakayopatiwa, ninaamini
mtafanya kazi zenu kwa weledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi
hili,” alisema Dkt. Abubakar.
Dkt. Abubakar aliwasihi kutumia uzoefu
walionao kuwasaidia wenzao ambao hawakuwahi kushiriki katika zoezi kama hili
ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.Vilevile, wakati wa uboreshaji wa
Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya
kuandikisha wapiga kura.
Alisema jambo hilo ni muhimu kwani litasaidia
kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua
waombaji wa eneo husika, hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za
lazima.
Mawakala hao hawaruhusiwi kuwaingilia
watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni. Maelekezo zaidi
kuhusu mawakala wa vyama vya siasa yatatolewa na wakufunzi na ni muhimu
kuyazingatia.
Alisema kuwa Tume imetoa kibali cha kutoa
elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari kwa asasi za kiraia 157 na
asasi za kiraia 33 kwa ajili ya uangalizi wa zoezi hilo hivyo ni muhimu kutoa
ushirikiano kwa asasi hizo zitakapofika kwenye maeneo yao kwa ajili ya
kutekeleza majukumu yao na kuwa Tume itawapa vitambulisho kwa urahisi wa
kuwatambua.
Dkt. Abubakar aliwasisitizia maafisa hao
umuhimu wa kutekeleza majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo
utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa, vifaa hivvyo vimenunuliwa
kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya
uandikishaji nchini.
Alisema kutokuwa makini katika utunzaji wa
vifaa hivyo kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hilo muhimu
na kuwa wanapaswa kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili waweze kuyafanyia
kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza.
Mshiriki wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Ester Chaula amesema katika Mkoa wa Singida
wanategemea kuanza uboreshai wa Daftari la Wapiga Kura kuanzia Septemba 25,
2024 hadi Oktoba 1, 2024 ambalo litafanyika mkoa mzima.
Alisema katika Wilaya ya Singida zoezi hilo litafanyika katika vituo 167 kwenye jimbo moja la uchaguzi lenye kata 21 na kuwa maandalizi yote yamekamilika.
0 Comments