DKT. KIPESHA MKURUGENZI TEA, ANAYEFANYA MABORESHO MAKUBWA YA MIUNDOMBINU MASHULENI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, October 23, 2024

DKT. KIPESHA MKURUGENZI TEA, ANAYEFANYA MABORESHO MAKUBWA YA MIUNDOMBINU MASHULENI

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dkt. Erasmus Kipesha akizungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Mamlaka hiyo.

--------------------------------------------------------------------

BIDII ya kazi na uzalendo inatajwa kuwa ni moja ya nguzo inayomfanya mtu kusonga mbele katika hatua ya maendeleo yake binafsi na Taifa kwa ujumla hali ambayo tunaiona katika baadhi ya mataifa makubwa kama China ilivyofanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kutokana na watu wake kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa bidii.

Ili kurahisisha utendaji wa kazi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeunda Taasisi mbalimbali na kuweka wasimamizi lengo likiwa ni kuharakisha maendeleo ya nchi hususani yanayowahusu wananchi katika sekta mbalimbali kama vile elimu, ardhi, maji, umeme, afya na nyinginezo.

Wakuu wa taasisi hizo wengi wao wamekuwa wakipatikana kutokana na elimu zao, uzoefu wa kazi ambazo wamewahi kuzifanya aidha wakiwa chini ya viongozi wengine au kwa kuteuliwa moja kwa moja na mamlaka za juu.

Leo katika safu hii napenda kumzungumzia Dkt. Erasmus Kipesha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA). Binafsi namuita mzalendo ambaye anawiwa kuipeleka mbele elimu ya Tanzania kutokana na maboresho makubwa anayoyafanya kupitia mamlaka hiyo iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 8 ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001 kifungu cha 5(1) ikiwa na jukumu la kusimamia na kuratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa. TEA ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Niseme tu kuwa Dkt. Kipesha na timu yake wapo kazini na wamejipanga vilivyo kuhakikisha wana msaidia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuboresha miundombinu ya elimu nchini kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.

Dkt.Kipesha si mkuu wa taasisi hiyo aliyetoka nje bali alikuwa ndani ya taasisi hiyo akihudumu kama Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi hivyo anaijua vizuri na ndio maana kuteuliwa kwake kuwa Mkurugenzi imekuwa rahisi kwake kuwa na mikakati endelevu na kuchukua hatua za haraka kuitekeleza ili kuinua ubora wa elimu sambamba na uboreshaji wa miundombinu.

Kila mwenye macho anaweza kuwa shuhuda wa haya ninayosema hivi sasa kupitia TEA chini ya Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunaona maboresha makubwa ya miundombinu ya shule zetu hapa nchini kuanzia madarasa, matundu ya vyoo, wingi wa maabara za sayansi, mabweni ya wasichana na wavulana, nyumba za walimu hali ambayo imeongeza ufaulu wa wanafunzi kwenye shule nufaika.

Kazi hii kubwa inayofanywa na TEA chini ya Dkt. Kipesha na timu yake inapaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo hasa katika sekta ya elimu ambayo ni msingi mkubwa wa maisha ya mwanadamu.  Kutokana na maboresho haya makubwa yanayofanyika kwenye miundombinu ya elimu, ni vigumu kutofautisha mabweni ya wanafunzi wa shule za watu binafsi na Serikali. Hakika kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika. Pongezi nyingi kwa TEA na shukrani nyingi kwa Rais Samia kwa kutoa fedha za miradi hii.

Tabia ya Dkt. Kipesha ya kukutana na watendaji wenzake na kupokea maoni yao na kuyafanyia kazi ni moja ya jambo kubwa linalochochea ufanisi wa kazi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu.

Kufanya ziara za kwenda kushiriki maadhimisho mbalimbali kama yale ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yaliyofanyika Mei 26, 2024 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal Jijini Tanga yamekuwa yakichochea utendaji kazi wa mamlaka hiyo na wananchi kujua shughuli zinazofanywa na TEA.  

Kutoa nafasi kwa maafisa wa TEA kwenda kushiriki shughuli mbalimbali za nje kama walivyo kwenda baadhi yao kwenye Maadhimisho ya Kitaifa ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika Viwanja vya Chipukizi mkoani Tabora pia ina leta afya ya uwajibikaji kwa maofisa wa mamlaka hiyo.

Kushiriki kwake katika mafunzo elekezi kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi za umma ambayo yalifanyika Oktoba 7, 2024 katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Kibaha, mkoani Pwani yana muongezea uelewa zaidi na usimamizi mzuri wa taasisi yake na kutekeleza kwa umahiri majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali.  

 Dkt.  Kipesha katika kujua umuhimu wa vyombo vya habari kupitia  uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina  alikutana na  wajumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa lengo la kuelezea utekelezaji wa majukumu na mipango ya TEA katika kutoa huduma kwa umma kupitia ufadhili wa miundombinu ya elimu.

Akizugumza katika mkutano huo, Dkt. Kipesha alisema moja ya majukumu ya TEA ni utafutaji rasilimali kwa ajili ya Mfuko wa Elimu wa Taifa na kwamba njia mojawapo inayotumika katika jitihada hizo ni uandaaji wa maandiko ya miradi yatakayowezesha kupata fedha kutoka taasisi za ndani na nje ya nchi ili kusaidia uendelezaji wa miundombinu ya elimu.

Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2019/2020 hadi 2022/2023 jumla ya michango na ufadhili wa Sh.1.4 ilikusanywa na TEA kutoka kwa wadau mbali mbali ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Taasisi ya Asilia Giving inayojihusisha na shuguli za utalii Jijini Arusha pamoja na Taasisi ya Flaviana Matata.

Tunaiona kazi kubwa inayofanywa na TEA chini ya Dkt. Kipesha na timu yake kwenye sekta ya elimu na kuthibitisha haya, Oktoba 21 na 22, 2024 Menejimenti ya TEA chini yake imekutana kwa siku mbili kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye Mpango Mkakati wa Mamlaka hiyo wa miaka mitano (2021/2022 – 2025/2026). Tathmini inayolenga kubaini maeneo ya kuboresha na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake hasa utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu na kuzifikia shule nyingi zaidi. 

Katika kikao hicho cha kufanya tathmini, Dkt. Kipesha, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha majukumu ya TEA yanaenda sanjari na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, ambayo inalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kuwa bora, salama, na endelevu katika shule na vyuo. 

Nitakuwa mchoyo wa fadhira kama sitamtaja aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Bi. Bahati Geuzye ambaye ameaminiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kuona kazi kubwa aliyoifanya akiwa TEA na kumteua kwenda kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara ambaye kwa kiasi kikubwa amechangia maboresho makubwa katika sekta ya elimu hasa miundombinu na kuacha alama katika taasisi hiyo.

Bi. Geuzye akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Kipesha alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi ambapo chini ya uongozi wake mwaka jana, TEA ilipanga kutumia Sh. Bilioni 8 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu Nchini.

TEA ambayo ni miongoni mwa Taasisi za muungano kupitia Mfuko wa Elimu imetoa ufadhili wa Sh. Milioni 500 kwa ajili ya mradi wa ukarabati wa miundombinu pamoja na ununuzi wa vifaa vya kufuindishia na kujifunzia katika vyuo viwili vya elimu ya juu vilivyopo Tanzania Zanzibar.

Katika ufadhili huoTaasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST) ilipokea ufadhili wa Sh. Milioni 200 na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kampasi ya Benjamin Mkapa iliyopo Pemba ilipokea ufadhili wa Sh. Milioni 300, ufadhili huo umenufaisha wanafunzi 700 katika vyuo hivyo viwili.

Katika kuunga mkono serikali kuhamia Dodoma, TEA kupitia Mfuko wa Elimu ilifadhili miradi mikubwa miwili ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya ya msingi inayofundisha kwa lugha ya kiingereza ya Msangalele kwa thamani ya Sh. Milioni 750 katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Aidha mfuko ulifadhili ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu katika shule nne za msingi za Jijini Dodoma ambazo ni Kisasa, Kizota, Medelin A, Mlimwa C kwa thamani ya Sh bilioni 1.9

Hayo ni baadhi ya mafanikio makubwa ya TEA kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa lakini makubwa zaidi ya hayo yana kuja baada ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni kumteua Dkt. Leonard Akwilapo kuwa Mwenyekiti Bodi ya TEA.

Dkt. Akwilapo tuna mjua kuwa ni mchapakazi, mbunifu na mpenda maendeleo. Tunaamini TEA sasa ina kwenda kufanya vizuri zaidi kwa usimamizi wa Mwenyekiti huyo wa Bodi na wajumbe ushirikiano wa Menejimenti na watumishi wote kwa ujumla.

Mafanikio na kazi yote hii kubwa inatekelezwa na TEA chini ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni Chama Tawala.

Imeandaliwa na Dotto Mwaibale, (0754-36 2990)

Shule ya Serikali ya Mchepuo wa Kiingereza Msangalalee iliyojengwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa Jijini Dodoma.

Muonekano wa ndani wa Shule ya Msingi Msangalalee iliyopo Jijini Dodoma.
Muonekano wa vyumba vya madarasa Shule ya Msingi Urughu wilayani Iramba mkoani Singida vilivyojengwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.
Matundu 24 ya vyoo Shule ya Msingi Umwe iliyopo Wilayani Rufiji mkoani Pwani yaliyojengwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa.
Maabara ya Sayansi iliyojengwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa Shule ya Sekondari William Lukuvi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa mkoani Iringa.
Bweni lililojengwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa Shule ya Sekondari Mbomai iliyopo halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.
Muonekano wa bweni lililojengwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa Shule ya Sekondari Mbomai iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro. 
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad